2015-07-03 15:41:00

Wape wape vidonge vyao, wakimeza wakitema ni shauri yao!


“Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana!” Yohane Mbatizaji alipoulizwa na watu waliokuja kumsikiliza juu ya utambulisho wake daima aliwajibu kuwa yeye ni sauti. Kwa maneno haya, ninapenda kukukaribisha katika Kipindi cha Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya kumi na nne ya Mwaka B wa Kanisa.

Sauti au mlio wa kitu chochote hupokelewa katika hali mbili tofauti kati ya viumbe. Wanyama na viumbe vingine visivyo na utashi huisikia sauti lakini hujibu kadiri ya taratibu za kimaumbile. Mwanadamu aliyepewa akili na utashi, Yeye aliyepewa uwezo wa kuupambanua ulimwengu na kuuratibu huipokea sauti na kuipatia maana. Ndiyo maana utaona, mathalani, mmoja anaposikia mngurumo wa mashine angali amejifungia ndani akili yake itajishughulisha kuupatia maana mngurumo huo: Je, ni mngurumo wa gari, au mngurumo wa trekta au ni mngurumo wa bomu n.k.

Sauti ya unabii kwa mwanadamu nayo hutupatia maana. Mwanadamu hapaswi kuisikiliza na kuiacha tu kama vile viumbe vingine, wanyama na hayawani wanavyosikiliza, na kuiacha bali wanapaswa kuipatia maana. Maana ya sauti ya unabii inaelezewa vizuri kabisa katika maneno ya Nabii Yohane Mbatizaji: Unabii ni sauti ya Mungu inayomwalika mwanadamu kuitengeneza njia ya Bwana.

Sauti hii inatualika kujitathimini maisha yetu, kuangalia mahusiano yetu na Mungu na kurekebisha kasoro zilizopo katika mahusiano yetu na Mungu. Maisha yetu wanadamu ni safari kuelekea kwa Baba yetu. Imani yetu thabiti kwa Mungu ni njia ambayo daima inakumbana na ukinzani mkubwa na hata kupoteza kabisa hadhi yake. Nabii katika jamii analo jukumu la kumkumbusha mwanadamu yeye ni nani mbele ya Mwenyezi Mungu na kumwalika kuirekebisha njia yake ili “apate kuishi”.

Katika Dominika ya leo wazo kubwa linalojitokeza ni wajibu wetu wa kinabii kama wabatizwa katika Ulimwengu mamboleo. Somo la kwanza linamtia nguvu nabii: “Nao kwamba watasikia, au kwamba hawataki kushika, hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao”. Nabii hapaswi kukata tamaa na ukinzani au ubaridi unaokuwepo katika jamii anayoitangazia ujumbe wa Mungu. Kwa kuwa Nabii ni “sauti ya Mungu” anapaswa kuipaza sauti yake kwa wote bila kuchoka. Mwanadamu aliyejeruhiwa na dhambi amejazwa ukaidi lakini bado ndani mwake kuna dhamiri, sauti ya Mungu inayozungumza naye, nguvu ya ndani inayomgutusha katika maovu yake. Pamoja na kiburi chake lazima atafika mahali na kutambua kuwa “Nabii amekuwepo kati yao”.

Somo la Injili linaweka mbele yetu jamii halisi ya Nazareti ambayo inakinzana bayana na Sauti ya kinabii. “Wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu amepata wapi haya?” Hii ni jamii halisi alimoishi na kukulia Bwana wetu Yesu Kristo. Ni jamii ambayo inapokea sauti ya kinabii kwa kuiambatanisha na hadhi na nafasi ya mtoa sauti na si kuzama katika maana na ujumbe wa sauti anayoitoa. Hapa mwanadamu anaingia katika kishawishi cha kutoisikiliza sauti anayoisikia, kuipatia maana yake na pia kuitumia katika kujiimarisha kiroho hata na kimwili na kuishia kumchambua kinagaubaga mtoa sauti, ubini wake, ndugu zake na hata elimu yake, ndiyo maana haya kwenye Injili wanataja, “si mtoto wa Mariamu?”

Mara nyingi tunasikia maneno akama haya: “Yeye ni nani hata atuelekeze hivyo?” “Elimu yake ni kiwango gani?” “Ni upi uwezo wake kiuchumi au kiushawishi katika jamii yetu?” na mengineyo mengi.

“Yesu alistaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao”. Tunu ya imani inadokezwa hapa kama njia muhimu sana ya kuoiona na kuitambua sauti ya Mungu inayotujia kwetu kupitia wajumbe wake mbalimbali. Imani kwa Mungu inaambatana pia na kumsadiki yule anayetupatia ujumbe wa Neno la Mungu na kuupokea ujumbe huo kama Neno la Mungu. Dunia yetu leo hii inaweza isitofautiane sana na jamii hii ya Nazareti tunayoisikia katika somo la Injili. Nafasi ya Mungu katika mioyo ya wanadamu inazidi kufifia siku hata siku. Wanadamu wanazidi kujaza mambo ya ulimwengu katika mioyo yao: mali zao, akili zao, marafiki zao, nguvu zao na hata ushawishi wao. Mwanadamu amempora Mungu nafasi yake ya kuwa yote katika yote na matokeo yake ni ugumu hata katika kusikiliza na kutilia maanani sauti na ujumbe wake anaotupatia kupita wajumbe wake manabii.

Changamoto kama hizi huweka ugumu hata kwa Nabii husika ambaye wakati mwingine huingia katika kishawishi cha kukata tamaa. Mtume Paulo anatuonya katika somo la pili, sisi kama manabii daima kutegemea Mungu. Ujumbe unaofunuliwa ndani mwetu, ujumbe tunaoubeba ndani mwetu na tunaotaka kuueneza ni kazi ya Mungu. Yeye ndiye kwa nafasi ya kwanza anajitetea na kuufanya uweze kuenea duniani kote na kwa watu wote. “Makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili”

Mtume Paulo alipokea mafunuo ya kimbingu lakini bado aliambatana na udhaifu wake ambao kwa namna fulani ungepelekea kumkatisha tamaa ya kuyaeneza makuu hayo ya Mungu kwa watu. Huu ni udhihirisho kuwa Mungu anatenda pamoja na mwanadamu kama chombo cha kueneza ujumbe wake bila kujali hali yake na ustadi wake. Pia nabii anahaswa kwamba, katika kutekeleza wajibu huu wa kinabii “neema yangu inakutosha”. Mungu mwenyewe anajitosheleza kuifanya sauti yake isikike kwa watu wote.

Kitu cha muhimu kwetu ni utayari tu wa kulipeleka Neno lake kwa mataifa. Nabii Yeremia aliambiwa “Usiseme mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake. Usiogope kwa sababu ya hao, maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe”. Nabii Isaya alijiona asiyestahili aliposema: “Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mwenye midomo michafu”.

Jamii yetu ya Leo bado inahitaji sana kuisikia sauti hii ya kinabii. Ni dhahiri kwamba ukahidi ule wa somo la kwanza unaonekana wazi kabisa katika jamii ya wanadamu. Kwa upande mwingine maamuzi mbele ya kibinadamu ya jamii ya Nazareth yanaendelea kushamiri na hata kuonekana kutuwekea kiwingu katika kueneza ujumbe wa Neno la Mungu. Sauti ya Mungu bado inaendelea kulia ndani mwetu leo hii, usiogope, wewe nenda tu katangaze Neno langu. Usiogope, ni Neno langu. Usiwe na shaka, Neema yangu iankutosha. Mimi ninakutuma wewe lakini nipo pamoja nawe. Hata kama inaonekana hawataki kukusikiliza lakini ujumbe wanaupata. Ni kana kwamba tunakumbushwa wimbo wa zamani wa kidunia uliosema: “wape wape vidonge vyao, wakiemeza ama wakitema shauri zao”.

Unabii ndani ya Kanisa ni wajibu wa kuwa mashuhuda wa imani. Katika ulimwengu wetu wa leo unaoonesha ukinzani mkubwa wa kuisikia sauti ya Mungu tunakumbushwa tena maneno ya Kristo: “Watu watawatambueni kuwa mu wanafunzi wangu, mkipendana ninyi kwa ninyi”. Umefika wakati wa kuuishi Upende wa Kristo na kuueneza kwa watu wote kwa mfano wa maisha yetu ya kindungu na upendo. Hii ndiyo sauti tunayopaswa kuipaza zaidi katika ulimwengu wa leo: “Ushuhuda wa kimaisha”. Mtakatifu Fransisko wa Asisi alikuwa daima anawaasa ndugu zake: “nendeni mkaihubiri habari njema kwa watu wote na kama itawalazimu sana tumieni maneno”. Sauti ya vitendo inagusa sana na inatoa maana katika kile unachokisadiki.

Leo tunaalikwa kutokata tamaa. Upo msemo unaokwenda hivi: “unaporusha jiwe katika giza na ukasikia sauti inatoka ujue hapo ndipo jiwe hilo limegonga”. Jamii yetu ya leo hata kama inaonesha kuwa ni giza totoro tuendelee kuwa manabii, kuwa chumvi na kuwa mwanga kwa mfano wa maisha ya kikristo.

Mwanadamu hakuumbwa kama mashine, akili na utashi wake vitamfanya kufikiri na kufafanua na hatimaye kufanya maamuzi ya kusonga mbele. Tuwaombee leo wanakanisa wote; wahubiri wetu, wazazi, viongozi wa kijamii kuwa vyombo na sauti ya kuleta ujumbe wa Mungu kusudi watu wote warekebishe njia zao na kuendelea vema na safari ya maisha kuelekea kuungana na Baba yetu aliye mbinguni.

Na Padre Joseph Mosha. 








All the contents on this site are copyrighted ©.