2015-07-07 09:02:00

Papa asema : mazuri zaidi yaja kwa ajili ya Familia


(Vatican Radio) Jumatatu,  Papa Francisko  akiwa katika  siku ya Pili ya ziara yake ya Kitume Amerika ya Kusini, majira ya asubuhi aliongoza ibada yake ya kwanza hadharani,  katika mji wa Guayaquil Equador, ibada iliyohudhuriwa na umati wa watu zaidi ya milioni moja. Homilia yake ililenga kuwatia nguvu waamini kwamba kila tunaposali na kunyanyua sauti zetu kwa Mungu hofu na mashaka yetu huondolewa . Sala huyahuisha juu ya yote yanayotuumiza au kuudhi au kutufadhaisha. Maombina sala  hutuweka katika nafasi yakujali pia mahitaji ya wengine.

Baba Mtakatifu  alieleza hilo wakati akitoa tafakari juu ya muujiza wa Kana , muujiza wa kwanza wa Yesu,  alipogeuza maji kuwa mvinyo, kama ilivyoelezwa katika somo la Injili ya Yohana , ambamo Mama Maria anaonyesha kujali mahitaji ya  watu na kuomba kwa Yesu akisema ; watu hawana mvinyo, na Yesu anatoa jibu akirejea saa ya mateso yake.

Ishara ya muujiza wa Kristo huko Kana - kugeuza maji kuwa mvinyo , Papa anasema, inaonyesha jinsi Mama Maria, anavyojali  mahitaji  yetu. “Mama Maria alikuwa makini, na aliweka hofu na mashaka yake kwa Mungu na kutenda kwa uangalifu na ujasiri."

Sura hii ya Maria katika kujali mahitaji ya Maarusi huko Kana , Papa Francisko alisema, inaonyesha jinsi  Maria alivyojali mahitaji ya wengine, Maria hakujifungia binafsi katika shida zake, lakini alijali pia mahitaji ya wengine. Papa aliianisha hali ya wakati huo wa Arusi ya Kana na  hali nyingi zinazoonekana leo hii,  kwamba "mvinyo" inakuwa ni  ishara ya furaha, upendo, na mengine mengi  kutokuwepo. Alihoji ,   ni vijana wetu wangapi wanaojisikia hawana makazi?  Na ni  wanawake wangapi wanaobaki wamemezwa na hali ya  huzuni na upweke baada ya kupoteza wapendwa wao au wakati hali za kijikimu kimaisha zinapokuwa mbali nao? Na ni wazee wangapi, wanaotelekezwa nje maadhimisho ya kifamilia, kutupwa kando na  kila siku wakitamani  walau kupata upendo kidogo? "

 Papa alijibu  hoja hizo kwa kurejea  utendaji wa Mama Maria katika Injili, jinsi alivyojali mahitaji ya wengine , alivyotafuta jibu katika  kukosekana kwa  mvinyo. Alimwendea  Yesu kwa ujasiri, na kuomba. Papa Francisko anasema, Maria anatufundisha kuweka familia zetu mikononi mwa Mungu, kuomba, kuwasha matumaini mapya wakati tunapoona kuna  matatizo, kuna upungufu. Ni kuweka wasiwasi wetu kwa  Mungu. Na sala na maombi , aliendelea, daima hutuhuisha  nje ya wasiwasi na mashaka yetu.

Homilia ya Papa iliendelea kuitaja familia kama shule ya sala , kama yalivyokuwa maneno ya Maria kwa wahudumu wa arusi , lolote atakalowaambia fanyeni.  Baba Mtakatifu anasema , huu pia ni mwaliko kwetu kufungua mioyo yetu kwa Yesu, aliyekuja kutumikia na siyo kutumikiwa. Na kwamba katika mfano huu sisi tunajifunza kuwa ndani ya familia ni  kuwa watumishi wa mtu mwingine, na ni mahali  ambamo  hakuna anayekataliwa. Familia ni mtaji bora  wa kijamii". Familia haina mbadala, na haiwezi kulinganishwa na  taasisi nyingine.  Papa Francisko alisisitiza na kutoa mwaliko wa nguvu kwa jamii  kutetea familia, akisema ni lazima  familia isaidiwe na kuimarishwa."

Familia, aliendelea kusema, pia ni "Kanisa dogo, 'Kanisa la ndani' ambamo, pamoja na maisha, pia ni mjumbe wa huruma na huruma ya Mungu.  Pamoja na familia zetu wakati mwingine kuwa nje ya mategemeo yetu , au kuwa na picha mbaya tusiyotegemea  hata hivyo, kila siku ndani ya familia  hapakosekani  miujiza kwa  madogo  yanayofanyika.  Katika familia zetu wenyewe na katika familia mkubwa  ambamo sisi sote tunahusika,  hakuna anayepaswa  kutekelezwa  kando, au wa kuonekana kama hana thamani.  Papa Francisko alieleza na kuomba  sala kwa ajili ya Sinodi juu ya familia, ili Kristo anaweza kuyabeba  yote , hata yale  yanayoonekana kwetu kutofaa,  kashfa, au vitisho, na kuyageuza kuwa miujiza.

Papa  amesema , ni jambo jema kujua jinsi Yesu anavyoguswa na mahitaji yetu . Na hivyo tunapata kujua kwamba Yeye daima yu pamoja nasi  wakati tunapopungukiwa, wakati wa  dhiki na katika furaha pia . Papa alielezana kurejea ombi la Maria kwa Yesu , hawana Mvinyo. Pamoja na mfano wa Maria katika kujali mahitaji ya wengine pia Papa alirejea mifano wa maisha watakatifu Narcisa na Mercedes , akisema si kazi ngumu kuyaiga maisha yao iwapo tutakuwa na Mungu ndani mwetu. Wao walitimiza kazo yao na wanatuonyesha hakuna kinacho shindikana iwapo tu pamoja na Mungu. Wanatuonyesha upendo wao mkuu kwa maisha ya wengine , maisha ya kila siku wakiguswa na mateso ya mwili wa Kristo kwa wengine., kama ilivyoelezwa pia katika Waraka wa Kichungaji wa Injili ya Furaha.

Papa anasema, watakatifu hawa  hawakufanya kazi zao kwa kujifungia wenyewe binafsi , lakini walitenda kwa kushirikiana na wengine , ili kwa njia hiyo , inakuwa ni njia yetu sote , njia asilia , kutenda katika hali ya ukimyakimya sambamba na jamii , kwa manufaa ya jamii nzima bila kutafuta faida binafsi au sifa binafsi .

Ukosefu wa Mvinyo amefafanua Papa  Francisko unaweza kuwa ukosefu wa ajira, ukosefu wa afya za kimwili, au uwepo wa mapungufu katika hali zingine za maisha. Mama wa Yesu hakudai kwa nguvu lakini alionyesha kwa upendo upungufu uliokuwepo . 

 Baba Mtakatifu alihitimisha hotuba yake kwa kuonyesha ukweli kwamba, wakati wa harusi ya Kana, yaliyo mazuri zaidi yalikuwa  bado kutolewa  kwa ajili ya  familia.  Kama Mungu alivyokwisha sema , tafuteni nanyi mtapata , daima ni kutafuta  hadi pembezoni, wale walioishiwa na mvinyo , wale wanao wanaotafuta kinywaji , baada ya kuishiwa , wale waliokata tamaa . Yesu anausikia udhaifu wao , na kutoa mvinyo ulio bora zaidi hata kwa wale wanaosikia kuvunjika moyo. 








All the contents on this site are copyrighted ©.