2015-07-11 15:53:00

Ujio wa Papa Francisko ni kielelezo cha neema na baraka nchini Paraguay!


Viongozi wa kisiasa na watunga sera za maendeleo ya watu wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wananchi wa Paraguay wanapaswa kuanza mchakato wa upatanisho, haki na amani, ili kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuhakikisha kwamba, wanawake wanaheshimiwa na kuthaminiwa, kwani wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya Paraguay.

Umoja na udugu viwasaidie wananchi wa Paraguay kuponya madonda ya chuki na uhasama yaliyopelekea vita ya wenyewe kwa wenyewe. Utu na heshima ya binadamu ni kielelezo makini cha uchumi na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Haya ni mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake alipowasili nchini Paraguay, Ijumaa, tarehe 10 Julai 2015.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Edmundo Ponciano Valenzuela Mellid wa Jimbo kuu la AsunciĆ²n, Paraguay anakaza kusema, ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao ni zawadi, neema na baraka kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wamejiandaa kwa njia ya sala; wakaangalia historia na mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili na mwishoni, maandalizi yaliyojikita katika sadaka, furaha, imani, matumaini na mshikamano wa dhati, Familia ya Mungu nchini Paraguay imeshiriki kikamilifu katika maandalizi na hatimaye mapokezi makubwa kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu imekuwa ni fursa kwa waamini kuonja kwa mara nyingine tena huruma, upendo na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya Neno la Mungu, Maisha ya Sakramenti na Matendo ya huruma, mambo ambayo yamekaziwa kwa namna ya pekee wakati wa maandalizi na wakati Baba Mtakatifu alipowasili, ili kweli ujio wake uwe ni chemchemi ya neema na baraka: kiroho na kimwili.

Ujio wa Baba Mtakatifu umesaidia kuimarisha mshikamano, umoja na mapendo kati ya waamini. Umewaimarisha katika kuthamini, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kanisa litaendeleza majadiliano ya kitamaduni, kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Ni matumaini ya wengi kwamba, hii itakuwa pia ni fursa ya kuanza mchakato wa upatanisho miongoni mwa wanasiasa kwa kujikita katika majadiliano, ukweli, uwazi na mafao ya wengi sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, bila kusahau tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Paraguay ni nchi ambayo imebarikiwa na Mwenyezi Mungu kuwa rasilimali nyingi ambazo zikitumika barabara zinaweza kusaidia kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu ya wananchi wake. Kilimo na ufugaji ni sekta muhimu sana kwa uchumi na maendeleo ya wananchi wa Paraguay. Kilimo cha umwagiliaji kinaweza kusaidia kupambana na baa la njaa ndani na nje ya Paraguay. Kwa bahati mbaya, rushwa, ufisadi na ubinafsi ni kati ya mambo ambayo yanagumisha mchakato wa maendeleo ya watu. Rasilimali na utajiri wa nchi vikitumika vyema, Paraguay anasema Baba Mtakatifu inaweza kuwa ni Paradiso ya watu wake, lakini hii ni dhamana inayopaswa kufanyiwa kazi na wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.