2015-07-03 11:05:00

Waraka wa kitume wa Papa Francisko kuhusu mazingira ni kwa mafao ya wote


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume juu ya utunzaji bora wa mazingira “Laudato si” anapenda kukazia umuhimu wa maendeleo endelevu yanayojikita katika kanuni maadili na utu wema, mwanadamu akipewa kipaumbele cha kwanza sanjari na kutafuta mafao, ustawi na maendeleo ya wengi.

Haya yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati alipokuwa anachangia mada Alhamisi, tarehe 2 Julai 2015 kwenye kampeni ya utunzaji bora wa mazingira inayoendeshwa na Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Maendeleo Kimataifa, CIDSE. Kardinali Parolin anasema, Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko juu ya utunzaji bora wa mazingira ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, lakini pia ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote.

Huu ni mchango utakaoisaidia Jumuiya ya Kimataifa kufanya maamuzi magumu wakati wa mkutano wa kimataifa juu ya mabadiliko ya tabianchi unaotarajiwa kufanyika huko Paris, Ufaransa, mwezi Desemba 2015. Kanisa linapenda pia kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika utunzaji bora wa mazingira. Wakristo kwa kushikamana kwa dhati wanaweza kusaidia kutoa majibu muafaka kwa matatizo na changamoto zinazoendelea kumwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa utunzaji bora wa mazingira anakazia umuhimu wa ushirikiano na mshikamano wa kimataifa unaojikita katika kanuni maadili, ili kudhibiti madhara yanayoendelea kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi; kwa kupambana na umaskini wa hali na kipato; ukosefu wa usawa pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kila raia anahamasishwa kuchangia katika utunzaji bora wa mazingira kwa ajili ya nyumba ya wote, kwa kutekeleza yale ambayo yako katika uwezo wake.

Kardinali Parolin anasema kwamba, Baba Mtakatifu anabainisha kwa kina na mapana mambo msingi ambayo yanapaswa kutekelezwa na wote. Hapa kila mtu anawajibika kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, kadiri ya ufafanuzi na maelezo yanayotolewa na Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa kitume, kuhusu utunzaji bora wa mazigira.

Kardinali Parolin anakiri kwamba, mkutano huu ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na wadau mbali mbali ni jukwaa la majadiliano yanayofanywa na wataalam kutoka katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Hii ni fursa makini ya kuufahamu na kuusambaza Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko juu ya utunzaji bora wa mazingira, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi cha sasa na kile kijacho na kwamba, uwepo wake kati ya wajumbe hawa ulipania kusaidia kuchangia katika mchakato mkubwa wa kusambaza Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Familia ya Mungu, sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.