2015-07-08 14:29:00

Mchakato wa majadiliano waanzishwa ili kunusuru jahazi Burundi!


Mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, katika kikao chake kilichohitimishwa hivi karibuni, wameiomba Serikali ya Burundi kuahilisha uchaguzi mkuu wa Rais hadi mwishoni mwa mwezi Julai na kwamba, Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ameteuliwa kuwa mpatanishi wa mgogoro huo wa kisiasa ambao unatishia kugeuka kuwa ni vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Kuahilishwa kwa uchaguzi mkuu nchini Burundi kunalenga kutoa nafasi kwa Rais Museven kuanzisha mchakato wa majadiliano, ili kuweza kufikia suluhu ya amani nchini Burundi, kwani kwa sasa hakuna uhakika wa uwepo wa mazingira ya uchaguzi huru na wa haki. Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wao uliokuwa unafanyika Jijini Dar es Salaam wanataka vyama vya upinzani na chama tawala kujadiliana ili kupata muafaka. Hadi sasa ratiba inaonesha kwamba, uchaguzi mkuu nchini Burundi unatarajiwa kufanyika hapo tarehe 15 Julai 2015.

Wachunguzi wa mambo wanasema, viongozi kama Paul Kagame wa Rwanda, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi hawakuhudhuria. Viongozi wa upinzani wanataka Rais Pierre Nkurunziza kujitoa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais kwani uwepo wake ni kuvunja kwa Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.