2015-07-12 11:46:00

Serikali ya Liberia kutunuku nishani maalum kwa Makanisa kwa kupambana na Ebola


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC linayapongeza Makanisa nchini Liberia kwa kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Liberia wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola tishio kubwa kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2015. Huu ni ugonjwa ambao umesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kwamba, itakuwa ni vigumu kwa wananchi wengi Afrika Magharibi kusahau madhara yake.

Kutokana na mchango wa Makanisa, Serikali ya Liberia imeamua hapo tarehe 17 Julai 2015 kutoa tuzo ya hali ya juu kwa Makanisa kwa kutambua mchango na huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ebola, ambao hadi sasa ni tishio kwa maisha ya watu. Makanisa yaliendesha kampeni ili kuwahamasisha watu kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ebola; yakatoa msaada wa hali na mali kwa waathirika kiasi hata cha wao wenyewe kuhatarisha maisha yao.

Mchungaji Georges Lemopoulos, Katibu mkuu mtendaji wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika barua ya shukrani na pongezi aliyomwandikia Mchungaji Dr. Kortu K. Brown anakaza kusema, Baraza la Makanisa Ulimwenguni linatambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Makanisa nchini Liberia, ushuhuda makini katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika huduma makini kwa wahitaji zaidi, watu waliovunjika na kupondeka moyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.