2015-07-06 11:28:00

Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida awekwa wakfu na kusimikwa!


Askofu mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, Jumapili tarehe 5 Julai 2015 amemweka wakfu na hatimaye kumsimika Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida, tayari kuanza kutekeleza dhamana ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, Jimbo Katoliki Singida. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki Singida.

Katika salam zake za shukrani, Askofu Edward Mapunda amekaza kusema, Mwenyezi Mungu humteua kiongozi kwa wakati, muda na malengo yake, tayari kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wake. Anamshukuru Mwenyezi Mungu na kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteuwa kuliongoza Jimbo Katoliki Singida.

Anamshukuru Hayati Askofu Bernard Mabula aliyemlea na hatimaye kumpatia Daraja Takatifu la Upadre. Anamshukuru Askofu Desiderius Rwoma wa Jimbo Katoliki Bukoba na Msimamizi  kitume wa Jimbo Katoliki Singida kwa malezi na tunza ya kibaba aliyomkirimia wakati alipokuwa Seminari ndogo ya Rubya, Jimbo Katoliki Bukoba.

Askofu Mapunda anamshukuru kwa namna ya pekee kabisa Askofu Rwoma aliyefanya naye kazi kwa karibu sana alipokuwa mtunza fedha wa Jimbo Katoliki Singida. Amejifunza kutoka kwake, upole, wema, upendo, uvumilivu na majitoleo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu Jimboni Singida. Ni kiongozi anayejisadaka sana ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Furaha inawafikia watu wengi zaidi, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.

Askofu Mapunda anatambua na kukiri mambo mengi yaliyotekelezwa na Askofu Rwoma alipokuwa akiliongoza Jimbo Katoliki Singida na kwamba, atayaenzi na kuyaboresha zaidi. Anawataka watanzania kuendelea kushikamana na kuliombea Taifa ili liweze kufanikisha uchaguzi mkuu, ili Tanzania iweze kuwapata viongozi ambao ni wachamungu, wazalendo, waadilifu, wakweli na wawazi, watu ambao wako tayari kusimamia utu na heshima ya binadamu, ustawi na maendeleo ya Watanzania wote.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Francesco Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, amemtaka Askofu Edward Mapunda kuwa kweli ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia; awe ni chombo cha haki, amani, upendo na mshikamano. Aoneshe ushirikiano na umoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na familia ya Mungu nchini Tanzania. Awe makini na watu wanaotaka kuligawa taifa kwa mafao yao binafsi.

Askofu mkuu Padilla amemshukuru na kumpongeza Askofu Rwoma kwa kulisimamia kikamilifu Jimbo Katoliki la Singida hadi hatua ya kumpata Kiongozi wake mkuu. Askofu Edward Mapunda amewekwa chini ya usimamizi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kusaidia katika maisha na utume wake kwa Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Singida.

Wakati huo huo, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, Jimbo Katoliki la Singida kwa sasa linamwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kumpata Askofu Edward Mapunda. Ameitaka Familia ya Mungu Jimboni Singida kuonesha ushirikiano na mshikamano na Askofu wao mpya, ili Kanisa liendelee kustawi na kuwahudumia watu kwa moyo wa unyenyekevu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linamshukuru na kumpongeza Askofu Rwoma kwa huduma makini aliyoifanya kwa Jimbo Katoliki Singida kama Askofu na Msimamizi wa kitume. Ni wajibu wa Askofu Edward Mapunda kuendeleza utume huu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Watu wa Mungu Jimboni Singida. Baraza la Maaskofu linamwombea na kumkaribisha miongoni mwao. Askofu Mapunda anakuwa ni Askofu wa tatu kuliongoza Jimbo Katoliki la Singida.

Katika hotuba yake, Parseko Kone, Mkuu wa mkoa wa Singida, amewataka wananchi wa Singida kuonesha moyo wa ushirikiano na mshikamano na Askofu Edward Mapunda. Serikali inamhakikishia ushirikiano wa dhati kwa ajili ya maendeleo endelevu ya wanasingida wote. Amewaomba viongozi wa kidini nchini Tanzania kuendelea kuombea misingi ya: haki, amani, utulivu na maridhiano wakati huu Tanzania inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu na baadaye kura ya maoni. Anawataka watanzania wenye sifa za kupiga na kupigiwa kura kuhakikisha kwamba, wanaitumia vyema haki yao.

Na Rodick Minja,

Dodoma. 








All the contents on this site are copyrighted ©.