2015-07-03 15:57:00

Ratiba elekezi ya hija ya kitume ya Papa Francisko Amerika ya Kusini


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 13 Julai 2015 anatarajiwa kufanya hija ya kitume katika nchi tatu za Amerika ya Kusini. Atatembelea Equador, Bolivia na Paraguay. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuondoka mjini Roma, tarehe 5 Julai 2015 na kuwasili jioni kwenye Uwanja wa Kimataifa wa “Mariscal Sucre” ulioko Quito, mji mkuu wa Ecuador. Hapa Baba Mtakatifu atatoa hotuba kwa wenyeji wake akiwa bado Uwanjani hapo.

Jumatatu, tarehe 6 Julai 2015 ataondoka kwa ndege kuelekea Guayaquil ili kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu mbele ya Madhabahu ya Huruma ya Mungu na baadaye jioni atarejea tena mjini Quito, ili kumtembelea Rais pamoja na kusali kidogo kwenye Kanisa kuu la Jimbo la Quito.

Jumanne, tarehe 7 Julai 2015, ratiba inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki wa Equador; baadaye ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya wanafunzi kutoka vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini humo na baadaye atazungumza na viongozi wa Serikali, kwenye Kanisa la Mtakatifu Francisko, baadaye jioni, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea Jumuiya ya Wakristo Kijijini.

Jumatano, tarehe 8 Julai 2015, Baba Mtakatifu atatembelea nyumba ya mapumziko inayoendeshwa na Shirika la Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta na baadaye atakutana na kuzungumza na Wakleri, Watawa na Majandokasisi katika Madhabahu ya kitaifa ya Bikira Maria “ El Quinche”. Baba Mtakatifu atakuwa anahitimisha hija yake ya kitume nchini Equador, tayari kuondoka kuelekea Bolivia.

Jumatano, jioni, Baba Mtakatifu atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa “El Alto” ulioko kwenye mji mkuu wa La Paz. Baada ya kukaribishwa rasmi, Baba Mtakatifu atamtembelea Rais Ikulu, atazungumza na viongozi wa Serikali na kiraia na baadaye ataondoka kwa ndege kuelekea mjini Santa Cruz de la Sierra.

Alhamisi, tarehe 9 Julai 2015, Baba Mtakatifu ataianza siku kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kristo Mfalme na baadaye jioni atakutana na Wakleri, Watawa na Majandokasisi kwenye Shule ya Don Bosco na baadaye atashiriki katika mkutano wa kimataifa wa vyama vya wanawanchi na hapo anatarajiwa kutoa hotuba.

Ijumaa, tarehe 10 Julai 2015, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea na kuhutubia kwenye Kituo cha kurekebishia tabia cha santa Cruz, kilichoko mjini Palmasola. Atakutana pia na Baraza la Maaskofu Katoliki wa Bolivia na baadaye jioni kuondoka kuelekea nchini Paraguay, ambako anatarajiwa kuwasili mchana na kupokelewa kwa heshima za kitaifa. Atapata fursa ya kumtembelea Rais wa Paraguay, Ikulu pamoja na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Wanadiplomasia walioko nchini humo.

Jumamosi, tarehe 11 Julai, 2015, Baba Mtakatifu Francisko ataianza siku kwa kutembelea Hospitali kuu ya Watoto “Ninos de Acosta nu”; baadaye ataadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Caacupè. Baadaye, atasali Masifu ya jioni na Wakleri, Watawa, Majando kasisi na wanachama wa vyama vya kitume nchini Paraguay. Ibada hii itafanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria kupalizwa mbinguni.

Jumapili, tarehe 12 Julai, 2015, Baba Mtakatifu atawatembelea na kuwasalimia wananchi wanaoishi kwenye eneo la “Banado Norte” pamoja na kuzungumza nao. Baba Mtakatifu anatarajiwa pia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye uwanja wa Nu Guazu; mchana atakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay pamoja na kupata nao chakula cha mchana.

Jioni kabla ya kufunga virago na kurejea tena mjini Vatican, Baba Mtakatifu atakutana na kungumza na vijana pembeni mwa Mto wa “Costanera”. Baadaye Baba Mtakatifu Francisko na ujumbe wake, watakuwa wanahitimisha hija kwa nchi za Amerika ya Kusini, yaani: Equador, Bolivia na Paraguay.

Kama kawaida, Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega, lakini kwa wenye haraka zao wanaweza kupata habari hizi moja kwa moja kutoka kwenye mtandao wa Radio Vatican, ili kufahamu yale yanayojiri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.