2015-07-05 10:49:00

Ujumbe kwa Papa Francisko akiwa njiani kuelekea Amerika ya Kusini!


Rais Sergio Mattarella wa Italia amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa matashi mema wakati wa hija yake ya kitume Amerika ya Kusini kuanzia tarehe 5 hadi 13 Julai 2015. Anasema, Italia na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, inaiangalia hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Equador, Bolivia na Paraguay kwa imani na matumaini makubwa. Nchi hizi za Amerika ya Kusini, kila moja ina utambulisho na hitaji lake maalum.

Ni nchi ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto kubwa ya maendeleo katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Rais Mattarella anasema kwamba, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko utasaidia kuimarisha imani kwa Kanda hii kwa siku za usoni, eneo ambalo Italia na Jumuiya ya Ulaya inaliangalia kwa umakini mkubwa. Ni fursa pia ya kuwaimarisha wale wote wanaopambana kufa na kupona dhidi ya umaskini, hali mbaya ya uchumi na kijamii ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.