2015-07-05 08:29:00

Jubilei ya miaka 200 ya C.PP.S: fursa ya kutangaza huruma na upendo wa Mungu


Padre Dietrich Pendawazima, Makamu mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Consolata, IMC akishiriki katika Jubilei ya miaka 200 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. anakaza kusema ni haki kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake, kwa kumtuma Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo kuja hapa duniani, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.

Katika kipindi cha miaka 200 ya maisha na utume wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, watu wengi wamemtambua Yesu na kumweka kuwa ni kiini cha maisha na vipaumbele vyao, kwa njia ya huduma ya kimissionari inayotolewa na Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Shirika lililoanzishwa na Mtakatifu Gaspari del Bufalo. Yesu Kristo anaendelea kuwaimarisha watu wake katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili waweze kutambua na kuonja huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Damu yake Azizi, ili hatimaye, kujikita katika misingi ya haki na amani.

Padre Dietrich Pendawazima katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema kwamba, Wamissionari wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, upatanisho, haki na amani. Hii inatokana na ukweli kwamba, Yesu alikuja hapa duniani ili kuwakirimia watu utimilifu wa maisha na kwamba, kwa njia ya Damu yake, kielelezo cha upatanisho kati ya Mungu na wanadamu, basi, hii iwe ni chachu ya binadamu kupatana na kupendana.

Padre Pendawazima anakaza kusema, Yesu anaendelea kuwaita watu wengi ili kushiriki katika maisha na utume wa kimissionari, ili kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya Furaha na Matumaini, Amani na Upendo. Damu Azizi ya Kristo iwe ni alama ya maisha mapya yanayoambata Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; iwe ni alama ya ukombozi na upatanisho dhidi ya chuki, uhasama na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Kimsingi, Damu Azizi ya Yesu iwe ni chemchemi ya neema na baraka; kiini cha upendo, haki na amani duniani. Jubilei ya miaka 200 ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu ni kielelezo makini cha upendo na huruma ya Mungu kwa watu wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.