2015-07-04 12:06:00

Amerika ya Kusini ni maabara ya kijamii; uwanja wa majadiliano na demokrasia


Askofu mkuu Paul Richard  Gallagher, Katibu mkuu wa mambo za nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa katika mahojiano maalum na gazeti la Avvenire, linalomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anakaza kusema, Amerika ya Kusini ni eneo ambalo kwa miaka mingi limependa kujikita katika mchakato wa maendeleo yake kwa kuzingatia vipaumbele na mahitaji ya watu wake.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Equador, Bolivia na Paraguay inajikita katika masuala msingi ya kijamii, maendeleo endelevu, utunzaji bora wa mazingira pamoja na ushirikiano wa kimataifa ambao kwa namna ya pekee unaendelea kuonesha kati ya Cuba na Marekani, baada ya kutunishiana misuli kwa muda wa zaidi ya miaka hamsini, sasa ni wadau wanaoweza kukaa na kuzungumza pamoja kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wao. Huu ndio utamaduni na utandawazi wa watu kukutana na kujadiliana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.

Baba Mtakatifu katika nchi hizi tatu anataka kukazia mtindo wa maendeleo unaoambata maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili; usawa, haki na amani; msamaha, upendo na upatanisho. Amerika ya Kusini ni jukwaa la maabara ya maendeleo ya kijamii, demokrasia na ushirikishwaji wa watu wengi zaidi, hususan wangonge na maskini ambao wanaendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Amerika ya Kusini ni eneo linalotaka kukuza na kudumisha maendeleo kadiri utambulisho wake na wala si kupokea kila kitu kinachotoka nje kwa majaribio kama “kichwa cha mwendawazimu”.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko inalenga kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo, tayari kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu. Kumbe, ni wajibu wa Familia ya Mungu katika eneo hili kujikita katika mchakato wa kutafuta, kujenga na  kudumisha misingi ya haki, amani, msamaha, upatanisho, maendeleo na mafao ya wengi. Viongozi wakuu wa nchi waliomtembelea Baba Mtakatifu Francisko wamejadili na kupembua mambo msingi yanayogusa ustawi na maendeleo ya watu wao huko Amerika ya Kusini

Vatican kwa upande wake, inaendelea kukazia umuhimu wa Kanisa kupata nafasi ya kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu ya watu kiroho na kimwili kwa kuzingatia uhuru wa kuabudu kama sehemu ya haki msingi za binadamu.  Kinzani na migogoro ni sehemu ya maisha ya watu. Kuna baadhi ya wananchi wa Paraguay wanataka kutumia hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao kwa mafao yao ya kisiasa.

Lakini, Baba Mtakatifu anataka kuwa ni shuhuda wa Injili ya furaha, matumaini na mapendo kwa wagonjwa, wazee, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Paraguay kwa miaka ya hivi karibuni imepiga hatua kubwa katika ustawi na maendeleo ya wananchi wake kijamii, kumbe bado inawajibu wa kuendeleza mchakato huu kwa ajili ya mafao ya wengi. Kinzani na migogoro kati ya Serikali na baadhi ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini ni sehemu ya mchakato wa maisha unaopaswa kujikita katika majadiliano, haki, ukweli, mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.

Hii ni sehemu ya mchakato wa Unjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa ni sauti ya kinabii, wakati mwingine, linaposimama kidete kutetea mambo msingi, “linapigwa madongo” kwa kuingilia masuala ya kisiasa! Lakini anayehudumiwa ni binadamu yule yule, kiroho na kimwili. Hija ya Baba Mtakatifu katika nchi hizi, inapania kuwagusa wananchi wote wa Amerika ya Kusini, bila kusahau Venezuela ambayo bado inakabiliana na ukinzani pamoja na mpasuko wa kijamii; Cuba inayoanza ukurasa mpya kwa kuwa na ushirikiano wa kidiplomasia na Marekani.

Vatican inaendelea kufuatilia kwa karibu mchakato wa majadiliano ya: haki, amani na upatanisho huko Colombia, Mashariki ya Kati, Ukraine na sehemu mbali mbali za dunia ambako bado watu wanaendelea kuteseka kutoka na vita na ukiukwaji wa haki msingi za binadamu. Amani inaweza kupatikana kwa kujikita katika ukweli na uwazi, kwa kusitisha biashara haramu ya silaha; kwa kupinga kwa vitendo biashara haramu na matumizi ya dawa za kulevya; uchu wa mali na madaraka mambo ambayo yanaendelea kusababisha maafa na majanga makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija hii ya kitume anataka kukazia kwa mara nyingine utunzaji bora wa mazingira kama nyumba ya wote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wote. Hapa wananchi wanapaswa kubadilisha mtindo wa maisha utakaosaidia kulinda na kutunza mazingira, kwa kujikita katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu ambayo pia ni rafiki kwa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.