2015-07-09 11:15:00

Taizè inaendesha mkutano wa kimataifa kuhusu wito na maisha ya kitawa!


Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 12 Julai 2015 inafanya tafakari ya kina kuhusiana na wito na maisha ya kitawa. Huu ni mkutano wa kimataifa unaowashirikisha watawa ambao bado hawajatimiza umri wa miaka 40 na wanaishi katika Jumuiya za kitawa pamoja na Monasteri. Wanashiriki pia vijana ambao wako katika safari ya majiundo ya kitawa na wale ambao wamebobea kwa sasa na wako tayari wanajiandaa kwa ajili ya kutoa maamuzi ya wito na maisha yao.

Taizè alipenda kusema Fra Roger, muasisi wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè inayowakusanya vijana kutoka katika madhehebu mbali mbali ya Kikristo kwamba, hii ni jumuiya inayojikita katika maisha ya kitawa na kimonaki. Wawakilishi wa mti huu mkubwa ni watawa, wakuu wa mashirika na vijana ambao wanataka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na jirani zao kwa njia ya maisha ya kitawa na kazi za kitume au kwa njia ya huduma makini kama ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya waamini.

Hawa ni watu kutoka katika Makanisa na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, wanaotaka kuendeleza wito na maisha ya kitawa sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuguswa na ushuhuda wa maisha, wito na utume unaotolewa na Mashirika ya kitawa pamoja na kazi za kitume. Ushuhuda unaotolewa na wahamasishaji katika mkutano huu wa kimataifa unafuatiwa na majadiliano ya kina yanayowahusisha wote wanaohudhuria mkutano huu, ili kuweza kujichotea utajiri wa maisha ya kitawa kwa namna ya pekee, Kanisa linapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani.

Baadhi wakuu wa Mashirika ya Kitawa wamechangia mada katika mkutano huu. Hawa ni wakuu wa Shirika la Wayesuit, Wadominican, Wamissionari wa Afrika pamoja na wawakilishi wa Jumuiya za Makanisa ya Kiprotestanti na Kiorthodox kutoka Barani Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.