2015-07-07 09:24:00

Boko Haram bado ni tishio kubwa Nigeria!


Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, kiasi kwamba, watu wanaendelea kuwa na wasi wasi juu ya usalama wa maisha yao kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara. Rais Muhammadu Buhari amesema kwamba, mashambulizi haya ni vitendo vya kinyama vinavyofanywa na Boko Haram na kwamba, kuna haja ya kuwa na ushirikiano wa kimataifa, ili kuhakikisha kwamba, Boko Haram inashikishwa adabu.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema kwamba, Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram ni watu ambao wamepoteza utu na heshima ya binadamu; kwao maisha si kito cha thamani kwani wamedhamiria kusababisha maafa kwa watu na mali zao ndio maana hawana hata aibu ya kuwauwa watu wakiwa kwenye nyumba za Ibada, shuleni au sokoni. Ni watu ambao kwa hakika wanakosa utu.

Boko Haram inaonekana kuwashughulikia wale wote wanaopingana nao ndiyo maana wanashambulia hata misikiti ambamo hawapewi ushirikiano wa kutosha. Hapa wananchi wote wa Nigeria wanapaswa kushikamana kwa dhati ili kupambana na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, kwani hiki ni kikundi kinachoonesha msimamo mkali wa kiimani, jambo ambalo ni hatari kwa mfungamano na maridhiano ya kijamii. Waamini wa dini mbali mbali wajenge umoja, upendo, mshikamano na udugu na kwamba, tofauti zao za kidini zisiwe ni chanzo cha choko choko, kinzani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Wananchi wa Nigeria hadi sasa wanashindwa kuelewa kazi inayotekelezwa na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwa kama kila siku Boko Haram inashambulia na watu wanaendelea kupoteza maisha na mali yao. Serikali ya Nigeria haina budi kujifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, inawahakikishia wananchi wake ulinzi na usalama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.