2015-07-05 09:11:00

Zingatieni sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuokoa maisha ya watu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, Jumapili tarehe 5 Julai 2015 linaadhimisha Siku ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayoongozwa na kauli mbiu: busara ni kiongozi mkuu uwapo barabarani. Katika ujumbe ulioandikwa na Askofu Ciriaco Benavente Mateos, Mwenyekiti wa Tume ya Wahamiaji Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania anawaalika madreva na watumiaji wote wa barabara kuwa na busara pamoja na kuhakikisha kwamba, wanaheshimu na kuzingatia sheria za usalama barabarani, kwani hapa kuna maisha ya watu wengi ambayo yanaweza kuhatarishwa kutokana na uzembe barabarani.

Fadhila ya busara ni muhimu sana katika mchakato wa kulinda na kudumisha maisha ya binadamu sanjari na kusimama kidete kulinda mafao na ustawi wa wengi. Maaskofu wanakumbusha kwamba, Kanisa linaendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka mia tano tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila, aliyefanya hija ya maisha ya kiroho, akajikita katika furaha ya kweli, maisha ya sala, udugu pamoja na kuhakikisha kwamba, anatumia vyema muda wake kwa ajili ya jirani zake.

Maaskofu wa Hispania wanaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapokuwa safarini, kujenga utamaduni wa kuzungumza na wenzi wao wa safari, marafiki, ndugu na jamaa, ili kuwa na mazingira ya furaha, amani na utulivu wa ndani. Wanapokuwa barabarani wajenge pia mazingira ya sala, hapa si kwamba, wasafiri wanatakiwa kugeuza vyombo vyao vya usafiri kuwa ni Makanisa madogo, bali kujenga mazingira ambazo wasafiri wanaweza kuonja kweli uwepo wa Mungu; kwa kusali kabla na baada ya kuwasili; kwa kusikiliza: Sala, Neno la Mungu au nyimbo za dini.

Maaskofu wanawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wawapo safarini wanajenga na kudumisha umoja na udugu, pale inapowezekana watoe msaada kwa wanaohitaji pamoja na kuguswa na mahangaiko ya wasafiri wengine wanapokuwa katika shida. Wasafiri wawe watulivu wawapo njiani na kamwe wasiwe ni watu wa haraka kwani haraka haraka inaweza kuwafikisha mahali pabaya wasipopatamani. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 22 % za ajali barabarani ni matokeo ya mwendo kasi, changamoto ya kujenga busara na uvumilivu watu wanapotumia vyombo vya usafiri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.