2015-07-04 10:15:00

Someni waraka wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira kwa moyo mnyofu!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, hivi karibuni wakati akiwasilisha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si” yaani “Sifa kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” kwa wajumbe wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF anasema, Waraka  huu unapaswa kusomwa kwa jicho la mtoto mdogo, kwani lugha inayotumika ni ile lugha ya kawaida kabisa.

Baba Mtakatifu anazungumzia juu ya ustawi na maendeleo ya mwanadamu kwa nyakati hizi na kwa siku zijazo, kwa kutambua kwamba, dunia ni nyumba ya wote, inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira, tayari yanaonesha athari zake kwa kizazi cha sasa na kile kijacho. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya kimataifa kutambua athari zinazotokana na uharibifu wa mazingira katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu, tayari kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha mazingira bora.

Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko ni ujumbe wa matumaini unaopaswa kumwilishwa katika sera, mikakati na vipaumbele vya Jumuiya ya Kimataifa, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Hii inatokana na ukweli kwamba, binadamu na mazingira ni sawa na chanda na pete; ni mambo ambayo kamwe hayawezi kutenganishwa. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu mwenyewe. Hapa utamaduni na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.

Pili anasema Kardinali Turkson ni jeuri ya binadamu kudhani kwamba, anaweza kutatua matatizo na changamoto zote za maisha kwa kujikita katika teknolojia na uchumi, bila kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, kanuni maadili na utu wema. Hapa kuna haja ya kutambua kwamba, hata maisha ya kiroho yana mchango mkubwa katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujiuliza, swali la msingi, Je, ni urithi gani wanataka kuacha hapa duniani kwa ajili ya vijana wa kizazi kijacho?

Kuna mwingiliano mkubwa kati ya maisha ya binadamu na mazingira, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mazingira ni nyumba ya yote inayofumbata masuala ya maendeleo endelevu, yanayopasa kugusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Uharibifu wa mazingira utawafanya watoto baadaye kushindwa kuona baadhi ya mambo. Watu wataendelea kuhama na kuzikimbia nchi zao, ili kutafuta unafuu na ubora wa maisha. Kutokana na umaskini, uchu wa mali na madaraka, biashara haramu ya binadamu itaendelea kushamiri na wazee na wagonjwa kutelekezwa pasi na msaada.

Kardinali Turkson anakaza kusema, ikiwa kama binadamu hatachukua hatua makini, ataendelea kusababisha madhara makubwa katika maisha yake, kwani maisha na mazingira ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, binadamu ataweza kufanya mabadiliko makubwa katika maisha, ili kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi.

Hii ni changamoto inayojikita katika unyenyekevu, kiasi na sadaka, ili kushirikishana rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, kwa kutambua kwamba, kazi ya uumbaji ni kielelezo cha utukufu wa Mungu na kwa ajili ya mafao na ustawi wa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.