2015-07-09 11:50:00

Miaka 4 ya Uhuru wa Sudan ya Kusini: Majanga na maafa tupu!


Ilikuwa ni tarehe 9 Julai 2011 Sudan ya Kusini ilipojipatia uhuru wake na kuanza kujiamria mambo yake yenyewe baada ya wananchi kupigana vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi. Huu ukawa ni mwanzo wa ndoto ya matumaini ya maisha bora, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Lakini kwa bahati mbaya, ndoto hii ikageuka kuwa cheche za machungu, kinzani, vita na maafa makubwa yanayoendelea kujitokeza nchini Sudan ya Kusini. Miaka minne ya uhuru, imepotea bure na watu wanaendelea kuteseka kama ilivyokuwa kabla ya kujipatia uhuru kunako mwaka 2011.

Machafuko ya kisiasa yaliyojitokeza kunako mwaka 2013 yamesababisha wananchi millioni 2 kuyakimbia makazi yao, ili kutafuta usalama wa maisha na mali zao. Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna wakimbizi 850, 000 kutoka Sudan wanaohifadhiwa nchini Ethiopia, Uganda, Sudan Kongwe na Kenya. Kuna watu zaidi ya millioni moja ambao hawana makazi nchini Sudan ya Kusini. Haya yamo kwenye taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Kipapa kwa ajili ya msaada kwa Makanisa hitaji; ACS.

Usalama wa wanawake hata katika kambi za wakimbizi uko mashakani kutokana na vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia unaofanywa na baadhi ya wakimbizi na wahamiaji wanaohifadhiwa kwenye kambi hizi. Wakati mwingine, kumekuwepo hata kinzani za kikabila kati ya wakimbizi hali ambayo inagumisha utoaji wa huduma, amani na utulivu miongoni mwa wakimbizi. Sudan Kongwe haiwatambui wakimbizi kutoka Sudan ya Kusini kadiri ya protokali ya Umoja wa Mataifa, bali inawaona kuwa ni wananchi wa Sudan wanaorejea nyumbani kwao, kwani Sudan Kongwe, hakifurahia sana na uamuzi wa Sudan ya Kusini kujitenga na kuwa huru.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.