2015-07-06 09:28:00

Wanafunzi wanahitaji elimu makini kwa ajili ya makuzi na maendeleo yao!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria lina ishauri Serikali ya Nigeria kuanzisha tena elimu ya dini na maadili shuleni, ili kusaidia kuwafunda vijana wa kizazi kipya  juu ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii, tayari kujisadaka kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa nchi yao. Hii ni changamoto ambayo imetolea hivi karibuni na wakuu wa idara ya elimu kutoka katika Majimbo ya Kanisa Katoliki nchini Nigeria.

Wajumbe kwa pamoja wamewataka wadau mbali mbali wanaosimamia na kuendesha shule zinazomilikiwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki nchini Nigeria kuhakikisha kwamba, wanakuwa waaminifu, wakweli na wabunifu katika matumizi ya fedha ya Kanisa, ili kuondokana na kishawishi cha: rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya Kanisa, jambo ambalo ni fedhea sana katika maisha na utume wa Kanisa.

Wajumbe wamekubaliana kimsingi kwamba, shule ambazo zinamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki lazima ziwe na utambulisho wake makini unaojikita katika, imani, maadili na utu wema. Kuwepo na alama wazi zinazozitambulisha shule hizi ndani na nje ya majengo yake, sanjari na kuhakikisha kwamba, wadau wote wa elimu Katoliki wanashirikiana na kusaidiana kutekeleza majukumu yao mbali mbali. Dhamana hii haina budi kwenda sanjari na majiundo endelevu ya wadau wa sekta ya elimu nchini Nigeria.

Wajumbe wamekazia umuhimu wa sekta ya elimu kuwaandaa wanafunzi katika somo la hisabati ambalo kwa miaka mingi limeonekana kuwa ni kizingiti kikubwa katika mchakato wa maboresho ya elimu nchini Nigeria. Wajumbe wanakumbusha kwamba, hisabati ni muhimu sana kwa kila mwanafunzi kwani huu ni msingi wa maisha kwa sasa na kwa siku za usoni. Wanafunzi wanapaswa pia kuelimishwa kuhusu umuhimu wa kuwa na matumizi bora na sahihi ya mitandao ya kijamii kama njia ya mawasiliano na kujipatia ujuzi na maarifa.

Wajumbe wanalitaka Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kuhakikisha kwamba, linatoa mishahara ya haki kwa kazi zinazofanywa na walimu, ili walimu nao waweze kuchangamotishwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wanafunzi wa Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.