2015-07-13 10:08:00

Mkimbilieni Bikira Maria wakati wa shida na raha; wakati wa mateso na majonzi!


Mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na bahari ya watu nchini Paraguay, Baba Mtakatifu Francisko, aliwaongoza waamini kusali kwa pamoja Sala ya Malaika wa Bwana kwa kumwelekea Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, kwa kuwazawadia watu wake Yesu Kristo. Waamini wanakumbushwa kwamba, Yesu alipokuwa ametundikwa pale juu Msalabani aliwakabidhi wafuasi wake Mama yake Bikira Maria; akawa ni Mama wakati wa Msalaba na mateso.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria ni mwombezi wa waamini mbele ya Yesu Kristo. Kama ilivyo kwa nchi nyingi Amerika ya Kusini, imani inawawajibisha kuonesha upendo wa dhati kwa Bikira Maria. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu nchini Paraguay kumkimbilia Bikira Maria kwa imani na matumaini; kwa kumfungulia hazina ya mioyo yao, ili kumshirikisha furaha na machungu ya maisha; matumaini na hali ya kukata tamaa wanayokabiliana nayo.

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa, anamwomba Bikira Maria aweze kulisimamia na kulilinda Kanisa; asaidie kuimarisha vifungo vya udugu kati ya Wakristo. Kwa njia ya msaada na maombezi ya Bikira Maria, waamini wote wanatambua kwamba, Kanisa ni nyumba ya wote; nyumba inayoweza kuwaonjesha watu ukarimu; nyumba ambayo ni Mama wa wote.

Mara baada ya Misa Takatifu na Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko aliondoka na kuelekea kwenye Makao makuu ya Ubalozi wa Vatican nchini Paraguay, ili kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay. Kwa pamoja wamepata nafasi ya kubadilishana mawazo, kama alivyofanya wakati alipokutana na Maaskofu kutoka Ecuador na Bolivia wakati wa hija yake Amerika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.