2015-07-09 09:57:00

Yaliyojiri wakati wa hija ya kitume ya Papa Francisko nchini Equador!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Julai 2015 amehitimisha hija yake ya kichungaji nchini Equador na kuelekea nchini Bolivia. Wakati wa hija yake nchini Equador amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kujenga na kudumisha Injili ya Familia kama mfano bora wa kuigwa na jamii inayotaka kujenga haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Familia ziwe ni mahali pa kwanza pa malezi na majiundo makini ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili, kijamii na kitamaduni; mambo yanayoshuhudiwa katika maisha na utume wa familia.

Baba Mtakatifu amekazia ari na mwamko wa kimissionari unaojikita katika Uinjilishaji mpya, ili kuponya madonda na makovu ya dhambi yanayojionesha kwa namna ya pekee katika: kinzani, migogoro, vita, ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; mambo ambayo yanaathari kubwa katika utu na heshima ya binadamu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaalika kushuhudia imani katika matendo kwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anakaza kusema, changamoto ya kimissionari na Uinjilishaji mpya vimekaziwa kwa namna ya pekee na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana kwa faragha na Baraza la Maaskofu Katoliki Equador. Amesisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati makini ya shughuli za kichungaji na kwamba, Uinjilishaji kwa sasa upewe msukumo wa pekee nchini Equador, ili kuondokana na ubinafsi, uchoyo, uchu wa mali na madaraka. Uinjilishaji iwe ni fursa ya kujenga na kuimarisha umoja na udugu; upendo na mshikamano wa kitaifa.

Padre Lombardi anakaza kusema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Equador imekazia pia umuhimu wa Kanisa kushiriki kikamilifu katika majiundo ya mtu mzima kiroho na kimwili kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika sekta ya elimu. Baba Mtakatifu analihamasisha Kanisa nchini Equador kujifunga kibwebwe katika sekta ya elimu kwa kuzingatia tunu msingi zinazopaswa kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya, ili kuwajengea kanuni maadili na utu wema, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii na Kanisa katika ujumla wake.

Utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Baba Mtakatifu Francisko anatambua kwamba, Jamii ni jukwaa na nyumba ya wote. Hapa kuna haja ya kukazia umuhimu wa kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali za dunia kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Waraka wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni jambo la kupewa kipaumbele cha pekee na wote. Hapa Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kulinda na kudumisha ekolojia ya binadamu, kwa kuambata Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna mwingiliano mkubwa katika masuala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kitamaduni. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaendelea kukazia umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Huu ni mkazo uliotolewa pia na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume Upendo katika Ukweli, “Caritas in veritate" anabainisha changamoto zinazoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Papa Francisko anaendelea kukazia kuhusu mchango wa Kanisa katika masuala yanayomgusa mtu: kiroho na kimwili. Dini bado ina nafasi ya pekee katika majiundo ya mtu mzima na Kanisa litaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; pamoja na kutambua kwamba, maskini ni amana ya maisha na utume wa Kanisa

Padre Federico Lombardi anasema kwamba, hotuba zote saba zilizotolewa na Baba Mtakatifu Francisko nchini Equador zimejikita katika umuhimu wa kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; upendo na mshikamano wa kidugu; majadiliano na maridhiano kati ya watu; umuhimu wa ujenzi wa jamii inayoheshimu na kuthamini tofauti zake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kila mwananchi wa Equador anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara na kwa njia hii, kweli nchi yao itakuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.