2015-07-05 09:52:00

Ni wakati wa kujikita katika mchakato wa upatanisho na umoja wa kitaifa!


Askofu mkuu Sergio Gualberti Calandrina wa Jimbo kuu la Santa Cruz de la Sierra, Bolivia anasema, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 10 Julai 2015 ni kielelezo cha neema, huruma na upendo wa Mungu kwa watu wake. Baba Mtakatifu Francisko ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ingawa idadi ya maskini inaendelea kupungua nchini Bolivia, lakini bado kuna idadi kubwa ya wananchi ambao hawana uhakika wa kupata mahitaji msingi katika maisha yao, hawa ni watu wanaoogelea katika umaskini.

Baba Mtakatifu akiwa nchini Bolivia atakutana na hali ya kinzani na migawanyiko iliyokuwa inatawala katika akili na mioyo ya watu, kiasi hata cha kuacha madonda ya kudumu katika masuala ya kisiasa na kijamii; mambo ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma; uchu wa mali na madaraka pamoja na kutozingatia kanuni maadili na utu wema. Hapa kuna haja kwa wananchi kuendeleza kanuni maadili, majadiliano, maridhiano na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko ni mjumbe wa huruma na upendo wa Mungu, atakayesaidia kuganga na kuponya madonda ya utengano, tayari kuanza mchakato wa upatanisho na umoja wa kitaifa, kwa kuzingatia ukweli, uwazi, ustawi na mafao ya wananchi wa Bolivia katika ujumla wao. Ni muda muafaka wa kuthamini tamaduni za wazawa kwa kutambua kwamba, huu ni utajiri mkubwa katika maisha ya wananchi wote wa Bolivia.

Wananchi wa Bolivia wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, kuwaonesha kuwa kweli ni sauti ya kinabii kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni kiongozi anayeonesha mfano bora wa kuigwa katika unyenyekevu wake, kiasi cha kuwa kweli ni Mchungaji mwema; mambo ambayo yanawasaidia waamini kuimarika katika imani yao.

Kanisa linaendelea kujipyaisha kwa kuzingatia changamoto zilizotolewa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini katika Waraka wake wa kichungaji unaojulikana kama “Aparecida” unaokazia ari na moyo wa kimissionari, majiundo makini kwa waamini walei; Uinjilishaji, maisha ya sala na huduma kwa maskini.

Vijana wengi wanataka kuonana na kusalimiana na Baba Mtakatifu Francisko, kwani ndani mwake, wanamwona kama Baba mwema na rafiki anayejitaabisha kwenda kuwasalimia na kuwaimarisha katika misingi ya imani, matumaini na mapendo. Hija hii itasaidia kuimarisha maisha na utume wa Kanisa nchini Bolivia. Ni wakati wa kutandaza msingi wa kweli na haki; upendo na mshikamano wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.