2015-07-03 09:41:00

Papa Francisko anataka kuwaimarisha ndugu zake katika imani na furaha!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Amerika ya Kusini kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 12 Julai 2015 ni hija ndefu itakayomwezesha Baba Mtakatifu kuwatangazia Watu wa Mungu Injili ya furaha, matumaini, upendo, haki na amani, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni hija inayotaka kuimarisha umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira; haki msingi za binadamu na utambulisho wa kila taifa dhidi ya mwelekeo wa sasa wa kumeza wadogo kwa kisingizio cha utandawazi.

Kardinali Parolin katika mahojiano maalum na Kituo cha televisheni cha Vatican anakaza kusema, Baba Mtakatifu anatembelea Equador, Bolivia na Paraguay. Bara la Amerika anasema Baba Mtakatifu Francisko ni eneo la matumaini ambayo yanapaswa kujikita katika mtindo wa maendeleo endelevu unaoambata maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, nchi hizi zitaendelea kukumbatia pia Mapokeo na utamaduni wa Kikristo unaojikita katika haki, usawa, upatanisho, maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia kwa kuambata pia busara na hekima za wahenga. Lengo ni kujenga na kudumisha Injili ya furaha na matumaini kwa wananchi wa Amerika ya Kusini.

Amerika ya Kusini ni Bara ambalo linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa: kitamaduni, kiuchumi na kisiasa. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, kumekuwepo na maendeleo makubwa katika mapambano dhidi ya umaskini; kuna dalili za kukua na kupanuka kwa maendeleo mijini, lakini pia kuna dalili za kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema kutokana na watu kumezwa mno na malimwengu pamoja na utandawazi usiokuwa na mashiko wala tija.

Katika kukabiliana na changamoto zote hizi, Kardinali Parolin anasema kwamba, Kanisa linajielekeza zaidi katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani katika sera na mikakati yake ya kichungaji; ari na moyo wa kimissionari; tayari kuwatangazia watu wa Mungu, Injili ya furaha inayojikita katika huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu pamoja na kuwa ujasiri wa kutoka kwenda kuwatangazia wengine furaha, imani na matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya binadamu.

Kardinali Parolin anasema, Amerika ya Kusini ni maabara ya shughuli za kisiasa, kwani hapa bado watu wanafanya majaribio ya siasa za kushirikishana na uwakilishi, ili kutoa sauti kwa wanyonge na wale ambao pengine kwa miaka mingi hawakuweza kusikilizwa kutokana na sababu mbali mbali. Hii ni demokrasia inayojikita katika tamaduni na vipaumbele vya wananchi katika eneo hili, sanjari na kukazia uhuru na haki msingi za binadamu.

Kanisa Katoliki katika nchi zote  hizi zinazotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko linaendelea kuwa ni sauti ya kinabii na mtetezi wa wanyonge; kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema, ili kusimama kidete: kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayojikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kunako mwaka 2014, Baraza la Maaskofu Katoliki Equador liliandika barua ya kichungaji kuonesha dhamana na nafasi ya Kanisa katika maisha na ustawi wa wananchi wa Equador.

Baraza la Maaskofu Katoliki Equador liliwataka waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha ya utume wa Kanisa kwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Lengo ni kudumisha utu na heshima ya binadamu; maendeleo na mafao ya wengi sanjari na haki msingi za binadamu, kwa kuendelea kuwa ni sauti ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Nchini Bolivia, Rais Evo Morales anaendelea kusimamia haki msingi za binadamu, utu na heshima ya maskini; utunzaji bora wa mazingira; mambo ambayo kimsingi anasema Kardinali Parolin yanapembuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Huu ni waraka unaokazia kwa namna ya pekee: haki msingi za binadamu; upendo na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; haki na amani; mapambano dhidi ya baa la umaskini na njaa na kwamba, rasilimali ya dunia ni kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay kwa upande wake, linakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko anawatembelea kama hujaji anayekwenda kuimarisha mchakato wa Uinjilishaji ambao umekuwa ukifanyiwa kazi na Maaskofu kwa muda wa miaka mitatu sasa. Baba Mtakatifu anataka kuimarisha Injili ya Familia, ili kweli waamini na watu wote wenye mapenzi mema waweze kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Hapa Kanisa linaendelea kusimama kidete kutangaza Injili uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaifa inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Familia zinakabiliana na changamoto kubwa hasa kutokana ukosefu wa fursa za ajira, ukata, uwepo wa familia tenge; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Baba Mtakatifu anataka kuonesha uwepo wake wa karibu na wote wanaoteseka, ili kuwatia moyo kusonga mbele kwa kujikita katika Injili ya furaha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.