2015-07-09 14:48:00

Papa Francisko amefunika: Mambo makuu: Sadaka, Mshikamano na Kanuni


Rais Rafael Correa wa Equador anasema wananchi wengi wa Equador hawataweza kusahau hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao, kwani wamemwonjesha upendo na ukarimu na kwamba amewagusa watu wengi kwa uwepo na ujumbe wake. Rais Correa anasema, binafsi ameguswa sana na hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa tarehe 7 Julai 2015 kwa viongozi wa serikali na jamii katika ujumla wake. RaisCorrea ameyasema haya wakati wa mahojiano maalum na Olivier Bonnel wa Radio Vatican ambaye yuko kwenye msafara wa Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kusini. 

Katika hotuba hii, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee mambo makuu matatu: sadaka, mshikamano na kanuni ya auni, ili kujenga na kudumisha jamii inayoshikamana na kuhudumiana, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Baba Mtakatifu amewakumbusha viongozi wa kisiasa kwamba, wamepewa bure na wanapaswa pia kutoa bure kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu katika hotuba hii amezungumzi juu ya umaskini na maskini pamoja na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi nzima unapaswa kusaidia mchakato wa maendeleo kwa wengi pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanashirikishwa katika kuamua, kupanga na kutekeleza mikakati na sera zinazohusu maendeleo yao: kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi anasema Rais Rafael Correa wa Equador katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu kwa kina na mapana amezungumzia kuhusu ekolojia na umuhimu wa kulinda na kudumisha ekolojia ya binadamu, changamoto na mwaliko kwa wananchi wa Equador kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira ambayo kimsingi ni nyumba ya wote, kwa ajili ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Kwa namna ya pekee, Serikali ya Equador inapenda kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuchapisha Waraka wake wa kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Katiba ya Equador inabainisha kwamba kila mtu ana haki ya kufaidi rasilimali za nchi na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira anakaza kusema, maji ni haki msingi ya binadamu kwani ina uhusiano mkubwa na maisha ya binadamu. Haya ni mambo ambayo yanabainishwa pia na Katiba ya Equador, dhamana ambayo inaendelezwa kwa ari na moyo mkuu na Serikali ya Bwana Rafael Correa.

Ni matumaini yake kwamba, Waraka huu utakuwa ni msaada mkubwa wakati wa maadhimisho ya Mkutano wa kimataifa juu ya mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika mjini Paris, Desemba, 2015. Kuna uhusiano mkubwa kati ya mazingira na maisha ya kiroho na kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa ili kutumia kwa ajili yake na kwa ajili ya vizazi vijavyo. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko unaweza kukubaliwa na kuwafikia watu wengi zaidi kwani ni ujumbe unaojikita katika wajibu na dhamana ya kimaadili, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Ujumbe huu unaweza pia kukabiliana na upinzani na changamoto kubwa kwani unagusa na kutikisa masuala ya kisiasa na kiuchumi; changamoto kubwa katika Jumuiya ya Kimataifa. Hii inatokana na ukweli kwamba, wachafuzi wakubwa wa mazingira ni Nchi tajiri zenye viwanda vingi, lakini wanaoathirika zaidi ni maskini. Nchi changa zaidi duniani zinakabiliwa na deni kubwa la nje, kiasi hata zinachechemea kulipa deni hili.

Kumbe, Nchi tajiri duniani zinawajibu wa kimaadili kuhakikisha kwamba, zinachangia katika mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, Nchi changa nazo zitapaswa kutekeleza dhamana yake kwa kutafuta teknolojia rafiki kwa ajili ya kukoleza maendeleo yake. Hapa kuna haja ya kubadili tabia ya uzalishaji, ugawaji na ulaji, ili kuendeleza na kutunza mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.