2015-07-10 16:54:00

Papa asema ;gereza ni mchakato wa kurejesha upya utambulisho uliopotea.


Baba Matakatifu Francisko, katika siku yake ya sita  ziarani  Amerika ya Kusini, akiwa  Bolivia,  Ijumaa tarehe 10 Julai 2015 majira ya asubuhi,  ameandika historia mpya kama Khalifa wa Mtume Petro kwa kutembelea Gereza la  Mtakatifu Santa Cruz la Palmasola. Papa kwa upendo mkuu akihutubia  gerezani hapo amesema, asingefurahia kuondoka  Bolivia bila ya kusalimia wafungwa, kushirikishana nao  imani matumaini na matunda ya upendo wa Yesu juu ya msalaba.

Na hivyo alishukuru kwa makaribisho mazuri  hasa kwa maneno ya Askofu Mkuu Jesús Juárez na ushuhuda uchungu wa  maumivu yenye kukandamiza matumaini  ya kina katika  moyo wa binadamu, na jinsi maisha yanavyoendelea kuwa magumu  hata katika  kutafuta nguvu mpya hasa katikati ya matatizo yanayowakabili.

Papa amewashuhudia kwamba, yeye aliyesimama mbele yao ni yeye yule mwenye kuwa na uzoefu katika kusamehewa. Ni yeye aliyekuwa mkosefu na sasa amesamehewa dhambi zake nyingi . Hana jingine la zaidi la kuwapa , lakini kushirikishana nao kile alichokifanya yeye na kile anachokipenda, naye ni Yesu Kristo , Baba wa Huruma.

Papa aliendelea kuzungumzia  upendo alionao Mungu kwetu . Kwako wewe na kwangu mimi. Ameutaja kuwa ni upendo wenye uwezo na halisi. Ni upendo wenye uwezo wa kuondoa shida na taabu kwa wale wanaompenda Mungu. Ni upendo wenye kuponya , kusamehe na kumwinua mtu katika unyonge wake wenye kujali  kila hali ya mtu. Na kwamba ni upendo uliokaribu na hurejesha upya heshima , kwa kuwa kuna njia nyingi zinazoweza kusababisha mtu kupoteza heshima yake. Lakini Yesu anatenda kinyume, kwa kuyatoa maisha yake mwenyewe kwa ajili ya kurudisha upya utambulisho wetu tuliopoteza.

Papa aliendelea kuwatia  moyo na kuwashirikisha uzuri wa upendo huu wa Yesu, akisema "hata  Petro na Paulo , wafuasi wa Yesu  waliwekwa jela pia. Pia wao walipoteza uhuru wao. Lakini kuna kitu kilichowadumisha , kitu kilicho wafanya wasipoteze imani yao, au kudhoofishwa na kipindi hicho cha giza na kisichokuwa na maana. Jambo lililowadumisha ni sala binafsi na sala za pamoja. Walisali , na kuombeana mmoja kwa mwingine. Mfumo huu wa sala ni  mfumo wenye kudumisha maisha na  tumaini. Ni mfumo wa maisha unaowezesha ujasiri wa kutokata tamaa, lakini huhimiza kusonga mbele .  Sala ni mfumo wenye  kusaidia maisha , si kwetu wenyewe tu lakini pia kwa familia"alisisitiza .

Papa aliendelea kuwatia moyo wafungwa kwamba , “wakati Yesu anapokuwa sehemu ya maisha yetu , hatuwezi tena kubaki ndani ya kifungo cha hali zetu zilizopita. Badala yake tunaanza kutazama siku za mbele  kwa maoni mapya  tofauti , kuwa na mtazamo tofauti  wa maisha na matumaini. Badala ya kubaki katika  giza nene la siku za nyuma , tunakuwa na uwezo wa kumwaga machozi na kutafuta ndani yake nguvu ya kufanya mwanzo mpya.  Wakati  tunapo kabiliwa na huzuni na  hisia hasi, tunamwangalia Kristo aliyesulubiwa.  Katika kuitazama sana sura yake, katika macho yake kuna mahali kwa ajili yetu. Na hivyo sote tunaweza kuleta kwa Kristo,  majeraha yetu, maumivu yetu na  dhambi zetu. Katika majeraha yake, kuna nafasi kwa ajili ya majeraha yetu wenyewe.  Kuna uwezo wa kurudia tena furaha,  kuburudika, na kuwa safi. Kubadilishwa na kupona. Yeye alikufa kwa ajili yetu, kwa ajili yangu na kwa ajili yako.

Papa alihimiza maungamo ya kweli , mbele ya wawakilishi wake Mapadre wanaowatembelea katika gereza hilo akisema, "Mkono wa Yesu  wenye uwezo wote upo tayari kwetu sote kutuinua juu, iwapo tutaungama dhambi zetu kwa wawakilishi wake , Mapadre . Ni kuzungumza nao na kufanya mabadiliko ya moyo! Yesu yu tayari kumsaidia kila mmoja kunyanyuka  daima."

Papa aliongeza kufungwa , kuswekwa jela haina maana ya kufungia nje kila jambo,  bali kuwekwa kifungoni  au kuwa kizuizini ni sehemu ya mchakato unaotafuta kumrejeshea mfungwa muungano mpya na jamii. Maelezo ya Papa pia yalionyesha kutambua mambo mengi yanayofanya maisha kwa wafungwa kuwa magumu , ikiwemo msongamano, ucheleweshwaji wa kesi kusikilizwa na haki kutendeka, ukosefu wa fursa za mafunzo na sera za ukarabati, pamoja na vurugu. Yote haya kwa hakika inakuwa ni hoja ya kidharura inayodai ufanisi  na ushirikiano kati ya taasisi ili kupata ufumbuzi. Hata hivyo wakati hayo yanafanyiwa kazi , hatupaswi kukata tamaa kwamba yote ni bure. Kuna mambo ambayo yanayoweza fanyika  hata leo.

Papa aliendelea kuwatia moyo kwamba , hapo walipo katika kituo hicho cha ukarabati, hali ya maisha yao ya pamoja , kwa kiasi fulani yanategemea sana wao wenyewe. Akaonya  mateso na madhulumu yanaweza jenga moyo wa ubinafsi wenye kuongoza katika mizozo na mapambano,  lakini pia ni wao hao  pia wanauwezo wa kupafanya mahali hapo kuwa mahali pa salama na nafasi ya kujenga  udugu wa kweli. Ni mahali na kusaidiana kujenga moyo wa udugu na ushirikiano, badala ya  ubinafsi, mgawanyiko na magenge, Papa alieleza na kuwasihi waendelee na utendaji wenye kujali  hali njema kwa wote.

Na aliwaomba wote wafikishe salaam zake za dhati kwa familia zao, bila kusahau kwamba uwepo na msaada wao  ni muhimu sana. Mababu, baba, mama, ndugu, dada, wanandoa, watoto: wao wote hukumbusha thamani ya maisha tunayopaswa kuitunza na kuitetea daima kwa ajili ya uwepo wa ulimwengu ulio bora.

Hatimaye, Papa alitoa neno  la kuwatia nguvu watumishi katika gereza hilo , wasimamizi wa utawala, maofisa wa polisi, na wafanyakazi wengine wote akisema, kazi zao ni muhimu katika  utumishi wa umma. Wana wajibu muhimu kwa ajili ya kuwezesha mchakato wa kuwaunganisha wafungwa na jamii. Ni wajibu wao  kumwinua mtu na si kumgandamiza chini, kurejesha hadhi na si kutesa; kuhimiza na si kuleta ugumu wa maisha. Hii ina maana kuweka kando mawazo yenye kuona mazuri au mabaya wa mtu, lakini  lakini badala yake, ni kulenga katika kuwasaidia wengine. Hili litasaidia kujenga mazingira bora kwa kila mtu. Itawezesha uwepo wa  heshima, na kutoa motisha kwa wote kuonekana  watu wote bora.

Papa kabla ya kutoa baraka zake, aliwasihi kwa muda wa dakika kadhaa wawe katika ukimya wa sala. Na aliwaomba waendelee pia kumwombea kwa sababu pia hufanya makosa na hivyo anapaswa pia kufanya toba.

Katika gereza hilo, Papa  alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Gereza akiwepo pia Kasisi wa Gereza na  Mons. Jesus Juàrez Pàrraga  , Askofu Mkuu wa Sucre , na Rais wa kazi za Kichungaji  kwa ajili ya misaada ya kanisa na kazi za Kichungaji kwa ajili ya wafungwa magerezani. 

Askofu Mkuu Jesus , akimkaribisha Papa  Francisco katika gereza hilo la Palmasola, amesema kwa hakika, Papa ametimiza kweli Maneno ya Yesu aliposema "Mimi nilikuwa gerezani na ukaja nitazama " (Mt 25, 35 ff.) Na kwamba , uwepo wa  Papa Francisco imekuwa ishara kubwa ya ukweli wa ujumbe wake unaolenga kujenga  kwa karibu udugu, mshikamano na haki. Na kwamba, wao wanaungana na Papa katika imani na tumaini: kama Neno la Mungu linavyosema,  "Hakuna anayeweza kututenga na upendo wa Mungu!  Na wala  kuta za gereza, haziwezi kuwatenganisha watu na Mungu.  Na hivyo Askofu Mkuu Juàrez Parraga, kwa niaba ya wote alitoa maneno ya shukurani kwa Papa kwa kuwa nao na walimpokea kwa upendo mkuu na kumtakia mema mengi.  

 








All the contents on this site are copyrighted ©.