2015-07-07 12:02:00

Kanisa Katoliki ni mdau mkuu wa maendeleo na ustawi wa jamii nchini Tanzania!


Dr. James A. Msekela, Balozi wa Tanzania nchini Italia na mwakilishi wa Tanzania katika Mashirika mbali mbali ya Umoja wa Mataifa mjini Roma katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kuwapongeza Wamissionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika lao. Hili limekuwa ni tukio la neema, baraka na faraja lililowawezesha mahujaji 54 kutoka Tanzania kufika na kushiriki maadhimisho ya Jubilei hii hapa Roma.

Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu linapoadhimisha Jubilei ya miaka 200 ni kielelezo makini kwamba, limekomaa kiimani dhana inayomjionesha kwa namna ya pekee katika huduma inayomlenga mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa Katoliki nchini Tanzania limekuwa ni mdau mkuu wa ustawi na maendeleo ya watanzania katika sekta ya elimu, afya, maji na ustawi wa jamii. C.PP.S nchini Tanzania inaendelea kuchangia katika huduma ya elimu kwa kuwa na shule nzuri zinazotoa elimu bora na inayozingatia viwango. Lengo kuu ni kumwendeleza mwanadamu: kiroho na kimwili, huo ndio ukombozi wa kweli.

Dr. James Msekela anasema, C.PP.S. kupitia kwenye Mradi wao wa maji, “C.PP.S. Mission Water Project” umekuwa ni msaada mkubwa nchini Tanzania hususan kwenye maeneo yenye ukame. Wamissionari wamejitahidi kupeleka huduma ya maji safi na salama katika maeneo ambayo Serikali ilikuwa haijafanikiwa kufika. Kwa hakika wamekuwa ni wadau wanaopaswa kuungwa mkono katika juhudi za kumwendeleza mtanzania kwa hali na mali.

Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu Vikarieti ya Tanzania hapo tarehe 8 Agosti 2015 litapandishwa adhi na kuwa Kanda inayojitegemea ndani ya Shirika. Ni tukio la kihistoria kwa Kanisa Barani Afrika linalobeba dhamana na changamoto zake. Hiki ni kielelezo kwamba, Shirika nchini Tanzania limekomaa na sasa linaweza kujiendesha lenyewe kwa kuwa na viongozi wake pamoja na kujitegemea katika masuala ya kiuchumi.

Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kulitegemeza Shirika, kwa kutambua kwamba, kwa miaka mingi limekuwa likipokea misaada ya hali na mali kutoka ng’ambo, sasa umefika wakati kwa watanzania wenyewe kulitegemeza Kanisa mahalia kwa kutumia rasilimali watu, vitu na fedha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wengi anasema Dr. James Msekela, Balozi wa Tanzania nchini Italia.

Na Padre Richard A, Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.