2015-07-11 14:07:00

Mkutano wa uchumi na maendeleo Addis Ababa ulenge kupambana na umaskini


Kardinali Antonio Luis Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanapunguza ubinafsi na utaifa kwa kujikita katika mchakato unaowashirikisha watu wengi zaidi katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati ya maendeleo endelevu.

Kardinali Tagle anayasema haya wakati viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanajiandaa kuanza mkutano wa tatu kimataifa unaozungumzia kuhusu fedha na uchumi, utakaofungulia mjini Addis Ababa kuanzia tarehe 13 hadi 16 Julai 2015. Kanisa Katoliki katika mkutano huu linawakilishwa na Caritas Internationalis, Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Walles, CAFOD, Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, Sècours Catholique Francese na Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana, Caritas Ghana.

Kardinali Tagle anakaza kusema, ni wajibu wa kimaadili kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa kupambana na baa la umaskini duniani, kwa kujikita katika: haki, kanuni msingi na mchakato unaowashirikisha watu wengi zaidi katika kuamua, kupanga na kutekeleza. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na ugawaji na matumizi sawa ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanayo dhamana pia kudhibiti vitendo vinavyohatarisha umoja, mshikamano na mfungamano wa kijamii, ili kuharakisha mchakato wa kupambana na baa la umaskini duniani.

Mkutano wa fedha na uchumi unaofanyika mjini Addis Ababa unawashirikisha wadau na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wanaochambua na kupembua kwa kina na mapana mafanikio, matatizo, na changamoto zilizopo katika mchakato wa kupambana na baa la umaskini, mintarafu Malengo ya Maendeleo ya Millenia na kadiri ya sera zilizokuwa zimepitishwa kwenye mkutano wa maendeleo endelevu uliofanyika huko Monterrey, Canada.

Hapa kwa mara ya kwanza, kulianzishwa jukwaa la mshikamano kati ya Nchi tajiri duniani na nchi zinazoendelea ili kushirikiana katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia; jambo lililokaziwa pia kwenye Mkutano wa Doha, uliofanyika kunako mwaka 2008. Mkutano wa Addis Ababa una dhamana ya kupembua kwa namna ya pekee, vikwazo na vizingiti vinavyoendelea kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu pamoja na kuangalia changamoto zinazoendelea kuibuliwa kwa sasa, ili kudhibiti masuala ya fedha na kuendeleza sera za maendeleo endelevu.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Kardinali Tagle bado inaendelea kuponya madonda ya mtikisiko wa uchumi kimataifa uliosababishwa  na uchumi kuegemea sana kwenye masuala ya fedha na kusahau kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Hapa kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya wa sera na mikakati ya kiuchumi inayojikita katika masuala ya kijamii badala ya mtindo uliowekeza zaidi katika masuala ya fedha kwenye sekta binafsi na matokeo yake hadi leo hii watu wanaendelea kuathirika kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Caritas Internationalis inawataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuondokana na ubinafsi, utaifa na masilahi ya muda mfupi na badala yake kujielekeza zaidi katika sera zinazowahusisha watu wengi zaidi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Kimataifa, G20 na OECD ni Jumuiya ambazo zimekuwa na mwelekeo tenge kidogo kuhusiana na mchakato wa maendeleo endelevu. Jumuiya ya Kimataifa itoe kipaumbele cha pekee kwa ajili maendeleo endelevu na mchakato wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, yanayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika janga la umaskini wa hali na kipato.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.