2015-07-04 11:01:00

Papa mstaafu Benedikto XVI atunukiwa shahada ya udaktari wa heshima!


Chuo kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Yohane Paulo II kwa kushirikiana na Taasisi ya Muziki kutoka Cracovia, Poland, Jumamosi, tarehe 4 Julai 2015 wamemtunuku Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI Shahada ya Udaktari wa heshima “Doctoratus honoris causa” kwa kutambua mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa.

Tukio hili limefanyika kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo, iliyoko nje kidogo ya mji wa Roma. Shahada hii ya heshima imetolewa kwa Papa mstaafu na Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, Poland ambaye pia ni mkuu wa Chuo kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Yohane Paulo II kilichoko nchini Poland.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kwa namna ya pekee, anawashukuru na kuwapongeza wananchi wa Poland waliomtunukia heshima hii ya hali ya juu na kwamba, inamkumbusha mahusiano ya karibu aliyo nayo na Poland, lakini kwa namna ya pekee na Jimbo kuu la Cracovia, mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na kutambua umuhimu wa muziki mtakatifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, kielelezo cha imani.

Muziki mtakatifu mintarafu mageuzi yaliyofanywa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni kielelezo cha furaha ya imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika masuala ya muziki mtakatifu ndani ya Kanisa, mambo ambayo yamechangiwa pia na Jumuiya za Seminari. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Vatican wanakaza kusema, hazina ya Mapokeo ya muziki mtakatifu ihifadhiwe na kukuzwa kwa uangalifu sana, kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI anasema kwamba, muziki unapata chimbuko lake katika upendo; nyakati za majonzi na uchungu na pale mtu anapokutana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yake na kugusa kwa namna ya pekee fumbo la uhai na kifo; mambo yanayojieleza katika Zaburi. Kuna utajiri mkubwa wa muziki mtakatifu ulioibuliwa ndani ya Kanisa Katoliki, tofauti kabisa na tamaduni nyingine za dunia. Muziki unapaswa kuwa ni chemchemi inayobubujika kutoka katika undani wa mtu anayekutana na Muumba wake; Mungu anayejifunua kwa njia ya Yesu Kristo.

Muziki ni kielelezo cha ukweli wa Kikristo, kwa kutambua ukweli, ili kukutana na Mwenyezi Mungu, Muumba wa vitu vyote, na hivyo Muziki mtakatifu  ni kielelezo cha ukweli na imani ya Kikristo, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika Liturujia ya Kanisa, Fumbo la imani ya Kanisa.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika maadhimisho ya Liturujia katika nchi mbali mbali wakati wa maisha na utume wake, yanabeba utajiri mkubwa wa Kiliturujia hata kutoka katika mataifa haya. Pale ambapo waamini wanapata fursa ya kukutana na Mwenyezi Mungu anayejifunua kwa njia ya Yesu Kristo, hapo kweli wanaweza kutambua na kuonja uzuri wa muziki mtakatifu.

Taasisi hizi mbili anasema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI zilizomtunukia Shahada ya heshima katika muziki mtakatifu, ni mashuhuda wa zawadi ya muziki unaopata chimbuko lake katika imani ya Kikristo, kikolezo muhimu sana katika mchakato wa kumwilisha imani. Kwa namna ya pekee, anawashukuru kwa heshima waliyompatia pamoja na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoendelea kuitenda kwa ajili ya kupamba huduma na uzuri wa imani.

Kwa upande wake, Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kwa kukubali kupokea heshima hii kama kielelezo cha utambuzi wa mchango mkubwa uliofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wa Kanisa. Papa mstaafu Benedikto XVI, amekuwa ni msaidizi wa karibu sana wa Mtakatifu Yohane Paulo II na kwamba, jina lake litaendelea kukumbukwa katika historia ya Chuo kikuu cha Kipapa cha Yohane Paulo II, Cracovia, Poland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.