2015-07-08 11:05:00

Jimbo kuu la Dar es Salaam lapata "majembe mapya matatu"


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walikazia kwa namna ya pekee umuhimu wa mahubiri wakati wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, kwani kwa njia yake katika Mwaka wa Liturujia, Mafumbo ya Imani na miongozo ya maisha ya Kikristo vinafafamuliwa kutoka Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu Francisko pia katika Waraka wake wa kichungaji Injili ya Furaha anaendelea kukaza kuhusu umuhimu wa Wakleri kujiandaa kikamilifu ili kuwatangazia watu wa Mungu Injili ya Furaha.

Askofu msaidizi Titus Mdoe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwapatia Daraja Takatifu Mashemasi watatu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam katika Ibada iliyoadhimishwa kwenye Parokia ya Mashahidi wa Uganda, Magomeni, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumanne tarehe 7 Julai 2015. Amewataka Wakleri kujiandaa vyema kuhubiri Neno la Mungu.

Lengo ni kuwawezesha waamini kulitafakari, kulifahamu na hatimaye kulimwilisha katika hija ya maisha yao ya kila siku, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mashiko na mvuto.

Askofu Mdoe anakaza kusema, Wakleri wanapaswa kuiga mfano wa Kristo mchungaji mwema, kwa kuhakikisha kwamba, wanawaonjesha waamini wao huruma na upendo pamoja na kuwapatia chakula kitakachowasaidia kuboresha maisha yao ya kiroho, yaani Neno la Mungu. Wakleri wanatekeleza dhamana na wajibu huu kwa niaba ya Yesu Kristo mchungaji mwema, kumbe hata wao wanachangamotishwa kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa yale wanayohubiri na kuyaishi.

Wakleri wanatakiwa kuonesha moyo wa unyenyekevu wanapowahudumia Watu wa Mungu, ili kweli watu wamtukuze Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Wakleri wameonywa kutomezwa na malimwengu kwa kutafuta utajiri wa mambo ya dunia, unaoweza kuwatumbukiza katika majanga ya maisha ya kiroho. Wakleri wajiandae vyema na kuwa tayari daima kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa ajili ya Familia ya Mungu, ili watu waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu, hususan wakati huu Mama Kanisa anapoajiandaa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Mapadre wapya ni Daniel Matungwa ambaye amepangiwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Keko; Padre Meinrad Kalikawe amepangiwa kuwa Paroko msaidizi wa Kitunda; Padre Raymond Mbaula anakuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mlandizi. Wakati huo huo, Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam amemteua Padre Aidani Mubezi kuwa Katibu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam; Padre Philip Tairo ameteuliwa kuwa Gombera wa Seminari ndogo ya Visiga na Padre Gerald Kamina anakuwa ni Mkurugenzi wa miito Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kardinali Polycarp Pengo amefanya pia mabadiliko makubwa kwa kuwahamisha Maparoko kutoka Parokia moja kwenda parokia nyingine pamoja na kuwapeleka Mapadre kadhaa masomoni, tayari kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji mpya Jimbo kuu la Dar es Salaam. Parokia teule mbili zimepandishwa hadhi na kuwa Parokia kamili nazo ni: Parokia ya Yohane Mwinjili, Mtakatifu Yohane Paulo II na Mtakatifu Thomas More.

Na mwandishi maalum,

Jimbo kuu la Dar Es Salaam. 








All the contents on this site are copyrighted ©.