2015-07-07 10:03:00

Vitendo vya kigaidi ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu!


Vitendo vya kigaidi ni ukweli ambao unaendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao; kiasi hata cha watu kukosa amani na utulivu. Vitendo hivi vimeharibu urithi mkubwa wa utamaduni na utambulisho wa watu pamoja na historia yao. Hadi sasa Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa  kwa kiasi kikubwa kudhibiti vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, hususan huko Mashariki ya Kati na katika baadhi ya nchi za Kiafrika.

Huu ni upembuzi yakinifu uliotolewa na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa ziliziko mjini Geneva, Uswiss wakati akichangia mada kuhusu madhara ya vitendo vya kigaidi pamoja na umuhimu wa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu. Vitendo vya kigaidi vinaendelea kusababisha madhara makubwa, kiasi hata cha kuhatarisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu na demokrasia.

Madhara ya vitendo vya kigaidi yataendelea kuongezeka maradufu, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, hawataweza kujifunga kibwebwe ili kupambana kufa na kupona na vitendo hivi. Hapa kuna haja pia ya kuhakikisha kwamba, mzizi wa vitendo vya kigaidi unabainishwa na kutafutiwa dawa. Ni jambo ambalo halikubaliki kamwe, kufanya mauaji, dhuluma na nyanyaso kwa kisingizio cha imani kali za kidini.

Kuna baadhi ya wanasiasa wanaotumia vitendo vya kigaidi, ili kufanikisha malengo yao kwa kuwajengea watu hofu na wasi wasi; lakini wanasahau kwamba, wanabomoa haki msingi za binadamu, wanawagawa watu kwa misingi ya udini usiokuwa na mashiko wala mvuto kiasi kwamba, maridhiano na mafungamano ya kijamii yanakuwa ni magumu sana, kwani watu wanaishi kwa wasi wasi mkubwa, jambo ambalo linajikita katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anakaza kusema, madhara makubwa yanayoletwa na vitendo vya kigaidi ni unyama dhidi ya: maisha, utu na heshima ya binadamu. Huu ni uhalifu dhidi ya binadamu na haki zake msingi. Hii inatokana na ukweli kwamba, ugaidi hautambui wala kuthamini utu wa binadamu na haki zake msingi. Lakini, ikumbukwe kwamba, mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi hayawezi kufanikiwa kwa njia ya mtutu wa bunduki peke yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.