2015-07-09 13:34:00

Watawa shirikianeni na Wakleri katika maisha na utume wa Kanisa


Maisha ya kitawa katika utume wa Kanisa ndiyo kauli mbiu iliyoongoza kongamano la kitaifa la Seminari lililofanyika hivi karibuni mjini Awka, nchini Nigeria. Wajumbe wa kongamano hili pamoja na mambo mengine, wamekazia umuhimu wa watawa kushirikiana na kushikamana pamoja na wakleri, ili kufanikisha utume wa Kanisa ambalo linatumwa Kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mashiko na mvuto.

Kongamano hili ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko anayewaalika watawa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.Mwaka wa Watawa Duniani ni sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ambamo Waraka wa Mapendo kamili ulichapishwa, ili kupyaisha maisha na utume wa watawa ndani ya Kanisa, tayari kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya Furaha kwa Watu wa Mataifa.

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, yatafikia kilele chake hapo tarehe 2 Februari 2016, katika Maadhimisho ya Sherehe ya kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani, iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Siku hii kutafanyika Kongamano la kitaifa, linalotarajiwa kuwashirikisha wajumbe kutoka katika Majimbo mbali mbali nchini Nigeria.

Watawa nchini Nigeria wanaendelea kukazia umuhimu wa Kanisa kujikita katika mchakato wa majiundo ya awali na endelevu, ili kuwajengea watawa uwezo wa kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, tayari kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu pamoja na kuwahudumia Watu wa Mungu kwa upendo na majitoleo makuu.

Askofu Michael Apoch, Mwenyekiti wa Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwa ajili ya Seminari anasema kwamba, majiundo makini ni changamoto endelevu na kwamba, watawa wanapaswa kubadilishana uzoefu na mang’amuzi katika hija ya maisha na utume wao wa kitawa na kimissionari. Kuna haja ya kuwa na ushirikiano kati ya watawa na wakleri katika ngazi mbali mbali ili kuwa na matumizi bora zaidi ya rasilimali watu na vitu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia.

Wajumbe wanasema kwamba, maisha ya kitawa na kazi za kitume ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Watawa watumie fursa mbali mbali katika tafakari na maboresho ya maisha yao, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na utume wao kwa Kanisa mahalia. Huu ni mchakato wa shughuli za kichungaji unaojikita katika ushirikiano, changamoto kubwa na endelevu, ili kuondokana na ubinafsi unaoweza kuwafanya watawa kujisikia kutengwa na kutothaminiwa na Makanisa mahalia. Jambo la msingi ni watawa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili katika maisha na huduma yao kwa Watu wa Mungu. Lakini, hii pia ni changamoto kwa waamini wote bila ubaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.