2015-07-08 14:07:00

Watawa kuweni macho na mitandao ya kijamii! Huko kuna waka moto!


Askofu Joseph Obanyi Sagwe wa Jimbo Katoliki Kakamega, Kenya, amewataka watawa kuwa macho na makini kutokana na changamoto mbali mbali zinazosababishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari kwa ajili ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa. Askofu Sagwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano ya Jamii, Baraza la maaskofu Katoliki Kenya ameyasema hayo hivi karibuni wakati akitoa hotuba kwenye semina iliyokuwa inafanyika kwenye nyumba Mama ya Masista wa Bikira Maria, Jimbo Katoliki la Kakamega.

Amewataka watawa kupyaisha: Imani, Karama na Maisha yao ya kitawa, tayari kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili kumshuhudia Kristo aliye njia, ukweli na uzima. Semina hii ya siku mbili imehudhuriwa na watawa zaidi ya 150 kutoka: Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan ya Kusini na Marekani.

Askofu Joseph Obanyi Sagwe amewakumbusha watawa kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, ili fursa ya kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini, changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa watawa.

Watawa wanaendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na katika jamii kwa ujumla. Watawa wasipojifunga kibwebwe wanaweza kujikuta wakimezwa na malimwengu. Watawa wa Bikira Maria, Jimbo Katoliki la Kakamega wanaadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu lilipoanzishwa. Watawa wanahamasishwa kujikita katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa kama chemchemi inayowapatia nguvu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini katika huduma makini katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii.

Askofu Joseph Obanyi Sagwe anakaza kusema, maisha ya ndoa na familia pia yanakabiliwa na changamoto ambazo zinahatarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, changamoto kwa Kanisa na wanandoa wenyewe kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Familia, dhidi ya utamaduni wa kifo na mmong’onyoko wa maadili na utu wema.

Njia makini ya uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Watawa waendelee kujibidisha katika utume kwa familia na vijana, ili kuwajengea watu misingi bora ya maisha ya Kikristo, kiutu na kitamaduni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CISA.








All the contents on this site are copyrighted ©.