2015-07-06 09:45:00

Papa apokewa kwa shangwe na heshima zote Ecuador


Jumapili 5 Julai 2015,  Baba Mtakatifu Francisco majira ya asubuhi alianza ziara ya kitume kwa nia ya kutembelea mataifa matatu ya Amerika ya Kusini , Ecuador, Bolivia na Paraguay kama shahidi wa Injili. Ziara inayomchukua muda wa siku tisa,  hadi tarehe 13 Julai atakaporejea Roma.

Jumatatu 6 Julai , Papa akiendelea na ziara hii katika siku ya Pili, ana ratiba ya matukio mawili makubwa kwanza itakuwa ni kuongoza Ibada ya Misa katika uwanja wa Guayaguil majira ya saa tano kwa saa za Ecuador , ambayo ni majira ya jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Na baadaye majira ya jioni kwa saa za Ecuador, Papa atakutana na umma wa Ecuador katika Kanisa Kuu la mjini Quito. 

Hapo siku ya Jumapili, Papa Francisco , mara baada ya kuwasili katika uwanja wa  ndege wa Marisal Sucre  Quito Ecuador , baada ya kusafiri mwendo wa kilomita 10,103 kwa muda wa saa 13 hewani kwa ndege ya Altalia, alilakiwa  na wenyeji wa Ecuador wakiongozwa na  Nuncio wa Papa Ecuador, AskofuMkuu Giacomo G. Ottonello, Askofu wa Jina wa Sasabe,na Rais wa Ecuador Raffael Correa, ikifuatiwa  hafla fupi ya makaribisho.

Mahali hapo, Papa kwa heshima na taadhima alitoa hotuba yake fupi, ambamo , alishukuru kwa majaliwa yake Mungu yaliyo mwezesha tena kurudi Amerika ya Kusini, kuwa tena pamoja na watu wa taifa zuri la Ecuador. Na alikiri kujisikia furaha na kushukuru kwa joto joto la makaribisho mazuri, akisema ni  ishara ya ukarimu na wema wa  watu wa Ecuador.

Na kwa namna ya kipekee alitoa shukurani zake kwa Rais Raffael , na viongozi katika mamlaka serikalini , pamoja na ndugu zake  katika dekania ya maaskofu, waaminifu wa Kanisa nchini Ecuador, na  wale wote ambao wameweza kuifunua mioyo na nyumba na taifa lao kwa ukarimu, kwake yeye Papa na wote alioandamana nao.Papa  alionyesha kuthamini  na kutoa shukurani  za dhati.

Aliendelea kusema, licha kwamba siku za nyuma alitembelea taifa hilo kwa mara kadhaa kwa sababu za kichungaji, katika ziara hii amekwenda kama shahidi wa huruma ya Mungu na imani katika Yesu Kristo.Papa alishuhudia jinsi kwa karne na karne,  imani kwa Kristo , imeweza tengeneza  umbo la utambulisho wa  Wakristo  katika taifa la Ecuador na kuzaa matunda mengi mazuri, wakiwemo Mtakatifu Mariana de Yesu, Mtakatifu Miguel Febres, Mtakatifu Narcisa de Jesús na Mwenye Heri Mercedes de Jesús Molina, aliyetajwa kuwa Mwenye Heri huko  Guayaquil miaka thelathini iliyopita, wakati wa ziara ya Papa Yohane Paulo II. Hawa, kama ilivyo  na wengine kama wao, waliishi imani yao kwa nguvu na shauku, na kwa matendo yao ya huruma wao wamechangia kwa njia mbalimbali ,  kuboresha jamii Ecuador katika  siku zao.

Papa kisha aliugeukia wakati wetu akisema, katika wakati wetu wenyewe pia, tunaweza kupata katika Injili,  ufunguo wa kukabiliana na changamoto za kisasa, kuheshimu tofauti, kukuza mazungumzo na ushirikiano kamilifu, kwa ajili ya kumwendeleza kila biandamu kiroho na kimwili pia ili  yaliyokwisha anzishwa tayari, eyaweze kuhakikisha maisha bora ya baadaye kwa kila mtu, na  kwa namna ya kipekee  hasa kwa ajili ndugu wake kwa waume wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. Papa alimhakikishia Rais Raffael, uwajibikaji na ushirikiano wa kanisa katika kmwendeleza mtu kiroho na kimwili pia. 

Papa alieleza na kukiri kuianza  ziara yake akiwa amejawa na  msisimko na matumaini makubwa kwa  siku za usoni, kwa kuweka  tumaini lake kwa Wakristo  wenye kumtambua Kristo kama Mwanga unaomulikia maisha yao kama ulivyo mwanga wa  jua, na mwanga wa mwezi kama Kanisa,  jamii ya waamini. Alisisitiza hakuna mtu mwingine anayeleta ukombozi , isipokuwa Yesu Kristo, kwa mwanga wake ambaye ni yeye mwenyewe. Papa alieleza na kuomba ili kwamba ,  siku zijazo, ziweze  kutufanya sisi sote kuutambua waziwazi mwanga huu na kuwa karibu nao kama vile jua linavyotuangazia kutoka juu.  Na ili kila mmoja wetu, aweze kupata tafakari za kweli juu ya  mwanga wa Kristo  na upendo wake.

Tokea hapo Papa alipeleka salaam zake za upendo kwa watu wote wa  Ecuador, kutoka pande zote za msitu ya Amazoni hadi katika visiwa vya Galapagos ,akisema  pasiwepo kamwe  mtu asiyetoa shukurani zake kwa Mungu kwa  majaliwa yake yote. Na aliwataka  kwamwe wasipoteze   uwezo wa kulinda mazuri yote ya nchi yao, hata yale yanayo onekana kuwa madogo na mepesi, ikiwemo  huduma kwa watoto wao na wazee wao, na pia wawe na matumaini kwa vijana na kuwa  daima kuheshimu watu wao na uzuri wa umoja wa nchi yao.   Papa alieleza na kuomba Moyo Mtakatifu wa Yesu na Moyo Safi wa Maria, ujalie kila neema na baraka kwa taifa la Ecuador. 








All the contents on this site are copyrighted ©.