2015-07-10 11:08:00

Kanisa nchini Hispania linawaombea watu wote waliokufa maji baharini!


Kanisa la Kiulimwengu linaadhimisha Jumapili ya Utume wa Bahari, tarehe 12 Julai 2015 na Baraza la Kipapa kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha mshikamano wa dhati na Mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na watu hawa katika ustawi na maendeleo ya binadamu.

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, linaadhimisha Siku ya Utume wa Bahari Kitaifa hapo tarehe 16 Julai 2015 sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, msimamizi wa Mabaharia na wavuvi nchini Hispania. Hii ni siku ya kutafakari kuhusu maisha na utume wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli katika maisha na utume wa Kanisa.

Mwaka huu, Kanisa Katoliki nchini Hispania linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa Mtakatifu Theresa wa Avila, aliyeambata imani na kuimwilisha katika uhalisia wa maisha yake, leo hii ni mfano bora wa kuigwa. Askofu Luis Quinteiro Fiuza wa Jimbo la Tui-Vigo, Hispania, mhamasishaji mkuu wa maadhimisho haya anasema, hii ni fursa makini kwa Kanisa kuungana kwa pamoja kwa ajili ya kuadhimisha Jubilei ya miaka mia tano tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Theresa wa Avila.

Maadhimisho ya mwaka huu yamewekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli na yanaongozwa na kauli mbiu “Nyota angavu; tunakuomba”. Waamini wanamwomba Bikira Maria awasaidie Mabahari na wavuvi waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo kama alivyofanya Mtakatifu Theresa wa Avila hususan wakati wanapokabiliwa na magumu pamoja na changamoto za maisha; watambue kwamba, Mwenyezi Mungu yuko daima pamoja nao na Yeye ndiye kimbilio lao.

Katika maadhimisho haya, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linatolea sala maalum kwa ajili ya watu wote waliokufa maji sehemu mbali mbali za dunia. Waamini wanawakumbuka na kuwaombea mabaharia na wavuvi wanaokabiliwa na magumu pamoja na changamoto mbali mbali wanapokuwa wakitekeleza dhamana na utume wao huko  baharini. Wafanyakazi baharini ni kati ya makundi yanayokabiliwa na hali ngumu zaidi ya maisha, ikilinganishwa na makundi mengine ya wafanyakazi.

Ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, licha ya kukaa muda mwingi pasi na kuonana na familia zao. Hi jukumu la wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuboresha utu, heshima na haki za mabaharia pamoja na wavuvi, ili waweze kuhamasishwa zaidi katika utekelezaji wa dhamana na utume wao kwa ajili ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.