2015-07-03 11:54:00

Jengeni mshikamano na huduma ya upendo kwa wahamiaji na wakimbizi!


Ukarimu kwa wahamiaji ni changamoto ya malezi; ndiyo kauli mbiu iliyoongoza mkutano wa Maaskofu na wakurugenzi wa idara za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, uliokuwa unafanyika Vilnius, Lithuania kuanzia tarehe 30 Juni hadi tarehe 2 Julai 2015. Kutokana na changamoto za utandawazi zinaoendelea kujitokeza kila siku, kuna haja kwa Jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa malezi ili kujenga utandawazi wa mshikamano na upendo.

Kuna sababu nyingi zinazopelekea watu kuhama au kuzikimbia nchi zao, ili kutafuta hifadhi na nafuu ya maisha Barani Ulaya; mambo ambayo yanapaswa kugusa na kutikisa dhamiri za watu. Uhamiaji si tatizo la kutafutiwa ufumbuzi au adui anayepaswa kushikishwa adabu au uvamizi unaopaswa kupigwa vita. Mhamiaji kwanza kabisa ni mtu: mwenye utu, heshima na haki zake msingi zinazopaswa kuheshimiwa na kulindwa na wote.

Kwa wakristo, kuwapokea na kuwakarimu wahamiaji ni sehemu ya haki maadili inayopaswa kutekelezwa na wote na kwamba, hii ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wanasema katika mkutano wao huko Lithuania, wametafakari, wakaipembua dhana ya uhamiaji na kukubaliana kimsingi kwamba, kweli kuna changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na Kanisa pamoja na jamii Barani Ulaya.

Hii inatokana na ukweli kwamba, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, idadi ya watu wanaotumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo imeongezeka maradufu, hali inayolitaka Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za wahamiaji pamoja na kuwasaidia kuadhimisha Mfumbo ya Kanisa kwa lugha wanazozifahamu waamini hao. Kanisa halina budi kujikita katika Injili ya upendo na mshikamano kwa kutambua na kuthamini utu wa watu.

Wahamiaji wanapaswa kuhudumiwa kiroho na kimwili na kwamba, hii inapaswa kuwwa ni changamoto inayopewa kipaumbele cha pekee Barani Ulaya ukizingatia hali na kinzani zinazoendelea kujitokeza katika Jamii nyingi za Ulaya kuhusiana na sera za wahamiaji na wageni. Ikumbukwe kwamba, watu wana haki ya kuhama, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao na kwamba, uhamiaji ni changamoto pana sana, kuliko inavyochukuliwa na wengi.

Kanisa na Jamii Barani Ulaya, ioneshe upendo na ukarimu kwa kuwapokea na kuwahudumia wahamiaji, wakimbizi na watu wanaoomba hifadhi ya kisiasa kutokana na sababu mbali mbali kwa kuachana kabisa na ubinafsi wa kijamii ambao hauna mashiko wala ustaarabu. Kanisa litaendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa watu wanaoteseka na kunyanyasika, ili waweze kutambuliwa utu na heshima yao. Ikumbukwe kwamba, katika idadi ya wahamiaji na wakimbizi, kuna watu halisi wanaohitaji msaada wa hali na mali, mwaliko kwa waamini kushuhudia imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na majadiliano ya kina, kama sehemu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa kutambua utu na heshima ya binadamu.

Mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wahamiaji haina budi kujikita kwanza kabisa katika mchakato wa kuwapokea na kuwakirimia; kuwashirikisha katika maisha na utume wa Kanisa; kuendeleza dhana ya utamadunisho, ili kweli Injili iweze kuwa ni sehemu ya maisha na vipaumbele vya wahamiaji na wageni hawa wanapokuwa ugenini na kwamba, Kanisa liendelee kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda sanjari na ushirikiano na watu wote wenye mapenzi mema.

Maaskofu wanakaza kusema, kuna haja ya kuwashughulikia kisheria watuhumiwa wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, wanaoendelea kuwanyanyasa watu. Jumuiya ya Kimataifa iendelee kulivalia njuga baa la umaskini wa hali na kipato pamoja na kuhakikisha kwamba, haki, amani na upendo vinatawala kati ya watu. Matumizi ya mitandao ya kijamii ni nyenzo ambayo  inakuza sana tatizo la biashara haramu ya binadamu nan utumwa mamboleo. Hapa ni vigumu sana kuweza kudhibiti hali hii, kumbe, kuna haja ya kuwa na ushirikiano mpana zaidi, ili kukomesha biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.