2015-07-11 09:19:00

Papa awasili Paraguay na wito wa kipaumbele kwa Maskini


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni aliingia nchini Paraguay,  sehemu ya  mwisho ya ziara yake ndefu ya kitume , kutembelea mataifa matatu ya Amerika ya Kusini,  kama mhujaji na shahidi  wa Habari  Njema ya Upendo wa Kristo kwa watu wote. 

Pamoja na hali mbaya ya hewa , Papa alipokelewa kwa shangwe zote kitaifa. Mara baada ya  hafla fupi ya mapokezi katika uwanja wa Kimataifa wa Asuncion wa Paraguay, ambako watoto walimpamba kwa shada la maua kwa utamaduni wao, kwa muda mfupi alipumzika katika chumba kilichokuwa kimeandaliwa  akiwa na mwenyeji wake Rais  Horacio Manuel Cartes Jara, na baadaye kwenda Ikulu, ambako  maofisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Paraguay  walitambulishwa  kwake. Akiwa Ikulu pia alibadilishana zawadi na mwenyeji wake.

Baadaye Papa akiwa katika viwanja vya Ikulu, aliwahutubia viongozi wa serikali na wanasiasa ambamo alianza kwa kutoa shukurani kwa  mapokezi  mazuri na kwa  ukarimu wao. Lakini mara alikumbuka uchungu historia ya Paraguay kati ya '800 na' 900 ambayo ilikuwa ni miaka ya mateso ya kutisha ya vita, migawanyiko, ukosefu wa uhuru na ukiukaji wa haki za binadamu.

Alikitaja  kipindi hicho kwamba ilikuwa ni wakati wa uchungu mkuu  na vifo vya kutisha.  Lakini basi baadaye  ushindi uliweza kupatikana kwa kujenga tena  moyo wa mshikamano  kwa watu Paraguay,na hivyo kuzishinda taabu nyingi na mateso na kuendelea ujenzi wa taifa, jitihada zilizo letea taifa amani na mafanikio.

Aliendelea kuzungumzia  migogoro ya zamani na nchi nyingine za Amerika Kusini, na kutoa shukurani na pongezi kwa wanawake wa  Paraguay ambao, waliweza simama imara katika kutoa jibu  la kusitisha mauaji  ya watu wao, katika vita hivyo vya dhuluma, vilivyofanya maafa na uharibifu makubwa kwa  watu wa taifa hilo.  Papa kwa masikitiko aliendelea kujali jinsi mabegani mwao, hao akina  mama, wake na wajane walivyotenda kwa ujasiri mkubwa na kuweza kuendeleza familia zao na nchi yao,  na kurejesha katika kizazi cha vijana matumaini bora kwa  siku za baadaye . Papa alieleza na  kuwaombea Baraka za Mungu wanawake wa  Paraguay, taifa tukufu sana Amerika ya Kusini.

Papa  akiendelea kuutazama uchungu  na madhara ya vita, na kukemea  mawazo yote yanayoweza zua vita akisema , kamwe pasiwe na vita na madhulumu dhidi ya haki na  hisia zote za kutaka kulipiza kisasi na chuki na  upuuzi wote wa vita. Pasiwe tena  kinyongo na chuki na kati ya ndugu! Daima, kizazi hiki chetu na cha baadaye iwe ni kujenga amani zaidi!  Amani siku hadi siku. Amani  katika maisha ya kila siku, kwa watu wote iwe hivyo. , Daima na iwe kuepuka vishawishi vyote vya kujenga  kiburi, maneno ya kukera na ufedhuli. Badala yake na iwe  kuendeleza ufahamu kupitia njia ya  mazungumzo na ushirikiano.

Hotuba ya Papa iliendelea kuutaka uongozi wa kiserikali na wanasiasa na watu wote , kutoa kipaumbele kwa maskini, kama ambavyo imekuwa sifa ya taifa la Paraguay kwa muda wa miaka kadhaa, kuendeleza nia ya kujenga demokrasia imara,  kupambana na rushwa, na kuhamasisha miundo na taasisi imara za kidemokrasia. Papa amehimiza  kuepuka majaribu yoyote yanayotaka kumomonyoa demokrasia rasmi. Pia amehimiza uimarishaji wa majadiliano kama njia  pekee ya kukuza manufaa ya wote, kwa kuzingatia utamaduni wa kuheshimiana , na  utambuzi wa tofauti halali na maoni ya wengine, kama njia ya kuondokana na migogoro na mgawanyiko wa kiitikadi.

Papa amesema "hadhi ya wanyonge ni kipimo cha mfumo wa kiuchumi!” Na kwamba, ni lazima kuheshimu  utu  wa binadamu, hasa wanaoishi katika mazingira magumu zaidi na wasioweza jitetea   Papa ameonyesha kufurahia ushirikiano wa Kanisa Katoliki kwa taasisi zinazo tetea haki na umoja wa kijamii, akisema huo ni mwanga unaomulika njia ya huruma wazi ya Kristo kwa watu wote. Na kutenda kwa  haki, hujenga upendo ulio imara zaidi kati ya mtu na mtu , na hivyo  kufuta moyoni  chuki na wivu usiokuwa na maana. Na hakuna anayeachwa nje au kupuuzwa katika mipango yote ya Kijamii, Papa amesisitizia watawala na wasiasa Paraguay.








All the contents on this site are copyrighted ©.