2015-07-04 09:59:00

Jengeni umoja katika utofauti, kwa kudumisha Uekumene wa damu, sala na huduma


Bahari ya wanachama wa Uamsho wa Roho Mtakatifu ilifurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa jioni tarehe 3 Julai 2015, ili kukutana na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko. Lengo lilikuwa ni kuendelea kuombea umoja wa Kanisa, kama moja ya changamoto kubwa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Baba Mtakatifu katika sala yake amemwomba Roho Mtakatifu alijalie Kanisa umoja katika tofauti zinazojionesha kwa karama na huduma.

Yesu aliwafundisha wafuasi wake kuwa na umoja, lakini kwa bahati mbaya, kutokana na ubinadamu wao na historia, wakajikuta wakiwa wamegawanyika. Baba Mtakatifu anamwomba Roho Mtakatifu awawezeshe Wakristo kuambata mchakato wa umoja katika utofauti uliopatishwa na kwamba, umoja wa Wakristo unawezekana tu, ikiwa kama Yesu Kristo ateweka neema yake!

Baba Mtakatifu Francisko anatambua mchango mkubwa uliotolewa na Mwenyeheri Paulo VI kwa kukubali na kuidhinisha Chama cha Uamsho wa Roho Mtakatifu kama kielelezo cha Pentekoste mpya ndani ya Kanisa, baada ya Mama Veronica O’Brien kuwaomba viongozi wa Kanisa kupembua kwa kina na mapana maisha na utume wa chama hiki kipya. Papa Paulo VI kunako mwaka 1975 akawashukuru wanachama kwa kukiweka chama hiki katika moyo wa Kanisa.

Ni matumaini ya viongozi wa Kanisa kwamba, mwamko ulioletwa na chama hiki utasaidia watu kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Uamsho wa Roho Mtakatifu ni kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hizi ni neema za Roho Mtakatifu kwa Kanisa zima, neema inayopyaishwa kama mwendelezo wa dhamana ya ubatizo na matokeo yake, ndani ya Kanisa kumeibuka: Jumuiya, vyama vya Uinjilishaji, Mashirika ya kitawa pamoja na Jumuiya za Kiekumene zinazojisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini. Haya ni Mashirika ambayo yanatambuliwa na Vatican kutokana na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake, amekazia umuhimu wa Kanisa kuambata umoja katika tofauti, ukweli unaojionesha katika maisha na utume wa Kanisa; changamoto na mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kuambata na neema na baraka zinazoletwa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Hapa viongozi wa Chama cha Uamsho wa Roho Mtakatifu wanapaswa kukumbuka kwamba, wameteuliwa kwa ajili ya huduma na wasipokuwa makini wanaweza kujaribiwa na mwovu shetani kwa njia ya: kiburi,madaraka, ufahari na fedha. Roho Mtakatifu ndiye nguzo kuu ya Kanisa; mambo mengine yanaweza kupita na kutoweka kabisa.

Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, uongozi ni huduma na dhamana ambayo inapaswa kuwa na kiwango chake cha muda, hakuna kiongozi anayeweza kutala daima. Viongozi waoneshe ujasiri wa kung’atuka madarakani, ili kutoa nafasi kwa wanachama wengine waweze kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa. Viongozi waendelee kujifunza kutoka kwa Kristo ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.

Viongozi waliopokea karama za Roho Mtakatifu wana dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanalinda na kuendeleza karama hizi ili ziweze kusonga mbele kadiri ya mapenzi ya Mungu. Wanachama wa vyama mbali mbali vya kitume wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wao ndani ya Kanisa; kwa kushiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu.

Baba Mtakatifu anawataka wanachama wa vyama vya kitume kuhakikisha kwamba, wanajenga moyo wa uaminifu na ushirikiano na Maaskofu mahalia; daima wakitafuta umoja, mafao na ustawi wa Kanisa. Waendeleze Uekumene wa maisha ya kiroho na katika sala, kwa kutambua kwamba, wakristo wote wamepokea neema ya Ubatizo kutoka kwa Roho Mtakatifu. Waamini wajikite katika Uekumene wa kazi na huduma ya mapendo; Uekumene wa tafakari ya Neno la Mungu.

Mchakato wa majadiliano ya kiekumene unajikita kwa namna ya pekee katika maisha ya sala, kwa kutambua kwamba, leo hii ndani ya Kanisa kuna Uekumene wa damu, unaotokana na madhulumu, nyanyaso na mauaji yanayofanywa dhidi ya Wakristo. Umoja wa Wakristo ni matunda ya Roho Mtakatifu. Majadiliano ya kiekumene yajikite katika ushuhuda wa maisha na hata katika kifo. Wakristo wanaunganishwa pamoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Sakramenti ya Ubatizo na maisha ya sala.

Uekumene wa damu ni ushuhuda unaotolewa na Wakristo kwa pamoja licha ya tofauti zao kama alivyofanya Mwenyeheri Paulo VI kwa kuwatangaza Mashahidi wa Uganda, walioyamimina maisha yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni changamoto kwa Kanisa kuunganika katika sala, ili kuwaombea mashuhuda wa imani ya Kikristo, pamoja na kuhakikisha kwamba, Makanisa yanawaenzi mashuhuda hawa wa imani kama mfano bora wa kuigwa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Uamsho wa Roho Mtakatifu ni neema ya Kipentekoste kwa Kanisa zima, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kidugu; upendo katika sala na huduma. Baba Mtakatifu anawaalika wanachama wa Uamsho wa Roho Mtakatifu kukutana ili kusali pamoja panapo majaliwa kunako mwaka 2017, ili kuadhimisha Jubilei ya Dhahabu tangu kuanzishwa kwa Chama cha Uamsho wa Roho Mtakatifu, ili kumwimbia Roho Mtakatifu utenzi wa shukrani, kwa wema na ukarimu wake aliolitendea Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.