2015-07-10 09:16:00

Uongozi ni huduma na dhamana! Watu wanataka amani na utulivu!


Askofu mkuu Edmundo Ponziano Valenzuela wa Jimbo kuu la Asunciòn, Paraguay anaitaka Familia ya Mungu nchini humo, lakini kwa namna ya pekee kabisa wanasiasa kuhakikisha kwamba wanatibu na kuganga saratani ya rushwa na ufisadi inayoendelea kutesa mamillioni ya watu wasiokuwa na hatia. Wanasiasa wakomeshe tabia chafu ya kutumia madaraka ovyo kwa ajili ya mafao ya binafsi kwa kukumbuka kwamba, uongozi ni huduma na dhamana. Umefika wakati kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba, kuna ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao.

Askofu mkuu Valenzuela anasema kwamba, wananchi wengi wamechoshwa na mambo haya ambayo kimsingi ni dalili za kumong’onyoka kwa maadili na utu wema na badala yake, wanataka kuona nchi inajikita katika kanuni maadili; utu wema sanjari na kuendelea kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Hapa ni mahali ambapo kila mwanafamilia anaheshimiwa na kuthaminiwa pamoja na kupewa haki zake msingi.

Familia ya Mungu nchini Paraguay imechoka kusikia mtutu wa bunduki ukirindima kila kukicha; haki msingi za binadamu zikitelekezwa kana kwamba hakuna utawala wa sheria. Mambo yote haya yanapaswa kusafishwa, ili nchi iweze kuwa safi, kimaadili na kiutu; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Viongozi wa Serikali waachane na tabia ya kutumia vibaya dhamana na madaraka yao, na badala yake wajielekeze katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa.

Licha ya magumu na kinzani hizi zinazojitokeza nchini Paraguay, lakini pia kuna dalili njema ambazo zinapaswa kuungwa mkono na wapenda haki, maendeleo na amani. Kuna haja wanasema Maaskofu kupanga na kuchagua vipaumbele, kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu; mambo yatakayofanyiwa kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Paraguay. Wananchi wasimame kidete na kamwe wasikubali kuyumbishwa na mielekeo ya mmong’onyoko wa kimaadili na tunu msingi za maisha. Wawe imara dhidi ya rushwa na  ufisadi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.