2015-07-07 11:05:00

Salaam za Papa kwa mhadhara uliokusanyika katika Kanisa Kuu la Quinto


Jumatatu Julai 6 majira ya jioni , Baba Mtakatifu Francisco akisalimia mhadhara wa watu waliokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Quinto, alitoa mwaliko kwa watu wote waige mifano ya maisha ya Watakatifu, kwa ajili ya amani na utulivu duniani.  Papa alisema Yuko Equador kama mhujaji , aliyekwenda kushiriki pamoja na watu wa taifa hilo, furaha yao ya kueneza Injili. Na kwamba alianza safari hii Vatican kwa kutoa heshima zake kwa sanamu ya Mtakatifu Mariana de Jesus , iliyowekwa kando ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro , kwa heshima ya taifa la Equador, ili watu waweze kujifunza kutoka maisha yake.

Papa alieleza kwa kifupi, ushujaa na wema  katika  sadaka ya maisha ya Mtakaifu Mariana de Jesus akitaja kuwa ni harufu nzuri ya maua waridi katika maisha ya waamini . Na kwamba, kwa sanamu yake kuwa ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, ikipambwa na shada la Maua , inamwakilisha Bwana ndani ya Moyo wa Kanisa, pamoja mazuri yote ya watu wote wa Equador. Papa alieleza na kutoa mwaliko kwa wote kuiga somo kutoka maisha ya Mtakatifu Mariana de Jesus kama yalivyo pia maisha ya watakatifu wengine Narcisa na Mwenye Heri Mecedes wa Yesu wa Molina .

Papa Franciko aliendelea kutafakari juu ya maisha  ya  Watakatifu, akitazama maisha leo hii na kuhoji ni wangapi leo hii wanajua umuhimu wa kujali mahitaji ya wengine kama watoto yatima . Ni wagapi wanaoona dhiki za watu wengine hasa walio sahauliwa katika maendeleo ya kijamii na kutupwa pembezoni? Ni wangapi wanaoona shida za vijana kukosa ajira  na ni wangapi wanaweza toa huduma kwa uvumilivu hasa kwa makundi dhaifu kama wazee na wagonjwa?

Papa alihoji na kutoa mwaliko kwa wote kufuata mfano wa Mtakatifu Narcisa na Mercedes. Amesema si kazi ngumu kuyaiga maisha yao iwapo watakuwa na Mungu katika maisha yao. Hakuna linaloshindikana kwa kumtanguliza Mungu katika maisha yote. Mungu yu pamoja nasi . Watakatifu wanatuonyesha sisi upendo mkuu waliokuwa nao kwa ajili ya huduma kwa wengine. Na ndivyo walivyoguswa na maisha ya watu wengine wakioona mateso ya mwili wa Yesu katika maisha ya watu wake, kama ilivyoelezwa katika waraka wa Kichungaji wa Injili ya furaha.

Papa aliendelea kusema, Watakatifu walitenda kwa kushirikiana na wengine kama ilivyokuwa katika kazi ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Quinto , na ndiyo jamii mahalia ilivyofanya kazi zake kimya kimya pamoja na wengine kwa ajili ya manufaa ya jamii bila kutafuta faida binafsi au sifa.

Papa alieleza na kumwomba Mungu , amjalie kila mmoja , kama yalivyoinuliwa  mawe ya Kanisa Kuu na wahenga , ndivyo pia kwa wakati huu, waweze kushikamana bega kw abega kubeba matatizo na shida za wengine, vivyo hivyo katika kazi za  kuleta uponyaji na msaada katika maisha ya ndugu zetu wake kwa waume, wanaoshindwa kujiinua wenyewe kimaisha -kiroho na kimwili pia.

Papa alikamilisha hotuba kwa kusema , yuko hapo pamoja nao kushirikishana furaha yenye  kuijaza mioyo , kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Isaya” Jinsi ilivyo vizuri kuwa  juu ya milima , miguu yake aletaye habari njema .  Huu ndio uzuri wa tunaotakiwa kuutangaza , kama ilivyo harufu nzuri ya Kristo,  katika sala zetu, katika  kazi zetu na katika kuhudumia wahitaji. Hiyo ndiyo furaha ya kuinjilisha na mmebarikiwa kwa kutenda hayo.  (Yn.13:17)

 








All the contents on this site are copyrighted ©.