2015-07-09 09:58:00

Papa apokewa kwa shangwe Bolivia


(Vatican Redio) Jumatano alasiri, Baba Mtakatifu Francisko,  alikamilisha ziara yake ya siku nne nchini Ecuador na kuelekea katika mji wa La Paz Bolivia, ikiwa ni hatua ya pili katika ziara yake ya kitume , kutembelea mataifa matatu ya Amerika ya Kusini, Ecuador, Bolivia na Paraguay.

 Safari hii ya kutoka  Quito Ecuador hadi La Paz/El Alto  ilichukua muda wa saa tatu na dakika kumi na tano, na hivyo aliwasili majira ya saa kumi na dakika kumi na tano katika Uwanja wa Kimataifa wa El Alto, ambako kulifanyika hafla fupi ya mapokezi  ya viongozi wa Kanisa na Kiserikali , ikipambwa na nyimbo za Kitaifa na gwaride la kijeshi kwa heshima yake .

Baada ya hotuba ya makaribisho kutoka kwa Rais wa Bolivia Mheshimiwa Juan Evo Morales Ayma,  Papa pia alitoa hotuba yake mbele ya wenyeji wake akishukuru kwa mapokezi mazuri, na kuwa katika taifa hili  pendwa la Bolivia lenye kuwa na utajiri mwingi asilia ,mabonde, misitu ya Amazon , jangwa na maziwa. 

Papa alisema yuko katika taifa hilo, kama  mgeni na Mhujaji , aliyekwenda   kuthibitisha imani kwa wale wanaoamini katika Kristo Mfufuka, ili kwamba , wakati wa hija yao ya maisha hapa duniani , kama waamini waweze kuwa mashahidi wa upendo wake Kristo na kuwa  chachu na mwanga  kwa ajili ya ulimwengu ulio bora zaidi kupitia ushiriki wao katika   ujenzi wa udugu katika jamii.

Papa alileleza na kuisifu Bolivia kwamba inapiga hatua muhimu katika kuboresha sekta za kijamii katika maisha ya Raia wake kiuchumi , kijamii na kisiasa. Na pia amefurahi kwamba  Katiba ya nchi hiyo ,  inatambua haki za watu binafsi, makundi madogomadogo na mazingira ya asili, kwa uwepo wa taasisi ya kuwatetea. Kupata mafanikio katika malengo haya ni katika  raia kuwa na  roho ya ushirikiano na majadiliano,  ikiwa ni pamoja na ushiriki wa watu binafsi na makundi ya kijamii katika mambo yanayogusa maslahi ya kila mmoja.

  Na kwamba maendeleo katika mwingiliano wa kitaifa unadai   kila mtu binafsi kuthamini  daima  maadili na  kukua kwa  umoja na mshikamano katika kazi za kutetea  manufaa ya wote, bila ya mtu kubaguliwa au kutengwa au kupuuzwa katika utendaji  wote. Papa ameeleza na kuonya kwamba ukuaji wa maendeleo yanayolenga katika  vitu tu,  daima huongoza katika hatari ya kujenga mgawanyiko mpya, kati ya matajiri na maskini.  Pamoja na hilo pia kunahitajika  taasisi kutenda kwa uwazi na umoja wa kijamii, katika kukuza elimu kwa wananchi wote.

Baba Mtakatifu Francisco aliendelea  kuzitazama siku za usoni kwa taifa hilo na kuhimiza wito kwa wafuasi wa Kristo, washiriki  katika kutangaza furaha ya Injili na kuwa chumvi ya dunia na mwanga wa ulimwengu. Na kwamba, sauti ya maaskofu, inapaswa kusikilizwa kama  Kanisa  na Mama  Bikira Maria kama sauti ya kinabii kwa  jamii, katika upendeleo wa  kiinjili wa kuhudumia hasa  kwa ajili ya maskini.  Huduma na upendo wa kidugu , wenye kuonyesha ushuhuda hai kwa amri mpya ya Yesu, inaoonekana katika mipango, kazi na taasisi zinazofanya kazi kwa ajili ya  maendeleo muhimu ya mtu, ikiwa  pamoja na kwa ajili ya huduma na utetezi wa makundi yaliyo katika hatari zaidi za kunyanyaswa au kudhulumiwa . Papa ameasa , haiwezekani kumwamini Mungu kama Baba, bila kumwona mtu mwingine mke au mme anayepungukiwa na mahitaji muhimu. Na haiwezekani kuwa mfuasi wa Yesu bila ya kuyatoa maisha yetu kwa ajili Wale ambao Kristo aliwafia msalabani.

Hotuba ya Papa iliendelea kusema, katika nyakati hizi ambako maadili msingi  mara nyingi yanapuuzwa au potoshwa, tahadhari katika kuilinda familia inakuwa ni wajibu muhimu kwa wale wote wanaohusika na utendaji kwa ajili ya mazuri ya wote., kwa kuwa familia ni kiini msingi cha jamii.  Katika  familia mna mwendelezo wa  vifungo imara vya umoja ambamo uwepo wa binadamu umefumbatwa kama msingi na   uzazi na elimu ya watoto, huhakikisha mwendelezo mpya wa  jamii.

Papa alieleza na kugeukia hisia za Kanisa, kwa ajili ya vijana, ambao hutetea  imani na maadili, kwamba wanakuwa ni tegemeo katiha ahadi za siku zijazo,kama watetezi katika kutangaza mwanga wa alfajiri na machipukizi mapya katika  Injili, kama alivyoeleza Mtakatifu Yohane Paulo II, katika ujumbe wake kwa ajili ya  Siku ya Vijana Duniani ya 18.

Papa alikamilisha hotuba yake kwa kurudia kutoa shukurani kwa uwepo wa Mheshimiwa Rais Juan katika hafla hii akisema kwamba, imemtia moyo kw na matumaini na matazamio mazuri kwa kipindi hiki cha kukutana, kuzungumza na maadhimisho ya Ibada . Na kwamba anajisikia nyumbani kuwa katika taifa hili ambalo limepiga hatua katika utamaduni wa amani na haki kwa amani.

Papa aliiweka ziara yake katika taifa hili la Bolivia chini ya Ulinzi wa Bikira Maria wa Copacabana, Malkia wa Bolivia, akimwomba pia awe msimamizi wa   raia wote wa Bolivia.  Bwana akubariki! Jallalla Bolivia. 








All the contents on this site are copyrighted ©.