2015-07-12 10:44:00

Dr. John Pombe Magufuli kupeperusha bendera ya CCM uchaguzi mkuu 2015


Baada ya vuta ni kuvute; machozi ya uchungu na furaha kwenye mkutano mkuu wa kumi wa Chama cha Mapinduzi, C.C.M uliokuwa unafanyika Dodoma, kutoka majina 38 yakateuliwa majina matano na baadaye majina matatu ya makada yaliyochunjwa na hatimaye Dr. John Pombe Magufuli akaibuka kidedea, tayari kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu wa Rais unaotarajiwa kufanyika nchini Tanzania mwezi Oktoba 2015. Dr. Magufuli, alizaliwa kunako tarehe 29 Oktoba 1959. Dr. Mohamed Ali Shein ameteuliwa kuwa Mgombea wa CCM Zanzibar.

Lengo kuu ni kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; muungano na mafao ya watanzania wote. Makada na mashabiki wao, wamelizwa; lakini watanzania wengi wanasema, hapa CCM imeonesha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia, sauti na kilio cha watu kimesikiwa! Magufuli wengi wanasema, ni “Jembe zito”! Watanzania wanasubiri UKAWA waoneshe makali yao!

BALOZI AMINA SALUM ALI, Balozi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa. Yeye alikua na haya ya kusema: Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa na kufikia katika hatua hii ya viongozi wa Kamati Kuu kunipitisha jina langu katika tano bora hadi tatu bora kwa viwango vyote vilivyowekwa. Naomba nishukuru kwa moyo mkunjufu viongozi wote na wajumbe wa Mkutano kuu kuwa mwaka 2000 nilisimama kuomba ridhaa ya CCM kuomba Urais kupitia Zanzibar lakini kura hazikutosha.

 Naomba mwaka huu kura zitoshe. Leo nipo hapa nikiwa nimelelewa kimaadili na kiutendaji na viongozi wetu wa serikali iliyo na huruma kwa wananchi wake na nidhamu aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, Benjamin Mkapa na wewe Rais Kikwete, mlinilea na kunipa uweze. Mimi si mbinafsi wala sina makundi nitafanya kazi na wanachama wote tuliokuwa kwenye kinyang’anyiro, akiwemo Edward Lowassa. Nitafanyakazi nao. Naomba tutoke Dodoma tukiwa wanachama wamoja wa CCM.

Nitadumisha Muungano kwa kuwa na chama Imara na chenye viongozi imara wenye kudumisha umoja. Nakishuruku chama chetu kwa kutuwezesha wanawake kuzunguka mikoani kusaka wadhamini na kuwa na imani kwa kuweka nafasi katika nafasi za juu za uongozi. “Wakati ni huu na wajibu ni huu wa kunichagua ili niweze kuwawakilisha na wahikikishieni suala la amani na utulivu linadumishwa kwa kuungana, kushirikiana na kuaminiana,” alisema.

DK. ASHAROSE  MIGIRO, Waziri wa Katiba na Sheria alikuwa na haya ya kusema: Nina elimu ya Chuo Kikuu na baada ya kupata malezi ya CCM nimeshika nafasi mbalimbali kutoka balozi wa shina hadi Katibu Mwenezi. Nimelitumikia taifa katika ngazi ya waziri na elimu yangu nimeipatia hapa Tanzania ambapo nilipata fursa ya kufanya kazi mbali mbali za kimataifa. Nilikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kurudi nchini kuendelea kufanya kazi ndani ya chama. Nikipata fursa hii, nitasimamia umoja wa taifa letu, nitasimamia kuendelea kudumu kwa Muungano kwa mfumo wa serikali mbili na kulinda Mapinduzi ya Zanzibar na kuhakikisha tunapata Katiba nzuri.

DK.  JOHN POMBE MAGUFULI: Waziri wa ujenzi ana haya ya kusema: Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufika hapa, wewe (Mwenyekiti) na Chama changu kwa kunilea hadi kufikia hapa. Nimesimama hapa kuwaomba kura zenu. Ninawaomba kura kwa sababu ninaamini nitafanyakazi na nyinyi. Ninaamini kwamba mtanituma na nitakuwa mwakilishi wenu. Mkinichagua nitakilinda chama chetu na kuendelea kushika dola katika nchi hii.

Nitaulinda Muungano wan chi ulioasisiwa na waasisi wetu, akiwemo hayati Julius Kambarage Nyerere.  Chama cha Mapinduzi kimenilea na nina ahidi sitawaangusha. Nimefanyakazi katika kipindi chote cha miaka 10 cha Rais Kikwete. Nilifikiri utaniuliza kiwango cha barabara nilichotengeneza! Wanachama wenzangu nitafanyakazi na nyinyi bega kwa bega kwa kuzingatia yote. Kazi ya uongozi ni kupokezana vijiti. Kazi nzuri imefanywa na Nyerere, Karume, Mwinyi, Mkapa, na Kikwete. Nimejifunza vya kutosha katika kipindi hicho. Ninaahidi sitawaangusha na sasa ninavyosema wapinzani wote matumbo joto.

Maendeleo lazima yaletwe na chama na yataletwa na Chama cha Mapinduzi. Ninawashukuru wajumbe wote na mnitume niwawakilishe ili niweze kulisukuma gurudumu la ushindi. Mwenyekiti naomba kura yako, Makamu Mwenyekiti naomba kura yako, Kamati Kuu na Wajumbe wote naomba kura zenu nyingi ili kwa pamoja muweze kunipa jukumu la kunituma katika kazi hii. Mtakapo nichagua nitakwenda kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mungu ibariki CCM, Tanzania na Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa magezeti ya Tanzania. 








All the contents on this site are copyrighted ©.