2015-07-07 14:21:00

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 15 ya Mwaka B wa Kanisa


Mpendwa mwanatafakari unayenisikiliza, ninakuleteeni kama kawaida habari ya furaha kutoka katika kisima cha wokovu, ndilo Neno la Mungu. Leo tunatafakari Neno la Mungu katika Dominika ya 15 ya mwaka B. Mama Kanisa ametutengea chakula cha kiroho ambacho kwacho Mungu anasema, kushika wajibu wa kuhubiri Injili bila malipo wala matarajio yoyote isipokuwa kwa sifa na utukufu wa Mungu ndiyo wajibu wetu.

Katika somo la kwanza toka kitabu cha Nabii Amosi, tunamwona Nabii akikemea uozo katika nchi ya Betheli ambao umekomaa kwa sababu ya makuhani kulipwa mishahara minono na mfalme. Nabii Amosi wakati akikaripia uozo huo, kuhani Amazia badala ya kupokea ujumbe huo na kubadirisha maisha yake, anamwambia Amosi arudi na kuhubiri katika nchi yake ya Yuda. Kwa nini anamwambia hivyo, ni kwa sababu Amosi anapinga ufisadi na unyonyaji unaofanywa na matajiri wakibebwa na mfalme, na hivi Amazia anaogopa mfalme akisikia hilo, ataacha kumlipa mshahara mnono!

Mpendwa, Nabii Amosi anaitwa Nabii wa haki katika maisha ya jamii, kumbe mafundisho yake yanalenga kuondoa uovu unaoletwa na ukosefu wa haki. Anawaambia makuhani waachane na mambo ya mishahara na malipo yanayokandamiza habari njema na badala wamtegemee Mungu wakati huohuo wafanye kazi kwa ajili ya chakula chao cha kila siku. Wanaalikwa kupokea sadaka halali na si mlungura ambao ni kinyume cha mpango wa Mungu na Kanisa. Hivi leo katika jamii zetu inaweza kutokea makuhani wakaacha kukemea uovu katika jamii au nchi kwa sababu ya marupurupu fulani au kwa sababu ya woga na udhaifu, basi Amosi anatukumbusha kuwa makini katika kutangaza habari ya wokovu katika msingi wa haki na amani.

Katika somo la Pili. Mtume Paulo anapowaandikia Waefeso anawapatia ujumbe wa furaha akiwaambia jinsi Mungu katika Mwanae wa pekee Yesu Kristo alivyowapatia heri na baraka tele kwa ajili ya kushiriki uzima wa milele. Mtume Paulo anaonesha sifa kwa Mungu mwanzoni mwa barua na kisha zinafuata baraka mbalimbali ambazo Mungu aliziwaza kwa ajili yetu kabla ya kuumbwa Ulimwengu. Anaweka mbele ya Waefeso baraka ya kuwa wana wa Mungu, baraka ya wokovu na kuwa ukoo mteule na mwishoni kuurithi uzima wa milele.

Mpendwa, wito kwako ni kutambua kwanza heri hizo na kuzipokea kwa moyo wa shukrani. Ni kuweka nguvu zako zote katika kukuza mapenzi ya Mungu moyoni mwako na kisha kwa ajili ya watu wote yaani Wakristu na wasio Wakristo.

Katika Injili Bwana anawatuma Mitume wawili wawili wakaende kutangaza habari njema. Anawakabidhi mamlaka ya kutenda kazi yake pasipo kupungukiwa na kitu. Hata hivyo anawapa mashariti ya kufuata ili mamlaka aliyowakabidhi yaweze kuwa ya maana. Anawaambia wasibebe kitu chochote isipokuwa fimbo tu! Katika hali ya kawaida kama mmoja atakuwa na mizigo mingi si rahisi kutembea haraka na kwa muda mrefu! Pili kuna uwezekano wa kujenga kiburi kwa sababu ya vitu vyake. Jambo jingine la kutafakari ni juu ya kulipwa na hivi kuwepo na uwezekano wa kukosa nguvu kukemea mlipaji anapotenda kosa. Kwa maana hiyo basi, Bwana anawaambia Mitume wasilipwe kitu chochote isipokuwa Neema zake tu! Anawaambia wabebe fimbo tu, akiwa na maana ya mambo yote yanayosaidia kazi ya kitume isonge mbele.

Katika historia ya wokovu Waisraeli wanapotoka utumwani Misri, Musa atakuwa na fimbo ambayo ni ya kawaida lakini Mungu anamwambia gonga mwamba kwa fimbo hiyo na Musa anapofanya hivyo mara moja maji yanatoka! Hii ni kuonesha nguvu ya Mungu ambayo hujionesha katika vitu dhaifu. Kumbe fimbo ni alama ya nguvu ya Neno la Mungu.

Mitume wanapotenda kazi kwa vyovyote vile wanahitaji kula na kupata maji, basi Bwana anawaambia mtakula katika nyumba zao mahali mtakapokuwa mnafanya kazi ya kutangaza habari njema. Kumbe ni wajibu wa Jumuiya, kuwatunza Mitume na kama haitafanya hivyo basi jumuiya hiyo haitapata heri na baraka za Mungu. Hivi wajibu wetu ni huohuo kuwatunza Mashemasi, Mapadre, Maaskofu na Baba Mtakatifu kwa sababu wametumwa kwa ajili ya kazi ya Bwana, na wanaalikwa kuifanya kwelikweli!!

Mitume wanatumwa wawiliwawili kwa sababu kazi ya kitume ni kazi ya Jumuiya si ya mtu binafsi, ni kazi ya Kanisa kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Kumbe kamwe isitokee mmoja akajisikia kuwa kazi ya kitume ni kazi ya Makasisi tu bali ni kazi ya wabatizwa wote.

Mpendwa zipo namna mbalimbali za kushiriki kazi ya kitume, yaani kwa njia ya sala katika jumuiya, kwa njia ya kutoa michango ili kusimika kazi ya kimisionari na sisi wenyewe kushiriki ana kwa ana kazi ya Bwana siku kwa siku mpaka mwisho wa maisha yetu. Kumbuka ukarimu katika kazi ya kimisionari ni wa maana sana na utakupatia tija na ni mlango wa uzima wa milele.

Ninakutakia heri na baraka tele za Bwana wetu Yesu Kristo zikulinde na kukupa nguvu kwa ajili ya kazi ya Bwana ambayo haina malipo hapa duniani kwa namna ya mshahara isipokuwa kumjua Kristo na taifa lake na hivi kukirimiwa neema za mbinguni.Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.