2015-07-09 15:17:00

Hotuba ya Papa kwa viongozi wa mamlaka ya kiraia Bolivia


Vatican Radio)Baba Mtaktaifu Francisco , Jumatano baada ya hafla ya mapokezi katika Uwanja wa Kimataifa la La Paz na kukutana na Rais katika Ikulu ya Bolivia ambako alipata muda wa kuwa na mazungumzo ya faragha na Rais Evo Morales Ayma,  alielekea  katika Kanisa Kuu la mjini La Paz, ambako alikuwa na ratiba ya kukutana na viongozi katika Mamlaka za kiraia na Wawakilishi wa tamaduni na vyama vya kiraia  Bolivia.

Katika hotuba yake iliyokuwa imeandikwa tayari, Papa Francisko , kwa mara nyingine arudia kuzungumzia haja  ya sera, mipango na kazi za serikali na taasisi mbalimbali kulenga kufanyika kwa  manufaa ya wote na katika kukabiliana na changamoto zinazokabili jamii, hasa migogoro ndani ya familia, uhamiaji, na maendeleo endelevu kwa binadamu, na changamoto katika uwakilishi  na viumbe.

Papa aliionyesha furaha yake ya kukutana na viongozi hao, kama nafasi makini ya kushirikisha uzoefu wa utendaji kwa manufaa ya wote. Na pia kwa namna yakipekee alimshukuru Askofu Mkuu Edmundo Abastoflor  wa Jimbo Kuu la  La Paz  kwa makaribisho yake mazuri,  na wao kumpa ruhusa kutoa maoni yake kwa kifupi,kuwatia moyo  na  kuunga mkono kazi zao. 

Hotuba ya Papa ilianza na wito kwamba, kila mmoja wao mahali hapo ameitwa kufanya kazi kwa ajili ya mazuri ya wote. Na alikumbusha kwamba Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican uliochapishwa miaka hamsini iliyopita unatoa ufafanuzi bayana juu ya  kufanya kazi kwa manufaa ya wote, kama sharti msingi katika maisha ya kijamii ikiruhusu vikundi vya kijamii na wanachama wake binafsi,katika   uhakika na utayari wa kufanikisha malengo yao wenyewe. Papa alieleza na kushukuru  kazi na malengo yao, yanayowezesha  watu binafsi na jamii  kwa ujumla , kuendeleza na kutimiza yanayotakiwa.

Na akaonyesha imani yake kwamba, wataendelea kwa uhakika, kupania ufanikishaji wa  mazuri kwa manufaa ya wote, kupitia huduma ya kazi zao. Na aliombea juhudi hizo  ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuheshimu utu wa mtu , uliofumbatwa katika misingi inayohamasishwa na utendaji wa haki katika maendeleo endelevu, na umuhimu wake,  katika ujenzi wa  amani katika kijamii yenye utulivu na usalama kama inavyotakiwa na sheria za nchi , ambazo haziwezi kufanikishwa bila kujali kwa namna ya kipekee uwepo wa haki kwa watu wote.

Hotuba ya Papa iliendelea kutazama kwa makini umuhimu wa kujali utetezi na utunzaji wa mazingira kama hoja msingi pia  katika maendeleo endelevu ya jamii  hasa katika mtazamo wa mahusiano yake ya karibu katika miundo  ya mazingira ya asilia  na mazingira ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Papa amelitaja hilo kuwa  jambo la dharura kwa kila mmoja wao, kutoa kipaumbele katika  misingi ya kudumisha  viumbe na mazingira katika asili zake, kama moja kipimo katika uwezo binadamu kuheshimu mazingira katika utatuzi wa masuala  na changamoto za kijamii na mazingira katika nyakati zetu.  Vinginevyo, Papa ameasa, matabaka ya barafu milimani yataendelea  kupungua siku hadi siku.  Papa ameeleza na kutoa shukurani kwa wale wote wanaofanya kazi  ya kutetea  wajibu kwa  kuzingatia karama hizi, kama hatua ya kuhakikisha dunia inabaki katika mazingira yake asilia hata kwa vizazi vijavyo.

Papa ameeleza na kukumbusha kwamba kila jambo hutegemea jambo jingine na tunahitajiana mmoja kwa mwingine. Na akaonya dhidi ya sera za kisiasa kuongozwa na kigezo cha upatikanaji wa faida za kifedha , au uchumi kutawaliwa na mfumo wa ubingwa au kutafuta faida kwa kuongeza uzalishaji wa kiwango cha juu, bila kujali athari zingine kwa dunia na ubinadamu. Papa anasema , mazingira asilia yana uhusiano wa karibu na maisha ya jamii, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi pia. 

Kwa maelezo hayo  aliwageukia Wakristo akisema wao kama wafuasi wa Injili, waenezaji wa Habari Njema na kama wajumbe wa wokovu wa binadamu , kwa namna ya kipekee wanatakiwa kuvuvia na  kuhamasisha  uadilifu  katika hayo. Na hivyo wanapaswa kushiriki katika uongozi wenye njia za utendaji zenye kujali yote,  maslahi ya mtu binafsi, na pia kwa ajili ya manufaa ya wengine, kuwa na  moyo wa kiasi, fadhila na wema kwa wengine, katika mfumo wa kuishi kwa ushirikiano kama inavyosema Injili .

Hotuba ya Papa iliendelea kutazamisha katika hali za kileo ambamo watu wengi wamemezwa na mazingira ya ukosefu wa usawa  na moyo wa kutojali wengine. Uwepo wa mafanikio yanayoelekezwa tu katika utajiri wa mtu mmoja kulimbikiza mali binafsi na tabia zauchoyo na umimi, sera za kulinda maslahi binafsi kwa migongo ya wengine, badala ya kuwa na njia za kueleweka katika  mafanikio. Papa ametaja tabia ya ubinafsi, hufungua njia ya mianya ya migogoro na migawanyiko ya kijamii;na hasa milango  ubaya wote wa rushwa, ambayo huvunjika moyo wanyonge na kuleta  uharibifu kwa wengine . Utendaji unaomhamisha mtu kujiweka mbali na utumishi kwa manufaa ya wote na kujikita katika ubinafsi na umimi.  

Pia Papa amezungumzia  makundi mbalimbali ya kijamii yanavyokuwa na wajibu wa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano katika maendeleo ya jamii, akihimiza uzingatia wa uhuru wa maoni kwa  wasomi, vyama vya kiraia na vyombo vya mawasiliano kwa ajili ya ufanikishaji wa sera na utendaji wa  shughuli za wote kwa  uwazi , upendo na ubunifu katika huduma kwa manufaa ya wote.

Katika hilo, Papa amewaasa  Wakristo kwamba wameitwa kuwa chachu katika  jamii, kupeleka  Injili ya upendo na mshikamano kwa manufaa ya wote.Amesema , Mwanga wa Injili ya Kristo si mali ya kanisa; lakini ni Kanisa katika huduma ya Injili, inayoweza  kufikishwa katika miisho yote ya dunia. Imani ni mwanga wenye kuwamulikia wote hata  viongozi kuheshimu  dhamiri na historia ya kila mtu na jamii. Ukristo una jukumu muhimu katika kuchagiza utambulisho wa watu Bolivia. Ni changamoto inayolenga  katika kusaidia kukuza ukuaji wa kiroho na dhamira ya Kikristo katika miradi ya kijamii.

Papa alieleza na kutaja makundi mbalimbali ya kijamii, na hasa  familia, ambayo ni kila mahali  hukutana na kitisho na unyanyasaji wa majumbani kutokana na , ulevi, ngono, madawa ya kulevya, ukosefu wa ajira, kukosekana kwa utulivu wa mijini, kutelekezwa ya wazee, na watoto mitaani. Matatizo haya mara nyingi, anasema Papa  yameonekana kuwa matokeo ya mifumo ya itikadi za ukoloni ..  Hivyo matatizo mengi ya kijamii  yanabaki kutatuliwa kimya kimya ndani ya familia;  na familia zikishindwa kuingilia kati familia zingine, na hasa wale  ambao wako hatarini zaidi na wasiokuwa na utetezi.

Papa ameitaja Bolivia kuwa iko katika  njia panda ya kihistoria:  kisiasa na kitamaduni , na kidini, kama sehemu ya changamoto kwenye kukuza umoja na mshikamano , kwa taifa hili ambalo historia yake ya nyuma iligubikwa na unyonyaji,choyo na aina zingine za ubinafsi na utengano. Na kwa sasa unakuwa ni  wakati kwa ajili ya kujenga upya  umoja na mshikamano. Papa ameonyesha imani yake kwamba, leo hii Bolivia inaweza "kujenga aina mpya ya utamaduni wake wa awali.  Kukishinda kigugumiza  cha kutoaminiana, na kuishi sera  za  ushirikiano na umoja hata na wale wanaoonekana kuwa tofauti,   kwa sababu mpya za maendeleo(Taz Evangelii Gaudium, 210).

Papa alihitimisha, kwa kumwomba Bwana ili taifa la Bolivia, liweze kupiga hatua kubwa za maendeleo endelevu yenye kuleta furaha kamili na baraka na amani kwa  watu wake wote wa Bolivia . Na ameliweka taifa lote la  Bolivia chini ya usimamizi na msaada wa Mama  Bikira Maria. Na kuwasihi pia wamkumbuke katika sala zao.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.