2015-07-10 10:28:00

Aguswa na ushuhuda unaotolewa na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo!


Patriaki Francesco Moraglia, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Venezia, Italia amehitimisha ziara ya kichungaji nchini Kenya ambako ametembelea na kukutana na Familia ya Mungu Parokia ya Mtakatifu Marko, Ol Moran, Jimbo Katoliki la Nyahururu linalongozwa na Askofu Joseph Mbatia. Anasema, huko Kenya amekutana na waamini wanaoishi maisha ya kawaida, lakini wenye furaha na imani thabiti, changamoto kwa waamini wote kuhakikisha kwamba, wanajikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Akiwa Jimboni Nyahururu anasema, ameweza kutembelea na kusali katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Ameshuhudia umaskini wa watu kutokana na hali ngumu ya maisha, lakini ameshangazwa na furaha iliyokuwa inabubujika kutoka katika undani wa maisha yao. Ni watu ambao wanaonesha upendo na mshikamano yanayojikita katika urafiki na mahusiano ya kweli. Ni faraja kuona jinsi ambavyo waamini wanashuhudia imani yao katika maisha ya kawaida pasi na makuu.

Patriaki Francesco Moraglia anasema kwamba, amesali na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, ametoa Sakramenti ya Mpako Mtakatifu kwa wagonjwa na wazee. Amekutana na Halmashauri walei; watu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia, licha ya majukumu yao ya kazi na nyajibu za kifamilia. Amekutana na kundi la Makatekista ambalo liko mstari wa mbele katika kuwafunda waamini tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kiimani.

Patriaki Francesco Moraglia anakaza kusema, changamoto alizokutana nazo wakati wa ziara yake ya kichungaji nchini Kenya ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani unaopaswa kuambata mwaliko unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji Injili ya Furaha, tayari kutoka kimasomaso kuwatangazia watu na kushuhudia Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo, chemchemi ya maisha ya uzima wa milele.

Huko katika Parokia ya Mtakatifu Marko, Ol Morani, ameshuhudia jinsi ambazo Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinavyojibidisha katika kulitafakari Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Ameonja upendo na mshikamano kama ule unaosimuliwa kwenye Kanisa la Mwanzo. Ameona na kushuhudia kazi kubwa la Mapadre wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwatangazia watu upendo na huruma ya Mungu. Hizi ni juhudi ambazo zimetekelezwa kwanza kabisa na Padre Giovanni Volpato na sasa zinaendelezwa na Padre Giacomo Basso, wote kutoka Venezia.

Pariaki Francesco Moraglia anasema, ameguswa kwa kiasi kikubwa na imani inayooneshwa na waamini walei nchini Kenya; imani ambayo inaambata furaha na kumwilishwa katika matendo. Hapa mwamini anashuhudia ari na moyo wa kimissionari kwa kutoka kwenda kuwahubiria maskini Habari Njema ya Wokovu. Huduma hii ya kimissionari inahitaji kwanza kabisa rasilimali watu, fedha na muda, ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha na utume kwa Kanisa mahalia. Licha ya umaskini na hali ngumu ya waamini wa Parokia ya Mtakatifu Marko, Ol Moran, lakini bado wako tayari kukumbatia Injili ya uhai katika furaha na matumaini.

Ni watu wanaoridhika na hata kile kidogo ambacho Mwenyezi Mungu anawakirimia katika maisha yao ya kila siku. Ni waamini wenye imani thabiti wanaoendelea kujenga na kukuza mahusiano yao na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, Bwana na Mwalimu. Hapa kwa kweli inaonekana anasema Patriaki Francesco Moraglia, Mwenyezi Mungu ndiye mchungaji mkuu wa Jumuiya ya waamini wa Parokia ya Mtakatifu Marko, Ol Moran.

Patriaki Francesco Moraglia anasema, kati ya watu aliokutana na kuzungumza nao, hakuona hata mtu mmoja ambaye alionesha nia ya kutaka kuhamia Ulaya. Hawa ni watu wanaofahamu kwamba, kweli Ulaya imesaidia kwa kiasi kikubwa katika maboresho ya maisha yao, lakini pia wanatambua madhara na changamoto ambazo zinaendelea kujitokeza kutokana na utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Barani Ulaya: utu na heshima ya binadamu vinaendelea kutoweka taratibu; watu wamechanganyikiwa kuhusiana na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kisingizio cha uhuru binafsi na haki msingi za binadamu zisizozingatia kanuni maadili na utu wema. Patriaki Francesco Moraglia ameitaka Familia ya Mungu nchini Kenya kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayoambata Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.