2015-07-11 10:51:00

Mnaalikwa kuyatafakari na kuyamwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, tunakusalimu Tumsifu Yesu Kristo. Kukukumbusha tu mpendwa msikilizaji, tunaendelea kuuchambua waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko ujulikanao kwa jina la Misericordiae vultus yaani uso wa huruma, maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Tunakazia maarifa: Jubilei hiyo itazinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko Katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican hapo tarehe 08 Desemba 2015 katika Sherehe ya kukingiwa dhambi ya asili Mama yetu Bikira Maria, na itahitimishwa katika Sherehe ya Kristo Mfalme 2016.

 

Mpendwa msikilizaji, usipitwe! Kwa ufahamu zaidi wa mambo haya, sikiliza Radio Vatican, ili usaidiwe kufikiri na Kanisa, kwenda na Kanisa, na kuishi ndani ya Kanisa, safina ya Mungu inayotupeleka katika Bandari salama.

Katika mwaka huo Mtakatifu wa Jubilei tunaoelekea kuuadhimisha, Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine mengi, analialika Kanisa ‘kurudi kwenye misingi’, na mmoja ya hiyo misingi ni kuhubiri na kuiishi huruma, inayomwilika katika matendo ya huruma. Na leo anatupatia mwanga wa yale ambayo Kanisa linatarajiwa kufanya katika mwaka huo wa Jubilei akisema: Kanisa lijiandae kufanya mambo mazito katika mwaka mtakatifu wa jubilei ya huruma ya mungu. Na dira yetu katika kuuishi mwaka huo, si kitu kingine bali ni Neno la Kristo Mwenyewe kama tusomavyo katika Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, tunataka kuuishi mwaka huo wa Jubilei kwa maneno ya Bwana mwenyewe asemapo “Iweni na huruma kama baba yenu wa Mbinguni alivyo na huruma”. (Lk. 6:36). Huo ni mpango wa maisha, wenye wajibu wake, lakini umejaa furaha na amani.  Amri hii ya Bwana anaielekeza kwa wote waliotayari kulisikiliza neno la Mungu. Hii ina maana kwamba, tunahitaji kung’amua uzuri wa unyamavu ili kuweza kulitafakari Neno linalokuja kwetu. Ni kwa njia hiyo tu itakuwa rahisi kuitafakari huruma ya Mungu na kuiweka katika mfumo wa maisha yetu ya kila siku.

Baba Mtakatifu anasisitiza tena juu ya hija katika mwaka huo wa Jubilei, na kwamba Hija hiyo inawakilisha safari ya maisha ambayo kila mmoja wetu huifanya katika maisha ya hapa duniani. Maisha yenyewe ni hija, na mwanadamu ni mhaji, msafiri anayesafiri kuelekea lengo-ukomo wa maisha yake. Mwaliko kwa waamini wote na wote Wanaompenda Mungu, kujiandaa vema, kutenga muda kwa ajili ya kufanya hija hiyo kwa tafakari ya kina juu ya maisha binafsi. Naye Mungu wa amani awajaalie safari salama ya maisha  wahaji wote.

Baba Mtakatifu anatualika daima tuombe msaada wa Mungu katika maisha yetu, kama Kanisa lisalivyo katika litirujia ya vipindi “Ee Mungu unielekezee msaada, ee Bwana unisaidie hima”. Kwa huruma Mungu wetu huja kutusaidia katika udhaifu wetu. Na msaada huo upo katika kutusaidia sisi kutambua uwepo wake na kuukubali ukaribu wake kwetu sisi. Ni mwaliko kwetu sote, jinsi ambavyo siku kwa siku tunaguswa na huruma yake, sisi nasi tuwe na huruma kwa wenzetu pia.

Katika mwaka huo mtakatifu, tunatarajiwa kuifungua mioyo yetu kuwatazama wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; hali ambayo jamii ya kisasa inajiundia yenyewe. Tazama, kuna hali za aina ngapi za mashakamashaka na aina ngapi za mateso katika jamii ya leo! Anahoji Baba Mtakatifu. Kuna majeraha mangapi katika miili ya wale masikini wasio na sauti; kwa sababu kilio chao kinanyamazishwa na kupuuzwa kutokana na kutojali kwa wale walio matajiri?

Katika Jubilei hiyo, Kanisa litaalikwa zaidi na zaidi kuyaganga majeraha hayo, kuyafuta majeraha hayo kwa matuta ya faraja, kuyafunga kwa huruma na kuyaponya kwa roho ya umoja na uangalizi mkubwa. Baba Mtakatifu anaonya, tukwepe kabisa kishawishi cha kudondoka katika hali ya kutokujali, au kung’angania tu mifumo ambayo inatuzuia sisi kugundua mambo mapya. Badala yake tufutilie mbali kabisa mashaka yasiotusaidia kitu. Tuyafumbue macho yetu kutazama mateso na mahangaiko ya dunia yetu hii; tuyatazame majeraha ya kaka na dada zetu wanaodhalilishwa utu wao, na tutambue kwamba tunawajibika kusikiliza kilio chao cha kuomba msaada. 

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tunapaswa kutoka nje, na kuwasaidia, ili walionje joto la uwepo wetu wa upendo, urafiki wetu na udugu wetu. Kilio chao kiwe kilio chetu, na sote kwa pamoja tushirikiane kuvunja vizingiti vya ubaridi na kutojali ambavyo mara nyingi vinatutawala  na ndanimwe vinaficha unafiki na ubinafsi mkubwa.

Anasema Baba Mtakatifu, “ni hamu inayowaka moyoni mwangu kwamba katika Mwaka huo mtakatifu wa jubilee, Wakristo wote wayatafakari sana matendo ya huruma ya kiroho na ya kimwili. Kwa njia hiyo, tutaamsha dhamiri zetu, ambazo daima zinabutushwa mbele ya umasikini. Na tuzame zaidi katika moyo wa Injili ambapo Maskini wana mang’amuzi ya pekee ya huruma ya Mungu”.

Kristo Bwana katika mafundisho yake anatuelekeza katika hayo matendo ya huruma, ili tujue kama kweli tunaishi kama wafuasi  wake au la! Matendo hayo ya huruma ya kimwili ni:- kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuwaponya wagonjwa, kuwatembelea wafungwa na kuwazika wafu. Na matendo ya huruma ya kiroho ni:-  kuwashauri wenye mashaka, kuwaelekeza wasiojua, kuwaonya wadhambi, kuwafariji walioonewa, kuwasamehe wakosefu, kuwavumilia wakorofi na wasumbufu, kuwaombea wazima na wafu. Baba Mtakatifu anamalizia kipengele hiki kwa kusema “hatuwezi kukwepa maneno hayo ya Bwana kwetu sisi. Hayo yatakuwa ndiyo vigezo vya hukumu yetu ya mwisho”. Kwa mantiki hiyo anatualika sote kutafakari kwa kina matendo hayo ya huruma ya kiroho na kimwili.

Mpendwa, msikilizaji kwa leo tunakuacha na matendo hayo ya huruma ambayo yapo saba kwa saba, yaani matendo saba ya huruma ya kimwili na matendo saba ya huruma ya kiroho. Huruma ya Mungu inatuinua sisi mwili na roho, na hivyo tunatumwa kuyamwilisha matendo hayo kimwili na kiroho. Huku tukiendelea kutafakari hayo matendo saba kwa saba, tunakutakia usikilizaji mwema wa vipindi vyetu.

Hadi wakati mwingine tena, Ninayekuaga kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.