2015-07-06 13:25:00

Jubilei ya miaka 50 ya Upadre na Miaka 36 ya huduma Tanzania!


Padre Ernest Gizzi mmissionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, Jumamosi, tarehe 4 Julai 2015 ameadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya Upadre sanjari na mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi Yesu na Mtakatifu Gaspar Del Bufalo. Ibada ya Misa Takatifu imehudhuriwa na mahujaji kutoka Tanzania ambao wamekuwepo mjini Roma kushiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu linalofanya utume wake nchini Tanzania na Guinea Bissa kwa sasa kwa upande wa Bara la Afrika.

Ibada ya Misa imeongozwa na Padre Ernest Gizzi ambaye ameishi na kufanya utume wake nchini Tanzania kwenye Majimbo ya Singida na Jimbo kuu la Dar es Salam kwa muda wa miaka 36. Hivi karibuni alilazimika kurejea nchini Italia kutokana na afya yake kuwa mbaya. Padre Oliviero Magnone, Mkuu wa Kanda ya Italia amemshukuru na kumpongeza Padre Gizzi kwa huduma na utumumishi alioutoa kwa Familia ya Mungu nchini Tanzania katika kipindi cha miaka 36 ya maisha yake.

Katika mahubiri yaliyotolewa na Padre Walter Milandu, moja ya washauri wakuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Takatifu, amewashukuru na kuwapongeza Wamissionari waliojisadaka kwa ajili ya huduma ya maisha ya kiroho na kimwili kwa watanzania bila kuwasahau maskini na wote waliokuwa wanakusumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni kutokana na kuguswa kwao na shida na mangaiko ya watanzania, wakaamua kuanzisha Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, wazo lililotolewa na Padre Genaro Cespites ambaye pia ameadhimisha kumbu kumbu ya miaka 62 ya Upadre. Huyu ni muasisi wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Jimbo Katoliki la Singida, hospitali ambayo inaendelea kutangaza na kusimamia Injili ya Uhai. Padre Evaldo Biasini anakumbukwa na wengi hasa kwa kuwa mstari wa mbele kwa huduma kwa maskini, akaguswa na mahangaiko ya wagonjwa wa Ukoma, Kijiji cha Sukamahela, kilichoanzishwa na Serikali ya Tanzania, lakini kutokana na ukata, kikatelekezwa, lakini leo hii, ni Kijiji ambacho kinaendelea kutoa huduma makini kwa wagonjwa wa Ukoma pamoja na familia zao, alama ya ushuhuda wa matumaini na mapendo.

Naye Bwana Humphrey Lyimo, mwamini mlei kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa niaba ya mahujaji kutoka Tanzania, wamemshukuru Mungu kwa uwepo na huduma makini inayotolewa na Wamissionari wa Damu Takatifu ya Yesu wakisukumizwa na tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu pamoja na kuguswa na mahitaji ya watanzania, leo hii watu wengi wameonja huduma mbali mbali zinazotolewa na Wamissionari hawa nchini Tanzania: hususan katika sekta ya afya, elimu, ustawi na maendeleo ya jamii, bila kusahau kwamba, huduma zote hizi ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.