2015-07-05 14:43:00

Iweni na huruma kama Baba Yenu wa Mbinguni!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, tunakusalimu Tumsifu Yesu Kristo. Kukukumbusha tu mpendwa msikilizaji, kwa wakati huu tunauchambua Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko ujulikanao kwa jina la Misericordiae vultus yaani uso wa huruma, maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Tunakazia maarifa: Jubilei hiyo itazinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Kanisa kuu lla Mtakatifu Petro, mjini Vatican hapo tarehe 8 Desemba 2015 katika Sherehe ya kukingiwa dhambi ya asili Mama yetu Bikira Maria, na itahitimishwa katika Sherehe ya Kristo Mfalme hapo 2016.

Tunasema tena Lengo letu: Tuufahamu vema ujumbe na mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko katika Mwaka huo Mtakatifu wa Jubilei. Ujumbe anauotoa  kwetu  kwa kifupi ni huu: Kutokana na hali  ngumu ya familia ya mwanadamu tuliyo nayo kwa wakati huu; dunia inahitaji huruma ya Mungu. Ni huruma ya Mungu tu ndiyo itakayotuionua na kutuokoa kutoka katika maangamizi ya kila sampuli tunayoendelea kuyashuhudia na kwamba Kanisa ndilo chombo haswa cha huruma ya Mungu, na hivyo kila mwamini ni mjumbe wa huruma ya Mungu. Na mwaliko anaotupatia ni huu: Kanisa lirudi kwenye misingi, lihubiri na kuishuhudia huruma ya Mungu, na sisi sote kila mmoja wetu ajibidishe kuimwilisha huruma ya Mungu katika upendo.

Baba Mtakatifu ndani ya “Misericordiae vultus” anaendelea kusema, “tunataka kuuishi mwaka huu wa jubilee katika mwanga wa maneno haya ‘huruma kama Baba’. Mwinjili anatukumbusha juu ya maneno ya Yesu aliyesema “Iweni na huruma kama vile Baba yenu wa mbinguni alivyo na huruma” (Lk. 6:36). Huo ni mpango wa maisha, wenye wajibu mkubwa sana lakini mpango huo umejaa furaha na amani. Amrii hii ya Yesu inawaelekea wote ambao wapo tayari kuisikiliza sauti yake (rej. Lk. 6:27).

Uzito na umaana wa huruma ya Mungu, umedhihirishwa katika maandiko matakatifu. Ili kuweza kuwa na huruma, ni lazima hivyo kwanza kabisa tujifunze kusikiliza neno la Mungu. Hilo lamaanisha kwamba, tunapaswa kuvumbua thamani ya unyamavu ili kuweza kutafakari Neno linalokuja kwetu. Ni kwa namna hiyo itawezekana  kutafakari Huruma ya Mungu na kuifanya kuwa ndiyo mtindo wa Maisha yetu.

Pamoja na nalo, Baba Mtakatifu pia anazungumzia suala la Hija katika mwaka huo Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Anasema Hija inawakilisha safari yetu nzima ya maisha. Maisha  yetu yenyewe ni  Hija, na mwanadamu ni msafiri na mhaji anayetembea barabarani, akielekea anakotamani kufika. Vivyo hivyo, kila mmoja anapaswa kufanya hija kwa kufika katika Lango Takatifu Roma, au katika sehemu nyingine kokote duniani. Hija hiyo itakuwa ishara kwamba, huruma pia ni lengo ambalo inapaswa kufikiwa na linahitaji kujituma na kujisadaka.

Baba Mtakatifu anatutakia wongofu wa ndani kwa kila mmoja wetu, anasema “hija hiyo iwe kichocheo cha wongofu, kwa kupita Lango Takatifu, tutaonja nguvu ya kuikumbatia huruma ya Mungu na kujibidisha sisi wenyewe kuwa na huruma kwa wengine, kama vile Baba alivyo na huruma kwetu sisi. Bwana Yesu anatuonesha hatua za hija ili kufikia lengo letu: “Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa, msiwalaumu wengine nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine nanyi mtasamehewa. Wapeni wengine wanavyohitaj, nanyi mtapewa; kipimo kizuri cha kusukwasukwa na kusindiliwa hata kumwagika, ndicho mtakachopimiwa” (Lk: 6:37-38).

Bwana anatualika zaidi ya yote tusihukumu na wala tusilaumu. Kama yoyote anataka kuizuia hukumu ya Mungu, basi asijifanye mhukumu wa wengine.  Daima wanadamu wanapohukumu, hutazama sura, wakati Baba yetu wa Mbinguni, hutazama katika kilindi kabisa cha roho zetu. Ni mara ngapi maneno yetu yanadhuru na kuangamiza kabisa, hasa pale yanaposindikizwa kwa tabia za wivu na kijicho? Tunapoongea  vibaya dhini ya wengine, tunawaweka katika mwanga mbaya, na tunawajengea jina baya mbele ya jamii, na tunawafanya kuwa katuni la masengenyo na dharau.

Badala yake, Baba Mtakatifu anasema, “kujizuia na tabia ya kuhukumu-hukumu na kulaumu katika maana chanya inamaanisha kujua namna ya kuona na kupokea jema ndani ya kila mtu, na kumkinga na maumivu na masononeko yanayoweza kutokea kwa sababu ya hukumu zetu na madhanio yetu, na kujifanya kujua kila kitu kuhusu mtu huyo”. Lakini hilo tu halitoshi kuonesha huruma. Kristo anatuagiza pia kusamehe na kutoa. Tunaalikwa kuwa vyombo vya huruma kwa sababu ni sisi kwanza ndiyo tuliyopokea huruma kutoka kwa Mungu. Tunaalikwa kuwa wakarimu kwa wengine, tukijua kwamba, Mungu anatumiminia wingi wa wema wake kwa ukarimu mkuu.

Baba Mtakatifu anasema ”Iweni na huruma” ni kauli mbiu ya Mwaka  Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ni katika huruma, tunatambua jinsi gani ambavyo Mungu ametupenda sisi. Anajitoa kwetu kikamilifu kabisa, tena bure, pasipo kuomba kurudishiwa chochote. Anatuelekezea msaada kila  tunapomwita. Tazama ilivyo vizuri pale ambapo Kanisa huanza sala zake za kila siku kwa maneno “Ee Mungu uje kunisaidia. Ee Bwana ujihimize kunisaidia” (Zab 70:2). Huu msaada tunaouomba, tayari ni hatua ya kwanza ya Mungu ya kutuelekezea huruma yake. Anakuja kutusaidia katika madhaifu yetu. Na msaada wake upo katika kutusaidia sisi kukubali uwepo wake na ukaribu wake kwetu sisi. Kila siku tukiguswa kwa huruma yake, tunaweza pia kuwa na huruma kwa watu wengine.

Asante kwa kuisikiliza Radio Vatican. Ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB, nikikutakia usikilizaji mwema wa vipindi vyetu.








All the contents on this site are copyrighted ©.