2015-07-08 09:55:00

Hotuba ya Papa kwa Wahadhiri na wanafunzi: Chuo Kikuu ni Kitalu cha Maisha


Jumanne , Papa Francisko akiwa katika ziara yake ya kitume nchini Ecuador, baada ya kuongoza Ibada ya Misa majira ya asubuhi, ibada iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu wapatao milioni moja, majira ya jioni alikutana na Wasomi, wahadhari, wafanyakazi na wanafunzi pamoja na wawakilishi wengine katika dunia ya elimu na utamaduni  wa Chuo Kikuu Katoliki cha Kipapa cha Quito Ecuador.  Na baadaye majira ya saa kumi na mbili alikutana na viongozi na wawakilishi wa vyama vya kiraia mkutano uliofanyika  katika kanisa la Mtakatifu Francis la mjini  Quito.

Chuo Kikuu Katoliki cha Kipapa cha Quito ,  ni taasisi binafsi iliyo anzishwa mwaka 1946 na ni mali ya Jimbo Kuu la Quito. Chuo kinaendeshwa na Wajesuit  tangu kuanzishwa kwake. Na kina wanafunzi wasiopungua  wanafunzi 30 elfu wanaosoma katika vitivo 14 mbalimbali  wakijichotea utaalam mbalimbali tangu Sayansi ya dini,  sayansi ya asili na  kijamii,  usanifu, uhandisi, na uuguzi, pamoja na sheria na dawa.

Papa Francisko akihutubia  katika Chuo hiki,  alionyesha kufurahi kwamba, kwa karibia miaka 60 ya uwepo wake , kimesaidia kutoa elimu zaidi katika utume wa Kanisa kwa watu wa Ecuador . Na pia kwa makaribisho mazuri yaliyompa matumaini zaidi katika jinsi chuo hicho kinavyojali changamoto za wakati wetu , katika yote mawili, kama mtu binafsi na kama jamii kupitia kazi yao ya kuelimisha.

Papa alielekeza  hotuba yake katika mfano wa Mpanzi , kama ilivyoandikwa katika Injili ya Luka akisema , Yesu alitumia mfano huo ili watu waweze kumwelewa zaidi. Hakutaka kufundisha kama mtaalam aliyebobea , lakini daima alilenga kuufikisha ujumbe wake ndani ya mioyo ya watu, ili watu waweze kuelewa nini maana ya maisha matakatifu  hapa duniani.  Papa alieleza na kuainisha aina  mbalimbali za udogo, mbegu na matunda yaliyotajwa katika mfano huu wa Mpanzi  na mahusiano yake , kama pia ilivyoelezwa katika kitabu cha Mwanzo ,wakati Mungu anamwagiza binadamu kulima na kuitunza aridhi.

Hivyo akafafanua  kwamba , Mungu si tu alimpa binadamu  uhai lakini pia aridhi na viumbe vyote. Na kwamba  hakumfanya binadamu kuwa  mbia na au kuwa na mamlaka yasiyokuwa na  mipaka , lakini  mtenda kazi,  utume wa kuitumikia nchi.  Kwa maoni hayo, Papa ameitaja ardhi kuwa ni zawadi ya Mungu kwa binadamu. Ni zawadi ambayo binadamu hawezi kuitengeneza wala kuinunua . Ni zawadi iliyotolewa kwa binadamu na viumbe wote, ili kwamba pamoja nae Mungu  inakuwa ni mali ya wote.  Ni mahali ambapo Mungu ametupatia ili tuweze kushirikishana na wengine, kama ilivyo historia ya dunia daima ni kuitumikia  dunia  pamoja Mungu.  Ni kujenga dunia ya sisi na si dunia ya umimi, Papa Francisco ameeleza na kusema huu ni mwaliko wa siku zote  katika  maisha yetu. Mwaliko usiokoma.  

Papa aliendelea kuaasa kwamba, si tu tumealikwa kushiriki katika kazi ya uumbaji na kuilima aridhi lakini pia katika kukuza na kuendeleza dunia kwa mtazamo chanya wa kutunza viumbe na hali ya nchi. binadamu anatakiwa kuihudumia , kuilinda na kuwa walinzi namtetezi wa mazingira asilia ya dunia. Na leo hii jambo hili linakuwa na umuhimu zaidi  kuliko hata siku za nyuma. Hata hivyo , Papa akaonya dhidi ya binadamu kujiona yeye ndiye bwana wa dunia na kutenda bila kupima athari za vitendo vyake, utendaji wenye kuagamiza dunia na kutojali  hali ya baadaye.

Kwa kujali athari hizo, Papa Francisko amesisitiza,  binadamu ni lazima aendeleze mahusiano mazuri yaliyowekwa na Mungu tangu mwanzo wa uumbaji kati ya maisha na Mama Dunia , kati ya njia za maisha na zawadi hii tuliyopokea toka kwa Mungu. Ni hatari kubwa iwapo mazingira ya binadamu yatadidimia sambamba na mazingira asilia , na haiwezekani kupambana na kudidimia kwa mazingira bila kwanza kujua chanzo cha hali hiyo.  Papa ameasa na kumtaka binadamu kufanya mabadiliko ya maisha kwa ajili ya kulinda maumbile ya dunia.

Kwa maelezo hayo Papa alimezitaja Taasisi za  elimu kuwa ni vitalu, mahali ambapo kuna uwezekano kamili wa kupanda mbegu nzuri ya maisha katika akili za watu , kama ilivyo mbegu katika udogo mzuri inavyozaa matunda mazuri. Binadamu anatakiwa kutunzwa , kuilima na kuilinda aridhi. ARidhi yenye rutuba yenye kiu ya maisha.

Kisha Papa aliwahoji walimu iwapo wanatoa msaada kwa wanafunzi wao, wa kuwa na hisia  muhimu katika nia  wazi na uwezo wa kutunza dunia ya leo. Na iwapo wanasaidia wanafunzi kutambua  kwamba wakati huu wa masomo siyo tu haki yao , lakini  kama upendeleo ? Na kwa kiasi gani , masomo yao yanaweza kusaidia kujenga hamu ya mshikamano pamoja?  Na akiwageukia  wote, alisema, "Kama chuo kikuu, na  kama taasisi za elimu, na  kama walimu na wanafunzi,  changamoto kuu kwao wote ni  kujibu swali hili: Ni nini dunia  inahitaji toka kwao ? Na ndugu yangu  yuko wapi ?

Papa alikamilisha hotuba yake kwa kuomba uvuvio wa Roho Mtakatifu uweze  kuhamasisha na kuwaongozana  wote, kutoa mwaliko ,  fursa na uwajibikaji zaidi kwa ajili ya mema kwa wote.  Yeye ni Roho yule yule ambaye tangu siku ya kwanza ya uumbaji  aliwaongoza juu ya maji, aliyeleta mabadiliko na kuyafadhili  maisha. Yeye ni Roho yule yule aliyewapa wanafunzi uwezo siku ya Pentekoste. Papa amewahakikishia wote kwamba , Roho huyo hatuachi peke yetu , lakini daima hukaa ndani mwetu kama mmoja wetu , ili tuweze kukutana katika njia mpya ya maisha.  Roho huyo na awe siku zote na daima mwalimu wetu na rafiki yetu katika safari ya maisha yote.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.