2015-07-09 08:36:00

Jumapili ya utume wa bahari: Lengo ni kuwaenzi mabaharia na wavuvi!


Mama Kanisa tarehe 12 Julai 2015 anaadhimisha Siku ya Utume wa Bahari, fursa kwa Familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kumshukuru Mungu kwa huduma na mchango mkubwa unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini sadaka ya watu hawa ambao wakati mwingine utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii.

Maadhimisho ya Utume wa Bahari, yalianzishwa kunako mwaka 1975, ili kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea mabaharia na wavuvi pamoja na familia zao. Hii ni siku maalum ambayo Kanisa linatambua mchango mkubwa unaotolewa na Mabaharia katika ustawi na maendeleo ya binadamu katika nyanja mbali mbali za maisha. Maadhimisho haya pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani yanawashirikisha Wakristo kutoka katika Makanisa na madhehebu mbali mbali, ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na mabaharia pamoja na wavuvi.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum katika ujumbe kwa maadhimisho ya Siku ya Utume wa Bahari linakaza kusema, kuna mabaharia zaidi ya millioni 1. 2 wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika mazingira magumu na hatarishi. Ni wafanyakazi ambao mara nyingi hawaonekani, lakini wanatoa huduma muhimu sana kwa ustawi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kwa bahati mbaya ni watu wanaokumbukwa pale tu panapotokea ajali au majanga, lakini sadaka wanayoitekeleza kila siku ya maisha, mara nyingi inasahaulika kama ndoto ya mchana.

Licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya usafiri wa bahari, lakini mabaharia bado wanalazimika kutumia muda mrefu zaidi wakiwa nje ya familia zao; wanakabiliwa na sheria kali na wakati mwingine maisha yao yako hatarini kutokana na vitendo vya maharamia ambao wamekuwa wakiwateka nyara. Ni matumaini ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi kwamba nchi mbali mbali zitaendelea kuridhia mkataba wa kazi za mabaharia uliotiwa sahihi kunako mwaka 2006, ili kuboresha hali ya maisha na maeneo ya kazi.

Kinzani, vita na migogoro ya kisiasa na kijamii imepelekea Mabaharia hususan wanaotekeleza dhamana yao Bahari ya Mediterrania kujikita zaidi katika kazi ya kuokoa wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na ubora wa maisha Barani Ulaya. Mabaharia wanaendelea kutekeleza kazi yao kikamilifu ili kuwapatia msaada wale wanaoteseka kutokana na shida mbali mbali.

Wakati mwingine, mabaharia hawa wanahatarisha usalama wa maisha yao kutokana na ukweli kwamba, wanabeba wakati mwingine mizigo ya hatari na mazingira yao ni kwa ajili ya wafanyakazi wachache, kumbe hawawezi kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi wengi wanaohitaji msaada wao. Mabaharia ni watu waliofundwa kitaaluma kutoa huduma ya dharura wakati wowote, lakini wimbi kubwa na wahamiaji na wakimbizi linalojionesha kwa wakati huu, hakuna shule wala taasisi ambayo imewapatia ujuzi na maarifa ya kuwasaidia watu hawa. Lakini pamoja na changamoto zote hizi wanapaswa kutoa huduma hata katika mazingira magumu na hatarishi. Ni watu wanaohitaji pia msaada wa kisaikolojia, kiroho na kiutu.

Mama Kanisa anapoadhimisha Jumapili ya utume wa bahari, anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa mabaharia na wavuvi kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu, licha ya changamoto, kinzani na matatizo wanayokabiliana nayo. Kanisa linawashukuru kwa huduma makini hata wakati mwingine kwa kuhatarisha usalama wa maisha yao, ili kuwaokoa wahamiaji na wakimbizi wanaoteseka baharini.

Kanisa linapenda kutambua mchango wa wahudumu wa maisha ya kiroho pamoja na watu wa kujitolea wanaotoa huduma kwa mabaharia pamoja na wavuvi. Uwepo wao kwenye bandari ni kielelezo cha Kanisa linalopenda kuwaonjesha upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo. Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi linahitisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Jumapili ya utume wa bahari kwa kuialika Jumuiya ya Kimataifa na Mashirika mbali mbali ya kitaifa na kimataifa kutafuta suluhu ya kudumu itakayosaidia kudumisha misingi ya amani, utulivu na maridhiano kati ya watu.

Jumuiya ya Kimataifa itenge rasilimali ya kutosha si tu kwa ajili ya kufanya tafiti na utoaji wa msaada, bali pia kujikita katika mchakato wa kudhibiti na hatimaye, kukomesha biashara haramu ya binadamu inayofanywa dhidi ya wahamiaji na wakimbizi wanaotoka kwenye maeneo ya vita na umaskini. Ujumbe huu umetiwa sahihi na Kardinali Antonio Maria VegliĆ², Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na Askofu mkuu Joseph Kalathiparambili, Katibu mkuu wa Baraza.

Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.