2015-07-08 15:06:00

Leo ni zamu ya kifimbo cheza! Mkong’oto wa kichungaji!


Toka enzi za Warumi Kamanda wa Polisi alikuwa anabeba fimbo ndogo mkononi kuonesha nguvu na mamlaka ya cheo chake. Fimbo hiyo aliitumika kufanyisha mazoezi ya kipolisi na kuadhibu. Hadi leo polisi wa cheo fulani hubeba fimbo. Kutokana na kuitumia kuadhibu waswahili wanaiita mkong’oto. Fimbo inashikwa pia na mwongoza bendi wakati wa maandamano au na anayepimisha (kondakta) “Orchestra” au kwaya. Wahasisi wengi wa mataifa ya kiafrika walikuwa na kawaida ya kubeba fimbo kokote waendako. Fimbo ya kiongozi ilikuwa ni alama ya nguvu, mamlaka na uongozi.

Katika Biblia Takatifu fimbo inamaanisha nguvu au mamlaka ya mpigania uhuru wa raia dhidi ya wakandamizaji. Kwa mfano, Musa alibeba fimbo iliyotenda maajabu aliyoagizwa na Mungu katika kuwakomboa Waisraeli. Mbele ya Farao fimbo ya Musa iligeuka kuwa nyoka na kuwameza nyoka feki wa waganga wake. Katika Bahari ya Sham Musa aliitumia fimbo kupiga maji na kuyagawa ili waisraeli waweze kupita pahala pakavu. Fimbo hiyohiyo ikayarudisha maji na kuzamisha majeshi ya Farao. Fimbo hiyo tena iligonga mwamba huko Meriba na kububujisha maji waliyokunywa Waisraeli.

Muasisi wa Taifa la Tanzania aliitwa Musa kwa hoja kwamba alipigania uhuru dhidi ya wakoloni na kulipatia dira ya maisha kwa falsafa ya kiafrika ya Ujamaa na Kujitegemea. Aidha, alikuwa daima anabeba fimbo hadi akaitwa “Mzee Kifimbo”. Katika Kanisa, Maaskofu na Maabate wanabeba fimbo (bakora) wakati wa kuendesha ibada kuonesha nguvu waliyopewa na Kristo ya kuwa wachungaji katika Kanisa, yaani kuongoza waamini kama Mchungaji wa kondoo, huku wakijitahidi kumuiga Yesu kristo mchungaji mkuu.

Katika fasuli ya leo tutashuhudia Yesu anawatuma wafuasi thenashara kwenda safari na anawaagiza wasichukue chochote isipokuwa fimbo, halafu wawe wawili wawili na wasivae kanzu mbili.  Kabla ya kuona maana ya maagizo hayo hasa hilo la kubeba fimbo, tuone kwanza mazingira yalivyokuwa:“Yesu akawaita kwake,” maana yake anakuita hata wewe kuwa mwandani wake. Kisha “akawatuma wawili wawili.” Ni utamaduni wa kiyahudi kuwa wawili wawili. Faida yake ni katika kusaidiana na katika kutoa ushahidi wa kuaminika: “Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja, maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake. Hata ikiwa mtu aweza kumshinda yule aliye peke yake, wawili watampinga….” (Mhub. 4:9-12).

Katika kanisa la awali mitume waliendeleza utamaduni wa Agano la Kale wakaenda kuhubiri wawili wawili. Mathalani, Petro na Yohane wanaenda wawili hekaluni kusali; Paulo na Barnabas walipelekwa Siria. Hali ya wawili wawili inawakilisha maisha ya kanisa. Wakristo tumeitwa kuishi imani yetu katika Jumuia ya kindugu, na kupendana katika Kanisa. Katika kipengee hiki tunatofautiana na imani nyingine zinazotilia mkazo utakatifu wa mtu binafsi na wa mahusiano ya binafsi na Mungu.

Kabla ya kuwatuma, Yesu “akawapa amri juu ya pepo wachafu.” Nguvu hii ni dhidi ya nguvu chafu zinazotutenga na maisha ya Mungu, yaani, kukosa utu, ubinadamu, zinazopelekea kukoseana haki na kunyimana uhuru. Nguvu za kimisionari ni mwendelezo wa nguvu alizotoa Yesu aliyesema: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” Kwa hiyo nguvu hizo Kristu amewapa mitume na wakristu wote. Baada ya kupewa nguvu hizo “wakashika njia” yaani wakaanza “safari,” kwa Kigiriki limetumika neno “hodos” (hodon) lenye maana ya barabara au njia. Kwa kawaida watu wana njia zao za maisha wanazofuata.

Kumbe, mitume wanaagizwa kufuata njia anayoonesha Kristu. Katika njia ya maisha anayoonesha Yesu mitume wanaamriwa: “Wasichukue chochote isipokuwa fimbo tu.” Katika Injili ya Mateo mitume wanakatazwa kubeba fimbo, ikiwa kama silaha ya kujitetea wakati wa madhulumu. Hivi mitume hawatakiwi kujitetea ndiyo maana wanaambiwa “Msichukue wala fimbo” (Mt. 10:10). Kumbe hapa mitume wanaagizwa kuchukua fimbo ikiwa kama ishara ya nguvu na mamlaka yale waliyopewa na Kristo yaani, “Nguvu juu ya pepo wachafu”. Hivyo wanaagizwa waitegemee nguvu hiyo pekee waliyopewa na Kristo yaani Injili.

Hiyo ndiyo bakora yao ambayo ni mamlaka yatokayo kwa Mungu. Ukitegemea nguvu za Mungu huhitaji tena kubeba kitu kingine zaidi cha kujihami, ndiyo maana Yesu anawaamuru: “Msibebe mkate” kwani mwalimu alisema “mtu hataishi kwa mkate tu.”“Wala msibebe mkoba au mfuko” yaani, kutojikusanyia mali na kuweka akiba, bali kumtegemea Mungu tu kama tusalivyo katika Baba yetu: “Utupe leo mkate wetu wa kila siku.” Halafu“kutobeba hela vibindoni.” Mitume wanakatazwa kubeba “vijisenti” vibindoni kwa ajili ya akiba mashakani. Ndiyo maana Petro na Yohane waendapo hekaluni kusali Petro anamwambia yule mskini: “Mimi sina fedha wala dhahabu lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama uende” (Mdo 3:6).

“Msivae kanzu mbili.” Katika amri hii kuna utata, kwa sababu haiwezekani kuvaa kanzu mbili wakati mmoja. Kanzu au vazi linawakilisha nafsi ya mtu, hapa kanzu inawakilisha nafasi ya Kristo mwenyewe. Wanafunzi wa Yesu hawana budi daima wamwakilishe Mwalimu wao, yaani wamvae Yesu Kristo peke yake. Picha hii ya kuvaa imefuatwa sana katika utamaduni wa wakristo: “Mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.” (Waef. 4:24) au “Basi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana… zaidi ya hayo yote jivikeni upendo ndio kifungo cha ukamilifu.” (Wakol. 3:12-14).

Yesu anaagiza tena: “Mahali popote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo, hata mtakapotoka mahali pale” maana yake mitume wasilowee katika nyumba nzuri wanazokula vinono na kuzisahau nyumba za walalahoi. Aidha, “Na mahali popote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu kuwa ushuhuda kwao.” Yasemwa kwamba Wayahudi warudipo kwao toka nchi ya kigeni (kipagani) walikuwa wanakung’uta vumbi za miguuni mwao ili kutoingiza vumbi la nchi ya kipagani katika nchi yao takatifu. Yesu anatumia picha hiyo, kwa maana tofauti: “mkung’ute vumbi … kama ushahidi kwao” akimaanisha kuheshimu uhuru wa watu.

Katika kuhubiri wanafunzi wasiwe king’ang’anizi na kisisitizi kama mwuza mitumba hadi unaharibu uhuru wa mtu. Injili ya Yesu ni mwaliko na mapendekezo yanayoweza kukubaliwa au kukataliwa. Hivi kukung’uta vumbi “Uwe ushahidi kwao” kwamba kwa upande wako wewe umeshatoa ujumbe wakiukataa “kazi kwao.” Maana nyingine ya “kukung’uta vumbi” inatuonya sisi sote kuwa tunapoingia katika mahusiano na ulimwengu wa kipagani, au hata ulimwengu wa kisasa. Humo tunaweza kunaswa au kukwazwa na kuchafuliwa kwa vumbi zake. Yabidi kuwa waangalifu sana kutokuathirika na malimwengu au kwa maneno mengine, kumezwa na malimwengu huko utalia na kusaga meno!

Ndugu zangu, tumeitwa kuishi duniani na tunasafiri katika maisha haya. Tumepewa nguvu (fimbo) ya Habari Njema dhidi ya kila pepo mdhulumu wa haki na amani. Ili tufanikiwe kuitumia vyema fimbo hiyo yatubidi kumvaa Kristu tu. Tunaalikwa raia pamoja na viongozi wote wa dini na serikali, tusivae kanzu nyingi kwa wakati mmoja, yaani kanzu ya kibebari, ya kiutawala wa mabavu, ya unyonyaji, ya majivuno, pamoja na kanzu ya ibada au ya uongozi uliodhaminiwa na wananchi, bali, kiongozi waivae kanzu ya mamlaka waliyopata ana Mungu katika kuongoza raia kwa haki, kwani mamlaka yote yanatoka kwa Mungu. Kadhalika mkononi mwa kiongozi awe na fimbo ya mamlaka aliyopewa na Mungu na siyo kuitumia kama mkong’oto ili kuwashikisha wapinzani wake adabu!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.