2015-07-10 14:59:00

Mwenyezi Mungu anapaswa kuwa yote katika yote!


Vyote anavyomiliki mwanadamu vinatoka kwa Mungu na vinapaswa kuongozwa na hekima ya Mungu itokayo juu. Sisi sote ni watoto wa Mungu, shughuli zetu na vyote tunavyomiliki ni tunu tulizopokea kutoka kwake na tunaalikwa kumrudishia kwa sifa na shukrani. Kwa utangulizi huu mfupi napenda kukualika katika tafakari ya Neno la Mungu tunapoadhimisha Dominika ya 15 ya Mwaka B wa Kanisa.

Katika somo la kwanza Nabii Amosi anakataliwa na Amazia mfalme wa Israeli. “Ewe mwona, nenda zako, ikimbilie nchi ya Yuda, ukale mkate huko, ukatabiri huko; lakini usitabiri tena huku Betheli; kwa maana ni mahali patakatifu pa mfalme”. Neno la Mungu kupitia kinywa cha Nabii Amosi linawachoma. Watawala wa Israeli pamoja na makuhani wa kipindi hiki cha Nabii Amosi wamekuwa katika hali ya starehe na anasa na kuwanyonya wanyonge.

Nabii Amosi anapowakemea na kuwakumbusha wajibu wao kama viongozi wa kijamii anaonekana kuweka kiwingu. Ni wawakilishi wa jamii ambayo wanatafuta kula “bata” kwa namna yoyote ile. Wajibu anaopewa mwanadamu wa kuwaongoza na kuwapatia wenzake anaowaongoza mahitaji yao ya lazima unawekwa kando na kubaki kujikita katika starehe binafsi. Mwanadamu anasahau kuwa madaraka hayo na utawala amepewa kutoka juu kwa ajili ya ustawi wa maisha ya kijamii.

Mwanadamu anaanza kujitwika yasiyo yake. Anathubutu kupaita mahali patakatifu kwa nafsi yake. “Hapa ni mahali patakatifu pa mfalme”. Utakatifu sasa si haiba ya kimungu bali ni mali ya mwanadamu kwani tunaona wazi jinsi ambavyo mjumbe wa Neno la Mungu, Nabii wa Mungu Amosi ambaye amelibeba Neno lake hapatiwi nafasi. Sehemu hiyo ni mahali patakatifu pa mfalme. Ni mahali pa kuonesha utukufu na madaraka yake ya kifalme na kamwe pasisikike neno la Mungu.

Hili linajidhihirisha katika jamii mambo leo ambayo imegubikwa sana na usekulari ambao unapelekea kukomaa kwa tabia ya ukani Mungu. Tunashuhudia mahali pengi ambapo sauti ya Mungu inapopazwa na watumishi wake kukemea uovu fulani na kutoa wito wa wongofu majibu huwa ni ya upinzani: Mara ngapi tunasikia watumishi wa Mungu wakiambiwa ninyi hubirini dini lakini mambo haya ya kisiasa au ya kuichumi waachie wataalamu wake; au wanaambiwa kwamba mambo haya hayawahusu n.k.

Mwanadamu mwanasiasa au mwanauchumi anajitenga na Mungu na matokeo yake ni kujitafutia utukufu binafsi, kuweka ulinzi wa kutosha kwa ufanisi wa mambo yake bila kujali au kuheshimu maelekezo ya Mungu, Yeye ambaye ameumba yote na kumkabidhi yeye kama wakili wa kuyagawa kwa wanadamu wote.

Katika somo la Injili Kristo anawatuma mitume wake kwenda kueneza habari njema ya wokovu kwa kumrudishia tena mwanadamu hadhi yake iliyoharibiwa na dhambi. Anawatuma kwenda kutoa pepo wachafu, anawatuma kwenda kuwaponya wagonjwa. Wajibu wanaopatiwa hautofautiani na ule wanaopatiwa viongozi wa kidini na wa kisiasa tuliwasikia katika somo la kwanza. Ni wajibu wa kuwafanya wote wauonje upendo wa Mungu kupitia huduma yao. “Akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu”. Maneno haya yanatusisitizia jambo lililo la muhimu sana wakati tunaposimama na kubeba majukumu ya kijamii.

Chakula ni hitaji la muhimu kibinadamu, mkoba wakati wa safari unasaidia kuhifadhi vifaa na mahitaji wakati wa safari, nguo za ziada ni muhimu kwa ajili ya kubadilisha wakati wa shughuli hiyo ya uinjilishaji na fedha zitasaidia kujitafutia mahitaji njiani. Lakini yote haya yanatanabaishwa na Kristo katika somo la Injili ya Dominika ya leo kuwa yanapaswa kuachwa. Nini maana ya katazo hili? Tutatimizaje wajibu huo wa kimisionari bila kujihudumia nasi kimwili ili kupata nguvu zaidi?

Hii ni tahadhari ambayo Kristo anatupatia kuwa makini kuambatana na mahitaji ya kidunia na kuacha kuwapelekea watu habari njema ya wokovu. Kujifikiria nafsi yako zaidi kunaweza kukuingiza katika kiwingu cha kuacha kueneza habari njema na kufikiri namna ya kujishibisha wewe binafsi. Wafalme na watawala wa kidini wanaokemewa katika somo la kwanza walijiweka wao kwanza. Wao walijifikiria wao kwanza na siyo wale waliokuwa wanawaongoza au wale ambao walitegemea kupata huduma yao iwe ya kiroho au ya kijamii.

Mwanadamu anapopatiwa wajibu wa kuihudumia jamii anapaswa katika nafasi ya kwanza kutambua kuwa anatumwa kwenda kuufunua uso wa Mungu, kwenda kuutangaza wema wa Bwana kwa wale anaokabidhiwa. Wajibu huu utatekelezwa vyema pale mmoja anapokuwa tayari kujisadaka, kujiachia na kujitoa kwa ajili ya wengine. Malipo ya huduma yako ni ustawi wa jamii ambayo unaihudumia kwani itakapoonekana kuchanua na kupendeza; pale itakapoonekana kuishi kadiri ya Neno la Mungu ndipo tutakapoambiwa na Bwana Yesu: “Vema mtumishi mwema na mwaminifu, ingia katika furaha yangu”.

Mtume Paulo katika Somo la Pili anatueleza mambo mawili ambayo yanatuangazia kupokea yote kama zawadi kutoka kwa Mungu. Kwanza Mwenyezi Mungu aliye asili ya vyote “atavijumlisha vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani”. Huu ni uthibitisho na ukumbusho kwamba mambo yote katika ulimwengu huu yanapaswa kuendeshwa na kupokelewa huku Kristo akiwa ni kielelezo. Sisi Wakristo tumepewa ufunuo huo. Tunaalikwa kuwa mashuhuda wa maisha na kuwafanya wengine waweze kutambua ukweli huu, kwamba ulimwengu na vyote vilivyomo na uendeshaji wake umejumuishwa katika nafsi ya Kristo.

Huyu ni Mwana wa Mungu aliyekuja duniani katika upendo mkuu kabisa kutuelekeza njia ya kwenda kwa Baba, yaani, kutenda kadiri ya mpango na uradhi wa Mungu. “Naam, katika Yeye huyo; na ndani yake sisi nasi tunafanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake”. Hivyo jambo la pili tunakumbushwa wito huu ambao wakristo wote tunaitwa kuuitikia, yaani, kufanya yote kadiri ya uradhi wa mapenzi ya Kristo ambayo ni mapenzi ya Baba yetu wa mbinguni.

Dominika ya leo tunaalikwa kutafakari huduma zetu za kijamii; tunaalikwa kutafakari juu ya karama mbalimbali tulizokirimiwa na Mungu; tunaalikwa kutafakari juu ya zawadi mbalimbali za kidunia ambazo mwenyezi Mungu ametukirimia. Zawadi hizi zinatuita na kututaka kuzijibu katika upendo.Haya yote; yawe ni madaraka, ziwe ni mali, viwe ni vipaji ni zawadi kutoka kwa Mungu.

Mwenyezi Mungu ananuia kupitia zawadi hizi kumtambua Yeye na pia kuwafanya wengine waonje jinsi Mungu alivyo mtamu. Tujiepushe na ubinafsi, tuepuke kujifikiria sisi wenyewe, tuepuke kujilimbikizia sisi wenyewe. Tulibebe neno la Mungu pekee, tuueneze upendo wa Mungu pekee na kwa kupitia kwetu wote waunganishwa katika Kristo Yesu.

Na Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.