2015-07-05 11:47:00

Papa Francisko aondoka kuelekea Amerika ya Kusini


Baba Mtakatifu Francisko ameianza safari yake kuelekea Amerika ya Kusini Jumapili tarehe 5 Julai na anatarajiwa kuikamilisha hapo tarehe 13 Julai 2015 atakaporejea tena mjini Vatican. Kabla ya safari hii, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililoko mjini Roma na kuweka shada la maua lililopambwa kwa rangi ya bendera za nchi tatu zinazotembelewa na Baba Mtakatifu kwa wakati huu yaani, Equador, Bolivia na Paraguay mbele ya Sanamu ya Bikira Maria.

Baba Mtakatifu amesali kwa kitambo cha dakika ishirini na baadaye kurejea tena Vatican. Haya yameelezwa na Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican. Huu ni utamaduni wa Baba Mtakatifu kwenda kusali kabla na baada ya kurejea kutoka katika hija zake za kichungaji mbele ya Sanamu ya Bikira Maria, afya ya Warumi, iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu.  

Jumapili asubuhi, majira ya 2: 50, Baba Mtakatifu Francisko na msafara wake waliwasili kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Leonardo da Vinci. Akasalimiana na kuagana na viongozi wa Kanisa pamoja na Serikali ya Italia. Kama kawaida, Baba Mtakatifu alibeba Mkoba wake na kuingia kwenye ndege, tayari kuelekea Amerika ya Kusini. Safari kutoka Roma hadi Equador ni mwendo wa masaa 13. Akiwa njiani kuelekea Equador, Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za matashi mema kwa wakuu wa nchi ambazo amepita juu ya anga zake, yaani: Italia Hispania, Ureno, Venezuela na Colombia.

Kwa wananchi wa Italia, Baba Mtakatifu amemwambia Rais Sergio Mattarella kwamba, hija yake Amerika ya Kusini inapania kuwapelekea ujumbe wa matumaini pamoja na kuunga mkono juhudi za maisha na utume wa Kanisa mahalia huko Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko anawatakia wananchi wa Hispania: matumaini, furaha na utulivu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.